Watu wengi wamekuwa wanapata mawazo mazuri sana, mawazo ambayo kama watayatekeleza basi maisha yao yatakuwa bora sana.

Changamoto ni kwamba wengi wamekuwa hawatekelezi mawazo mazuri wanayokuwa nayo, wamekuwa hawachukui hatua kuyageuza mawazo hayo kuwa uhalisia.

Na kinachowazuia wengi kuchukua hatua kwenye mawazo yao, ni kusubiri.

Pale unapopata wazo, unakuwa na hamasa kubwa ya kulifanyia kazi, lakini kadiri unavyosubiri, hamasa ile inapungua mpaka inafika mahali hukumbuki tena wazo lile.

Hivyo kadiri unavyoendelea kusubiri pale unapokuwa umepata wazo zuri, ndivyo inavyokuwa vigumu kwako kuanza kuchukua hatua.

Moja ya vitu vitakavyokuwezesha kufanikiwa, ni uwezo wakufanya maamuzi haraka kwa kutumia taarifa chache unazokuwa nazo. Kwa kuwa na wazo, kisha kulifikiria kwa muda mfupi na kufanya maamuzi ya kuanza.

Na usiogope kukosea, kwa sababu mwisho wa siku kila mtu anakosea, na ni bora kukosea ukiwa unafanya kwa sababu utajifunza, kuliko kuepuka kukosea kwa kutokufanya kabisa.

Chukulia mfano wa kusoma vitabu, unaweza kusoma kitu kwenye kitabu na ukakifurahia sana, unaona jinsi ambavyo kinaweza kuyaboresha maisha yako ukichukua hatua. Lakini huchukui hatua mara moja, unasubiri, na haikuchukui muda unakuwa umesahau kabisa kile ulichojifunza.

Dawa ya kuepuka kusahau yale uliyojifunza, ni kuchukua hatua mara moja. Umejifunza kitu ambacho unaona kitayafanya maisha yako kuwa bora, chukua hatua hapo hapo.

Punguza muda unaosubiri kati ya wazo na kuchukua hatua na utaweza kufanya mengi na makubwa.

Lakini pia kuwa makini, usikimbilie kuanzisha vitu vipya kila wakati. Bali boresha zaidi yale ambayo tayari umeshachagua kufanya. Siyo kila unaposikia fursa mpya inalipa basi unakimbilia kuchukua hatua mara moja. Chagua fursa zipi utakazozifanyia kazi kwa kina, kisha jifunze njia ya kuboresha zaidi na hizo ndiyo ufanyie kazi.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha