Habari za leo rafiki yangu?

Karibu kwenye tano za juma la kwanza kabisa kwa mwaka wetu huu mpya kabisa wa 2019. Mwaka huu ni mpya na mchanga kwetu, tuna majuma 51 mbele yetu ambayo ni sisi wenyewe tunaochagua tunayatumiaje majuma haya kupiga hatua.

Karibu kwenye #TANO ZA JUMA, ambapo kwa kuuanza mwaka huu 2019 nimekuandalia mambo muhimu yatakayokuwa mwongozo kwako kwa mwaka mzima 2019. Naweza kusema hizi ni TANO ZA JUMA ambazo unapaswa kuzihifadhi mahali na urudie kuzisoma kila juma kwa mwaka mzima kwa sababu nimekuandalia mambo yatakayokusaidia kwa mwaka mzima 2019 na uwe wa mafanikio makubwa sana.

Twende kwenye sindano zetu tano za juma hili la kwanza, ambazo zitatupa dozi ya kutupeleka kwa mwaka mzima kwa mafanikio makubwa.

2019

#NENO; SALAMU ZA MWAKA MPYA 2019.

Rafiki, kwanza kabisa tushukuru kwa nafasi hii nyingine nzuri tuliyoipata, ya kuuona mwaka huu mwingine 2019. Ni wengi ambao walipanga mengi kwenye mwaka huu, lakini hawajapata nafasi ya kuuona mwaka huu. Lakini mimi na wewe tumepata nafasi hii siyo kwa ujanja wetu, bali kwa sababu bado tuna jukumu kubwa la kufanya kwenye hii dunia.

Rafiki, nenda kautumia mwaka huu 2019 vizuri, nenda katunze na kutumia vizuri muda wako na nguvu zako. Nenda kafanye mambo ya tofauti mwaka huu.

Rafiki, nataka mwaka huu 2019 kwako uwe mwaka wa vitendo, mwaka wa kuchukua hatua. Uwe mwaka wa kuweka sababu pembeni na kuchukua hatua, hata kama ni hatua ndogo sana, muhimu ni kuchukua hatua.

Rafiki, mimi nikuahidi kitu kimoja, 2019 nitaendelea kuwa na wewe bega kwa bega nikikuandalia na kukushirikisha maarifa bora sana yenye hatua za kuchukua ili maisha yako yaweze kuwa bora zaidi.

Mwaka huu 2019 nakwenda kuweka muda, nguvu na maarifa zaidi katika kukupatia maarifa bora zaidi, hivyo karibu sana tuendelee kuwa pamoja.

Pia karibu sana ujiunge na KISIMA CHA MAARIFA, ambapo tutakuwa karibu na kujifunza kwa kina zaidi. Kwa mwaka 2019 kila siku tunaianza kwa tafakari bora kabisa ya kistoa, tafakari ya kifalsafa ambayo inayafanya maisha yetu kuwa bora zaidi. Pia kila siku tunaimaliza kwa kutafakari jinsi ilivyokwenda kwetu na hatua bora zaidi za kuchukua siku inayofuata.

Kama umesubiri sana kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA, na kusema bado hujawa tayari au kufikiri hakuna kipya utakachojifunza, nakuambia jiunge leo na tusafiri pamoja kwa mwaka huu 2019. Na ikifika mwisho wa mwaka, wewe jifanyie tathmini mwenyewe, ukiona upo kama ulivyoingia, basi niandikie na niambie umekaa mwaka mzima kwenye KISIMA CHA MAARIFA na maisha yako yako vile vile. Bila ya kukuuliza swali jingine nitakwenda kukurudishia ada uliyolipa.

Nakusisitiza hivi rafiki kwa sababu naweka nguvu kubwa sana kwenye KISIMA CHA MAARIFA na najua kama haupo kwenye KISIMA basi unayakosa mengi. Ufanye mwaka 2019 kuwa wa majaribio, na kama jaribio halitalipa basi utakuwa hujapoteza chochote, kwa sababu ada utakayokuwa umelipa nitakurejeshea. Kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA tuma ujumbe kwenye wasap namba 0717396253 wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA na utatumiwa maelekezo.

Karibu sana rafiki tusafiri pamoja kwa mwaka huu 2019, nakupenda sana na nakuahidi tutaendelea kuwa pamoja katika safari hii ya kuelekea mafanikio makubwa kwenye maisha yetu.

#1 KITABU CHA JUMA; SAYANSI YA KUPATA UTAJIRI.

Rafiki, kipo kitabu kimoja ambacho nataka kila binadamu hapa duniani akisome na kukiishi kwa mwaka huu 2019. Ni kitabu kifupi sana, lakini chenye mafunzo mazito sana kuhusu fedha na utajiri. Ni kitabu chenye nguvu kubwa sana kwenye kuzibadili fikra zetu na matendo yetu na kutuwezesha kuondoka kwenye umasikini na uhaba na kwenda kwenye utajiri na utele.

Kitabu ninachoongelea hapa ni THE SCIENCE OF GETTING RICH kilichoandikwa na Wallace D. Wattles, ni kitabu ambacho kilichapwa zaidi ya miaka 100 iliyopita, lakini misingi iliyopo ndani ya kitabu hii bado inaishi mpaka leo.

Neno moja ninaloweza kukuambia rafiki yangu ni hili, kama mwaka huu utaamua kuishi kwa misingi ya kitabu hiki pekee, utaiga hatua kubwa kuliko hatua ambazo umepiga kwa miaka 10 iliyopita.

Nakusihi sana mwaka huu 2019 ishi kwa misingi ya kitabu cha THE SCIENCE OF GETTING RICH na maisha yako yatakuwa bora sana.

