Uchumi wa nchi yoyote ile, unaweza kuvurugwa na mambo madogo sana yanayotokea ndani ya nchi na hata nje ya nchi. Maamuzi ya viongozi wa nchi yanachangia sana kwenye kuboresha au kuharibu uchumi wa nchi.

Mambo yanayoendelea duniani pia yanaathiri sana uchumi wa nchi nyingi. Vitu kama vita, mabadiliko ya bei za mafuta na mdororo wa uchumi kwenye nchi moja, vinaweza kuathiri uchumi wa nchi nyingine.

Mchumi na mwandishi Tim Harford anatushirikisha kwenye kitabu chake cha The Undercover Economist Strikes Back, anatushirikisha hatua ambazo zikichukuliwa zinaweza kuboresha uchumi uliodorora na zile ambazo zikichukuliwa zinazidi kuharibu uchumi.

undercover economist strikes back

Karibu tujifunze mambo muhimu kuhusu uchumi wa nchi kupitia uchambuzi wa kitabu hichi.

 1. Uchumi wa nchi unapimwa kwa jumla ghafi ya bidhaa zinazozalishwa kwenye nchi kwa mwaka husika (Gross Domestic Product – GDP). Hii inapima thamani ya vitu vyote vilivyozalishwa kwenye nchi ndani ya mwaka husika. Ukichukua thamani hiyo na kuigawa kwa idadi wa watu kwenye nchi husika, unapata wastani wa uzalishaji ambao mtu anafanya kwa mwaka, japo haufanani kwa watu wote.
 2. Kipimo cha uchumi cha bidhaa zilizozalishwa kwa mwaka (GDP) hakiwezi kupima utajiri nchi au wa mtu mmoja mmoja kwenye nchi. Kinaweza kupima uzalishaji na mwenendo wa kiuchumi. Hivyo kupima utajiri inahitajika njia tofauti, ambayo itakuwa ngumu na yenye changamoto kujua kwa uhakika.
 3. Mdororo wa uchumi ni pale ambapo uzalishaji wa nchi(GDP) unashuka kwa miezi michache. Anguko la uchumi ni pale uzalishaji wa nchi (GDP) unaposhuka na kusimama kwa miaka.
 4. Ni kawaida kwa nchi kuingia kwenye mdororo wa kiuchumi katika kipindi fulani, na hatua zinazochukuliwa na viongozi zinaweza kuiondoa nchi kwenye mdororo au zikazidisha mdororo huo zaidi.
 5. Mdororo wa kiuchumi una madhara mengi kwa nchi na kwa watu pia. Unachangia ongezeko la watu ambao hawana ajira, kwa sababu kama hakuna uzalishaji hakuna ajira. Pia mdororo wa uchumi unapelekea maisha ya watu kuwa magumu, watu kukosa furaha na kutokujiamini.
 6. Mdororo wa uchumi umekuwa unazalisha viongozi wabaya na madikteta duniani. Hii ni kwa sababu wakati wa mdororo watu wanakosa matumaini na hivyo akijitokeza mtu mmoja wa kuwapa matumaini hata kama siyo ya kweli, wanamwamini. Mfano mzuri ni anguko kubwa la uchumi (The Great Depression) lililotokea mwaka 1929 ambalo lilipelekea kuibuka kwa madikteta kama Hitler na kupelekea vita vya pili vya dunia.
 7. Yeyote anayefikiri kuendesha uchumi kunahitaji akili ya kawaida (common sense) anajidanganya na anajiandaa kuangusha uchumi. Kuendesha uchumi siyo sawa na kusema 1 + 1 = 2, kuna mambo mengi yanayogusa uchumi, kiasi kwamba ukigusa eneo moja, linaathiri eneo jingine na jingine na jingine zaidi. Hivyo lazima viongozi wawe makini sana wanapofanya maamuzi ya kiuchumi, kwani nia njema inaweza kupelekea uchumi kudorora.
 8. Mdororo wa uchumi unaosababishwa na kukosekana kwa uhitaji (demand). Zipo hali ambazo zinaweza kupelekea mdororo wa uchumi, na moja wapo ni watu kutokuwa na uhitaji au wana uhitaji lakini hawawezi kumudu kupata kile wanachotaka. Hapa uzalishaji unakuwepo lakini watumiaji hakuna, hili linapelekea uzalishaji kushuka na uchumi kudorora.
 9. Mdororo wa uchumi unaosababishwa na kupungua kwa uzalishaji. Aina ya pili ya mdororo wa uchumi ni pale ambapo uzalishaji unapungua, au ulipo haukidhi mahitaji ya watu. Katika hali hii, watu wanahitaji vitu, lakini hawavipati. Aina hizi mbili za mdororo wa uchumi zina suluhisho tofauti, hivyo njia moja haiwezi kutatua kila changamoto ya kiuchumi. Kabla ya kuchukua hatua ya kuinua uchumi, ni muhimu kujua mdororo ni kwa upande wa uhitaji (Demand) au upande wa uzalishaji na usambazaji (Supply).
 10. Gharama zisizobadilika pia zinachangia mdororo wa uchumi. Kwa mfano pale ambapo uhitaji umekuwa mdogo, wauzaji wangeweza kushusha bei ili watu wengi zaidi waweze kupata, lakini kuna hali zinazuia kupandishwa huko kwa bei. Hivyo kunakuwa na mkwamo wa uchumi, kwa sababu bei haziwezi kubadilika na watu hawawezi kumudu kile wanachotaka.
 11. Kuondolewa kwa dhahabu kama kipimo cha thamani (fedha). Zamani kipimo cha thamani ilikuwa dhahabu, dhahabu ile halisi. Hivyo ili kuipata lazima gharama kubwa itumike kuchimba dhahabu, kuisafisha kisha kupata hizo fedha. Hii ilifanya mdororo wa uchumi kuwa mkali zaidi. Kwa sababu moja ya njia za kuinua uchumi ni kuongeza fedha kwenye mzunguko, ni vigumu kupata dhahabu ya kuongeza kwenye mzunguko kwa urahisi. Sasa nchi zote zimeondoka kwenye viwango vya dhahabu na inatumia fedha za noti, ambazo ni rahisi kuchapa na kuingiza kwenye uchumi kama uchumi unadorora.
 12. Ili kitu kikubalike kuwa sarafu inayotumika kwenye uchumi, kinahitaji kukidhi mambo haya matatu;

Moja; kama njia ya kubadilishana thamani, mtu atoe thamani na apewe kile ambacho kinatumika kama sarafu ya fedha.

Mbili; uhifadhi wa thamani, kwamba unaweza kununua kitu sasa na kuja kukiuza baadaye kwa thamani kubwa zaidi.

Tatu; kipimo cha uhasibu, lazima iweze kutumika katika mahesabu ya mapato na matumizi.

Vitu vingi vimewahi kutumiwa kama sarafu kwenye jamii tofauti, kuanzia dhahabu, chumvi, mawe adimu, maua, na vingine vingi. Lakini vyote vimekuwa na changamoto mbalimbali.

SOMA; UCHAMBUZI WA KITABU; THE SMALL BUSINESS BIBLE (Kila Kitu Unachopaswa Kujua Ili Kufanikiwa Kwenye Biashara Ndogo).

 1. Fedha za kidigitali (cryptocurrency) kama Bitcoin ni vigumu kuwa sarafu inayotumika na watu wote kwa sababu zinabadilika kwa haraka sana. fedha hizi hazina utulivu unaohitajika kwenye uchumi ili kuweza kuwa njia ya kubadilishana thamani, kuhifadhi thamani na kipimo cha uhasibu. Mwandishi anasema kwamba fedha hizi zitaendelea kuwepo kwa sababu wapo wanaozipenda, kama ambavyo wapo watu ambao wanahifadhi fedha zao kama dhahabu, lakini hazitakuwa fedha zinazotumika kiuchumi.
 2. Mfumuko wa bei unaodhibitika ni mzuri kwa uchumi. Mfumuko wa bei ni kitu ambacho watu wamekuwa wanakipigia kelele kwamba kinafanya maisha kuwa magumu. Lakini mfumuko wa bei unaoweza kudhibitiwa ni muhimu ili uchumi uweze kukua. Kwa mfano mfumuko wa bei wa asilimia chini ya 2 kwa mwaka ni mzuri, kwa sababu unachochea shughuli za kiuchumi. Unaongeza riba na bei ya vitu hivyo watu kuhamasika kununua na kutumia fedha zaidi kitu ambacho kinaendesha uchumi.
 3. Mdororo wa bei ni hatari sana kwa uchumi. Bei za vitu zikishuka, uchumi unadorora, hii ni kwa sababu riba zinashuka, hivyo watu wengi hawasukumwi kutumia fedha. Pia bei za vitu vinaposhuka, watu wanachelewa kufanya maamuzi ya kununua wakiamini bei zinashuka zaidi, hali hii inapelekea watu kutokununua na uchumi kushuka zaidi.
 4. Kuchapa fedha kunakodhibitiwa ni njia ya kuchangamsha uchumi. Pale ambapo uchumi unadorora kwa sababu za uhitaji (demand) serikali inaweza kuchapa fedha na kuziingiza kwenye uchumi, hii itasaidia watu kupata nguvu ya kuweza kununua. Lakini hili linapaswa kufanywa kwa umakini sana kwa sababu linaweza kupelekea mfumuko wa bei kuwa mkubwa na watu wakawa na fedha nyingi zisizo na thamani.
 5. Njia nyingine ya kuchangamsha uchumi, hasa ule ambao unatokana na uzalishaji kuwa mdogo ni serikali kutoa mpango wa kuchochea uchumi, ambapo fedha zinaingizwa kwenye miradi mbalimbali ili iweze kuzalisha zaidi. Badala ya fedha kuingia kwenye mzunguko moja kwa moja, fedha zinawekwa kwenye miradi, na uzalishaji unaongezeka kitu ambacho kinainua uchumi.
 6. Mfumuko wa bei usiodhibitika ni matokeo ya utawala kukosa fedha za kuendesha nchi, kama vile kulipa mishahara, kugharamia huduma za kijamii. Hapa serikali inalazimika kuchapa fedha, na kadiri inavyochapa ndivyo uhitaji unakuwa mkubwa zaidi. Hapo ndipo serikali inajikuta ikiendelea kuchapa fedha zaidi na zaidi na zinazidi kushuka thamani kadiri zinavyochapwa. Hii imetokea kwa nchi kama Zimbabwe ambapo thamani ya fedha ilishuka sana kutokana na uchapaji wa fedha.
