Wataalamu wa ujenzi ni watu ambao wamefunzwa vizuri kwa lengo la kutoa huduma bora za ujenzi kwa jamii inayowazunguka, ni watu waliobobea kwenye fani mbalimbali zinazohusu ujenzi na taratibu zake. Maendeleo ya teknolojia na mapinduzi ya viwanda yanayotokea duniani yamechangia kwa kiasi kikubwa mabadiliko ya ukuaji na maendeleo ya sekta ya ujenzi duniani ikiwemo Tanzania. Kama ilivyo kwenye sekta nyingine kuwa na wataalamu wake, pia sekta ya ujenzi ina wataalamu wake ambao wamebobea kwenye fani tofauti zinazohusu ujenzi, leo tuna wataalamu wengi wa fani mbalimbali za ujenzi ambao wakitumika vizuri watakuwa chachu ya mabadiliko na maendeleo ya watu binafsi na nchi kwa ujumla. Baadhi ya fani tulizonazo kwa sasa ni wabunifu na wasanifu majengo, wahandisi majenzi, wakadiriaji majenzi, wasimamizi majenzi na wapambaji wa majengo. Wengi wamejikita kwenye ujenzi wa majengo na miundombinu na baadhi wanatoa elimu na ushauri kwa watu binafsi, kampuni na taasisi mbalimbali. Hawa ni watu muhimu sana kwa hatua zote za maendeleo ya mtu binafsi na hata kwa nchi. Wakati tulionao sasa ni muhimu sana kuwatumia wataalamu kwenye ujenzi wako ili uwe salama na upate kilicho bora.

majengo 34.jpg

Pamoja na uwepo wa wataalamu wengi wa ujenzi, lakini bado idadi kubwa ya watanzania hawajafahamu umuhimu wa kuwatumia kwenye shughuli zao za ujenzi. Hali hii ndiyo inayochangia ujenzi holela na matokeo yake ni nyumba nyingi kuwa sehemu ambazo si salama na zisizo kidhi viwango. Nyumba bora ni haki ya kila binadamu, ni hitaji la lazima kwa kipindi cha uhai wa maisha yake yote. Maisha hayana thamani kama hutakuwa na mahali safi, bora na salama kwa ajili ya makazi na shughuli zote za kiuchumi na kijamii katika kujiletea maendeleo yako binafsi na kwa jamii yote. Leo nitaelezea baadhi ya faida utakazo nufaika nazo endapo utatumia wataalamu kwenye ujenzi wa nyumba yako.

SOMA; Fahamu Hatua Tano (05) Muhimu Za Kuzingatia Kabla Hujaanza Kuwekeza Kwenye Ardhi Na Majengo.

Ubora Wa Nyumba Na Matumizi Ya Muda

Wataalamu wa ujenzi ni watu wanaozingatia sana ubora wa nyumba na majengo mbalimbali wakati wa ubunifu na wakati wa ujenzi. Hii ndiyo sababu kubwa inayokulazimu uwatumie wataalamu kwa kuwa nyumba ni kitu kinachogusa uhai na maendeleo ya maisha yako. Changamoto mbalimbali za ubora wa malighafi, matumizi ya rasilimali fedha na muda ambazo wanakutana nazo baadhi ya marafiki ni matokeo hasi ya kutokutumia wataalamu. Mabadiliko ya sasa yanatulazimisha kuwa na nyumba bora na za kisasa ambazo ubora wake ni matokeo ya kutumia wataalamu wa fani husika kwenye kila hatua ya ujenzi.  Epuka hasara ya matengenezo ya mara kwa mara kwa kuamua kutumia wataalamu kabla na wakati wa ujenzi.

Usalama Na Maarifa

Watanzania wengi bado hawajatambua thamani na umuhimu wa wataalamu wa ujenzi, ni watanzania wachache tu ndiyo wametambua  umuhimu wa kuwatumia wataalamu wa ujenzi kupitia vyanzo mbalimbali vya taarifa. Mtaalamu wa ujenzi ana maarifa ya ziada ambayo ni tofauti na mtu aliye nje ya fani ya ujenzi ambayo atayatumia kuhakikisha anakidhi malengo yako kwa uhakika na usalama usio na shaka. Ujenzi unatumia sana michoro ambayo ni chanzo kikuu cha mawasiliano na maamuzi yote, sio kila mtu anaweza kutafsiri lugha ya ujenzi kwenda kwenye uhalisia. Epuka majanga ya bomoabomoa na misuguano toka mamlaka za ujenzi kwa kutumia wataalamu wa fani husika. Ujenzi wako utakuwa bora na salama kwa kuwa utakuwa unatekelezwa na mtaalamu mwenye uzoefu na maarifa ya kutosha kwenye kile anachokifanya.

Ushauri Na Usimamizi Bora

Mara nyingi sana nimesisitiza kuwaona wataalamu kabla ya kufanya chochote kwa ajili ya ujenzi wako. Wazo lako la kutaka kufanya ujenzi linapaswa kuwa sababu pekee ya wewe kuwatafuta wataalamu wa ujenzi, lengo kuu ni kupata ushauri na kufahamu taratibu mbalimbali zitakazo kuwezesha kufanya ujenzi wako pasipo na tatizo lolote la kiutendaji. Changamoto kubwa iliyopo hapa ni watu wengi kuwa wasimamizi wa ujenzi ingawa hawana maarifa yoyote ya ujenzi, ni hatari kwa kuwa watashauri na kusimamia kitu wasichokijua vizuri. Usisubiri ukwame au uharibifu utokee ndiyo iwe sababu ya kuwatafuta wataalamu, ni hatari na itakugharimu sana. Ni muhimu sana ukapata mtaalamu atakayekuwa dira kwenye kila hatua utakazopitia kwenye ujenzi wako. Naamini atakuwa rafiki na mshauri wako katika kutimiza malengo yako ya kuwa na nyumba bora na yenye mwonekano wa kisasa.

SOMA, Mambo Muhimu Ya Kuzingatia Ili Kuepuka Nyufa Kwenye Nyumba Yako Pale Unapokutana Na Udongo Wa Mfinyanzi.

Ni Ngao Dhidi Ya Majanga

Marafiki wengi wamejikuta wakiingia kwenye matatizo wakati wa ujenzi pasipo kutarajia. Wengi hujikuta wakikabiliana na changamoto za kiutendaji na misuguano toka mamlaka husika kutokana na sababu mbalimbali, changamoto hizi huwaweka katika wakati mgumu wa kifikra na kimaamuzi, haya ni matokeo hasi kwa kuwa marafiki wengi bado hawajafahamu vizuri taratibu za ujenzi. Ujenzi wa kisasa una changamoto nyingi sana tofauti na ujenzi wa wakati uliopita, hivyo ni muhimu sana kuwa na mtaalamu wa ujenzi atakaye kupatia ushauri na mbinu za kukabiliana na hatari zozote zitakazojitokeza kwenye ujenzi wako. Epuka msongo wa mawazo kwa kuwa karibu na mtaalamu wa ujenzi katika kukabiliana na changamoto za ujenzi. Mtaalamu wako atakuwa ni ngao, msimamizi, mtendaji na msemaji wa mambo yote yanayohusu ujenzi wako dhidi ya mamlaka na taasisi zote zinazosimamia ujenzi kwa kuwa wajenzi huzungumza lugha inayofanana ambayo ni tofauti na fani nyingine.

Ni Msaada Kwa Ukuaji Wa Mji

Wataalamu wa ujenzi ni wadau wa utekelezaji katika mipango mbalimbali ya upangaji miji na vijiji na maendeleo ya miundombinu ambayo ni kichocheo kikubwa kwa maendeleo ya sekta nyingine. Ni fani yenye ukaribu sana na wataalamu wa sekta mbalimbali ikiwemo ardhi, sheria, mazingira, nishati na madini katika kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi unaotakiwa. Matatizo tuliyonayo kwa sasa ikiwemo ya kuwa na miji na vijiji holela ambavyo ni hatari kwa maisha ya watu ni matokeo hasi ya kutokutumika vizuri kwa wataalamu hawa. Usimamizi hafifu wa fani hizo ni hatari kwa maendeleo ya nchi kiuchumi, kijamii na kisiasa kwa kuwa kutakuwa na jamii inayoishi kwenye mazingira ya hatari wakati wote, hii ni hasara kubwa kwa kuwa rasilimali fedha na muda zitakuwa zinatumika kwenye kukabiliana na matokeo hasi yatokanayo na kuwa na makazi yasiyo rasmi na salama kwa watu na viumbe wengine.

Tafakari yako kuhusu Makala hizi ni muhimu sana…..!!!! maoni na maswali yako ni mambo ambayo nayazingatia sana. Usisite kuwasiliana nami endapo dhamira yako itakusukuma kufanya hivyo. Karibu sana.

 

Tuendelee kuwa pamoja kupitia AMKA MTANZANIA tufike kwenye kilele cha mafanikio, pia endelea kufuatilia makala zijazo ili ujifunze zaidi.

Mwandishi wa makala hii ni mwanataaluma wa ujenzi.

Anapatikana kwa: Simu: +255 685 729 888

Baruapepe: kimbenickas@yahoo.com