Mafanikio yako ni matokeo ya thamani unayoongeza kwa wengine. Kadiri unavyoongeza thamani kubwa ndivyo unavyojitengenezea mafanikio makubwa zaidi.

Sasa changamoto ni moja, mara nyingi watu huwa hawajui wanataka nini mpaka pale wanapokipata. Kwa mfano kabla hatujawa na simu janja (smartphone) watu hawakuwahi kusema kwamba wanahitaji aina hizi za simu. Lakini baada ya simu hizi kuja, watu wanazitaka na wanataka ambazo ni bora zaidi na zaidi.

IMG-20170217-WA0007

Hii ni kusema kwamba, chochote unachofanya, njia pekee ya kufanikiwa ni kuwapa watu kile ambacho kwa sasa hawakijui, ila wakikijua, hawawezi kuishi bila ya kitu hicho.

Ikimaanisha kwamba, kama unachowapa watu ni kile ambacho walikuwa wanategemea kupata kutoka kwako, basi hakuna kikubwa ambacho unafanya.

Kama watu wakipata unachotoa, hawawezi kutofautisha na wanachopata kwa wengine, uwepo wako hauna umuhimu.

Kuna haja gani ya wewe kuwepo kama unachotoa kinaweza kupatikana kwa wengine 100 wanaofanya kile unachofanya?

SOMA; UKURASA WA 594; Njia Ya Uhakika Ya Kujulikana Na Wengine…

Wape watu kile wanachotegemea, lakini nenda zaidi kwa kuwapa ambacho hawategemei kupata.

Kwenye kila unachofanya, nenda hatua ya ziada, fanya zaidi ya ulivyozoea, wape watu zaidi ya walichotegemea kupata. Utashangaa na wao wanakulipa zaidi ya walivyozoea kupita na utafanikiwa zaidi ya ulivyozoea kufanikiwa.

Fanya zaidi ya mategemeo ya wengine wote, fanya zaidi ya ulivyozoea kufanya na utakuwa na wachache sana wa kukusumbua kwenye safari yako ya mafanikio.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog