Ipo misukumo ya aina mbili kwenye jambo lolote unalofanya kwenye maisha yako.

Msukumo wa kwanza ni kwa sababu inabidi ufanye. Hapa ni pale unapofanya kitu kwa sababu huna namna nyingine, inakubidi tu ufanye, hata kama hutaki au hupendi kufanya. Kufanya kwa sababu inakubidi ufanye, mara nyingi hakuleti matokeo bora kabisa, kwa sababu wengi hawafanyi kutoka moyoni.

Msukumo wa pili ni kwa sababu umechagua kufanya. Hapa ni pale unapofanya kitu kwa sababu umechagua wewe mwenyewe kufanya, kwa sababu ndiyo kitu muhimu sana kwako kufanya na upo tayari kukifanya kwa ubora. Unapofanya kwa sababu umechagua kufanya, unapata matokeo bora sana kwa sababu unafanya kutoka moyoni.

Hebu jitafakari kwa nini unafanya chochote unachofanya sasa. Je ni kwa sababu huna namna inabidi tu ufanye? Au ni kwa sababu umechagua kufanya na upo tayari kufanya kwa ubora?

SOMA; UKURASA WA 982; Ni Muda Ambao Ungeutumia Kufanya Mengine Muhimu…

Dalili kwamba unafanya kwa sababu inabidi ufanye ni kutopenda unachofanya, kutaka kiishe haraka, mawazo yako kuwa sehemu nyingine na kutokuwa na hamasa ya kuboresha zaidi.

Dalili kwamba unafanya kwa sababu umechagua kufanya ni kupenda unachofanya, kuweka akili na mawazo yako yote kwenye kile unachofanya, kuwa tayari kuwasaidia watu zaidi na kile unachofanya, kujali zaidi, na kufanya kitu hicho kuwa kipaumbele kwako.

Utafanikiwa kupitia vile ambavyo umechagua kufanya na siyo kupitia vile ambavyo inabidi ufanye.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha