Habari za leo rafiki yangu?
karibu kwenye makala yetu ya leo, ambapo kupitia makala hizi tunashirikishana maarifa muhimu ya kutuwezesha kuwa na maisha bora na yenye mafanikio makubwa.Watu wengi wamekuwa wakitaka kuingia kwenye biashara, lakini kikwazo chao kikubwa kimekuwa waanzie wapi. Wengi wanakuwa hawana mtaji wa kuanza biashara, licha ya kuwa na mawazo bora ya kibiashara. Wengi wamekuwa hawapo tayari kuanzia chini, na hivyo kutafuta njia ya kuwawezesha kufika malengo yao makubwa kibiashara haraka, kitu ambacho huwa hakitokei na hivyo kuwaangusha zaidi.

Leo nakwenda kukushirikisha hadithi moja kuhusu supu ya mawe, ambayo itakuonesha ni jinsi gani unaweza kutoka hapo ulipo na kupiga hatua kubwa.

Hadithi hii nimekutana nayo kwenye mtandao, ina vyanzo mbalimbali, lakini hapa nitakushirikisha kwa namna ambavyo itakusaidia wewe kuchukua hatua.

Hadithi inakwenda kwamba kwenye kijiji kimoja, mwanakijiji aliona wanajeshi watatu wakiingia kijijini, walionekana kuchoka na wenye njaa. Mwanakijiji yule alikimbia na kuwaambia watu wengine kuna wanajeshi wanavamia kijiji, hivyo wote wakimbie na kujifungia ndani na kulinda vyakula vyao. Wanakijiji wote walifanya hivyo.

Wanajeshi wale walipoingia kijijini, wakiwa na njaa kweli, walijaribu kupiga hodi kwenye kila nyumba wakiomba kupata chakula. Mwanakijiji wa kwanza aliwaambia yeye hana hata chakula chake binafsi, wa pili akawaambia chakula chake kimeisha. Walienda nyumba kadhaa na kote majibu yakawa ni hakuna chakula.

Wakiwa wanafikiria wafanye nini, mmoja akawaambia wenzake kwamba ana wazo, akawaambia tutengeneze supu ya mawe. Basi wakapiga hodi kwa mwanakijiji mmoja, wakamwambia wanaomba chungu na kuni ili waandae supu ya mawe. Mwanakijiji yule kwanza alishangaa, supu ya mawe! Akajiambia kimoyomoyo, ngoja niwape nione hiyo supu ya mawe inakuwaje.

Basi walipewa chungu na kuni, wakawasha moto, wakachukua mawe matatu pamoja na maji wakayasafisha, wakaweka kwenye chungu, wakafunika na kukaa kusubiri supu iive. 

Basi habari zilianza kusambaa kijiji kizima, kwamba kuna wanajeshi wanaandaa supu ya mawe. Kwa kuwa lilikuwa jambo ambalo halijazoeleka, wasi wanakijiji walijikusanya pale kushuhudia supu hiyo ya mawe inakuwaje.

Wakiwa wamekaa pale, mwanajeshi mmoja akasema, supu hii ingekuwa tamu sana kama tungepata viazi, supu na viazi vinaendana sana. Mwanakijiji mmoja akasema ninavyo viazi, ngoja nikachukue. Mwanajeshi mwingine pia akasema tukipata karoti na hoho, supu hii itakuwa tamu zaidi, wanakijiji wengine wakaenda kuchukua karoti na hoho. Baada ya muda mfupi, kila mwanakijiji alijikuta anatoka na kwenda kuleta kiungo ambacho kitaifanya supu kuwa tamu zaidi. Supu ile ilipata kila aina ya kiungo.

Baadaye wanajeshi wale walisema supu imeshakuwa tayari, leteni vyombo tule, na kweli supu ile ilikuwa tamu sana, na kila mwanakijiji akasema supu ya mawe ni tamu mno.

Kitu ambacho hawakujua ni kwamba, yale mawe hayajachangia chochote kwenye supu, bali viungo ambavyo kila mmoja amechangia, ndiyo vimefanya supu iwe tamu.

Je unawezaje kuitumia hadithi hii kwenye maisha yako?

Kama umenifuatilia vizuri tangu mwanzo utakuwa umeshaanza kuona jinsi ya kutumia hadithi hii. Unaweza kuitafsiri vyovyote utakavyo, lakini mimi nitaitafsiri na kukufundisha kitu kikubwa sana kwenye kuanza biashara.

Utakapokuwa na wazo kubwa la kibiashara, ukitegemea wengine wakusaidia kulifanyia kazi, kila utakayemwomba akusaidia atakuambia hana fedha. Wengine watakuambia maisha ni magumu, wengine watakuambia kwa sasa hawapo vizuri. Siyo kwamba kweli hawana fedha, ila wana hofu kwamba fedha zao zitapotea. Kama ilivyokuwa kwa wanakijiji, walikuwa na hofu kwamba wale wanajeshi wangeipa chakula chao chote.

Lakini unapochagua kuanza na kile ulichonacho, kuanza na wazo lako kubwa, kuweka nguvu na juhudi kubwa pale unapoanzia, kuonesha mapenzi makubwa kwenye kile unachofanya, hapa watu wataanza kukufuatilia, kukuangalia waone unaelekea wapi. Hii ndiyo supu yako ya mawe.

Watu wakishaanza kukuangalia sasa, na kukufuatilia unaelekea wapi, hapo sasa ndipo unaweza kuwashawishi wakaweka mtaji zaidi, wakakusaidia rasilimali ulizokosa, wakakuunganisha na watu unaowahitaji ila hawakujui na unaweza kuwajua kupitia wao. 

Utapata kila aina ya msaada kwa sababu unaonekana kuna kitu unafanya.

Mwishoni biashara inakuwa na mafanikio na kila mtu anasema umeweza kukuza biashara kubwa, wengi wasijue kuna michango ya wengi imekufikisha pale.

Unahitaji kuwa na supu ya mawe ambayo unaiandaa, supu hii ya mawe ni kile kilichopo ndani yako, ambacho kwa nje kinaonekana hakiwezekani, lakini wewe upo tayari kupambana kuhakikisha kinawezekana. Supu hii ya mawe ni kuamini kwako kwenye lile wazo ulilonalo, kuwa na ndoto kubwa, kuwa na mapenzi makubwa mno kwenye ile biashara unayowaambia watu unataka kufanya. Pia kuweza kuanzia pale ulipo, kuweka kazi kubwa zaidi ya wengine. Kila mtu anapokuona kwenye hali hiyo, anakuwa tayari kuleta mawazo bora zaidi, fedha, watu na mengine unayohitaji ili kukamilisha biashara yako.

Nimekuwa nasema mara zote, kusema tu una wazo la biashara hakutawafanya watu wahangaike na wewe, wapo wengi mno wenye mawazo, ila pale unapochukua hatua na watu wakaanza kuona kumbe kweli unamaanisha, watajileta wenyewe kukusaidia.

Swali langu kwako rafiki yangu ni moja tu; SUPU YAKO YA MAWE NI NINI?

Jipe jibu la swali hili, na kama hujaanza kuiandaa supu hiyo, chukua chungu na kuni, kisha anza kupika supu yako ya mawe. Watu watakufuata pale ambapo kuna kitu unafanya, watakukataa pale unapokuwa na maneno pekee, kama tulivyoona kwa wanajeshi kwenye hadithi hii.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,

Kupata blog yako ya kitaalamu, unayoweza kuitumia kutengeneza kipato, BONYEZA maandishi haya.

Kama umejifunza kupitia makala hii karibu tujifunze zaidi kupitia KISIMA CHA MAARIFA, ambapo utaingia kwenye kundi la wasap na kupata mafunzo kila siku. Bonyeza maandishi haya kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Pata kitabu BIASHARA NDANI YA AJIRA ujifunze jinsi unavyoweza kuanzisha na kukuza biashara yako, pia utajifunza mifereji nane(08) ya kipato unayopaswa kuwa nayo ili kufikia uhuru wa kifedha. Bonyeza maandishi haya kupata kitabu.