 7. Ukosefu mkubwa wa ajira ni dalili za uchumi kudorora. Na ukiingia ndani zaidi unaweza kuona tatizo la ukosefu wa ajira ni la aina mbili. Kuna watu ambao hawana ajira, ila wanaajirika, hawa ni wale ambao wameondoka kwenye kazi ndani ya muda mfupi. Na wapo watu ambao hawana ajira na hawaajiriki, hawa ni wale ambao wameondoka kwenye mfumo wa ajira kwa muda mrefu. Kadiri watu wengi wanavyokuwa hawana ajira na hawaajiriki, ndivyo uchumi unavyokuwa umedorora zaidi.
 8. Wakati mzuri wa kudhibiti matumizi, kulipa madeni na kuchangamsha uchumi, ni wakati ambapo uchumi upo vizuri. Lakini viongozi wengi hujisahau pale uchumi unapokuwa unakwenda vizuri, na kuja kustuka pale mdororo wa uchumi unapoanza. Wakati wa mdororo wa uchumi ni wakati mbaya sana kudhibiti matumizi na kulipa madeni, huo ndiyo wakati ambapo jitihada za kuchochea uchumi zinapaswa kufanyika zaidi.
 9. Jinsi Henry Ford alivyotengeneza nidhamu ya kazi na tatizo la ukosefu wa ajira. Wakati wa zama za mapinduzi ya viwanda. Kazi za viwandani zilikuwa zinapatikana kwa urahisi, muda wa kufanya kazi ulikuwa mrefu na malipo yalikuwa kidogo. Hivyo watu hawakuwa na nidhamu na kazi, watu walienda kazini siku waliyojidikia, wasipojisikia hawaendi, na wakikosa kazi kwenye kiwanda kimoja, ni rahisi kupata kwenye kiwanda kingine. Henry Ford, aliyekuwa na umiliki mkubwa kwenye kiwanda cha magari, aliona ni vigumu kuendesha kiwanda katika mazingira hayo. Hivyo alichukua maamuzi ambayo hakuna aliyeyategemea wala kuyaelewa. Alichofanya ni kuongeza malipo mara mbili, na kupunguza masaa ya kazi. Kitu ambacho kilifanya watu wengi kwenda kuomba kazi kwenye viwanda vyake. Kwa kuwa uhitaji ulikuwa mkubwa kuliko nafasi za kazi zilizokuwa zinapatikana, watu wengi walikosa kazi, lakini hawakuwa tayari kwenda kufanya kazi kwingine ambapo bei ni ndogo. Hii ilifanya wale wanaopata kazi waifanye vizuri, waithamini na kujituma zaidi kwa sababu wakiondoka, wapo wengine wengi wanahitaji kazi hiyo. kwa njia hii alitengeneza nidhamu ya kazi na pia kuongeza tatizo la ukosefu wa ajira, kwa sababu watu walikataa kufanya kazi za bei ya chini hata kama zilikuwa zinapatikana.

Kuendesha uchumi wa nchi ni zoezi gumu, zoezi ambalo linahitaji umakini mkubwa sana. Zoezi hili linakuwa gumu zaidi pale ambapo wanaofanya maamuzi ni wanasiasa na siyo wataalamu wa uchumi. Kwa sababu wanasiasa wanaweza kufanya maamuzi yatakayowaletea sifa za muda mfupi, lakini yakaharibu uchumi kwa muda mrefu.

Fanyia kazi haya ambayo umejifunza kwenye uchambuzi wa kitabu hiki ili uweze kuona matokeo bora kwenye maisha yako.

Kupata vitabu vya Kiswahili vya kujisomea ili kuweza kufanikiwa kwenye kazi, biashara na maisha kwa ujumla, tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.kisimachamaarifa.co.tz