Na hapa nakwenda kukushirikisha misingi yote muhimu iliyopo kwenye kitabu hichi kwa kukuchambulia kwa ufupi sura zote 17 zilizopo kwenye kitabu hiki.

Karibu sana upate uchambuzi huu mzuri wa kitabu cha THE SCIENCE OF GETTING RICH na uiishi misingi hiyo kwa mwaka huu 2019.

UTANGULIZI; NI VITENDO NA SIYO FALSAFA.

Kitabu cha SAYANSI YA KUPATA UTAJIRI siyo kitabu cha kifalsafa, bali kitabu cha vitendo, ndani yake unajifunza hatua za kuchukua ambazo zinakuwezesha kufika kwenye utajiri mkubwa.

Mwandishi anatuambia kitu kimoja, tunapaswa kuyapokea yale tunayojifunza kwenye kitabu hiki kwa imani. Kukubaliana na kile tunachojifunza na kukifanyia kazi bila ya kujiambia hakiwezekani au wewe huwezi.

Hili ni muhimu sana kwa sababu tumekuwa tunajirudisha nyuma kwa kujiwekea ukomo sisi wenyewe. Chukulia kile unachojifunza kwa imani na kifanyie kazi kama kilivyo na bila ya kujaribu kukibadili kwa namna yoyote ile na utapata matokeo bora.

SURA YA 1; HAKI YA KUWA TAJIRI.

Kila mtu anayo haki ya kuwa tajiri, utajiri haujatengwa kwa ajili ya wachache na wengi kuachwa wateseke. Ni haki ya kila mtu kuwa tajiri na utajiri ni kitu kizuri.

Hakuna ubaya wowote kwenye kutaka kuwa tajiri. Sisi binadamu tunaishi kwa mwili, akili na roho, na maisha yako hayawezi kukamilika kwenye maeneo hayo matatu kama huna utajiri.

Hivyo taka kupata utajiri kwa sababu ni kitu kizuri na pia ni haki yako kuwa tajiri.

SURA YA 2; IPO SAYANSI YA KUPATA UTAJIRI.

Kupata utajiri ni sayansi kama zilivyo sayansi nyingine. Uzuri wa sayansi ni kwamba matokeo yanatabirika na ni yale yale. Mbili jumlisha mbili ni nne, na hilo litakuwa hivyo mara zote.

Kadhalika kwenye utajiri, kama utafanya kile ambacho wenye utajiri wanafanya, na wewe utapata matokeo ambayo wanapata, ambayo ni utajiri. Zipo sheria na kanuni za kupata utajiri ambazo kama mtu atazifuata, lazima atapata utajiri.

Kila mtu anaweza kuwa tajiri bila ya kujali mazingira, kipato, kipaji au hata shughuli anayofanya. Ipo namna ya kufikiria na kufanya ambayo kila mtu anaweza kuitumia na akapata utajiri mkubwa kwenye maisha yake.

SURA YA 3; JE FURSA ZIMEHODHIWA NA WACHACHE?

Hakuna mtu ambaye amezuiwa kuwa tajiri kwa sababu watu wachache wamehodhi fursa zote na kuzizuia kwao pekee. Unaweza usiweze kuingia kwenye biashara fulani, lakini fursa bado zipo nyingi ambazo unaweza kuingia na ukatengeneza utajiri mkubwa.

Zipo fura nyingi kwa yule ambaye yupo tayari kuziangalia fursa na kuzifuata.

Dunia ina utele na siyo uhaba, fursa zipo nyingi na nyingine zinaendelea kutengenezwa kila siku. Hivyo fungua macho na ziangalie fursa na uzitumie ili kufanikiwa.

SURA YA 4; MSINGI WA KWANZA KWENYE SAYANSI YA KUPATA UTAJIRI.

Fikra ndiyo nguvu pekee inayoweza kutengeneza utajiri kutoka kwenye mfumo unaoendesha ulimwengu mzima. Mfumo unaoendesha ulimwengu mzima ni mfumo wa fikra, na mfumo huu huzalisha vitu kulingana na fikra ambazo zinawekwa juu ya vitu hivyo.

Hatua ya kwanza kwako kufikia utajiri ni kuwa na fikra za utajiri unaotaka, kufikiri kile unachotaka na mfumo unaoendesha dunia nzima, utakusaidia kuleta kile ambacho unakifikiria kwa muda mrefu.

Kwa muhtasari; kuna mfumo wa kufikiri ambao kutoka kwao vitu vyote vinatengenezwa, na kwa uhalisia wake unaruhusu, kupenyeza na kuujaza ulimwengu wote.

Fikra kwenye mfumo huu inazalisha kile kilichofikiriwa.

Mtu anaweza kutengeneza kitu kwenye fikra zake na kwa kuweka fikra hizi kwenye mfumo huu, anasababisha kile anachofikiria kitengenezwe.

SURA YA 5; MAISHA YANAYOONGEZEKA.

Katika kutengeneza utajiri, unapaswa kuondokana na fikra za uhaba na kuwa na fikra za utele. Dunia haina uhaba wa kitu chochote, kila kitu kipo kwa utele wa kutosha na kikipungua kitazalishwa zaidi na zaidi.

Chukulia mfano wa samaki, kila siku binadamu tunakula samaki, na bado wanaendelea kuzalishwa zaidi na zaidi. Sisi binadamu tumekuwa tunachimba madini ya dhahabu tangu enzi na enzi, lakini bado yanaendelea kupatikana. Siyo kwa sababu hayaishi, bali kwa sababu dunia inaendelea kutengeneza kwa kadiri tunavyohitaji.

Hivyo chochote unachotaka, jua kuna utele na hakuna uhaba kwenye dunia. Mfumo wa kufikiri ambao unaiendesha dunia, utatengeneza chochote unachotaka kama utakifikiria kwa muda mrefu.

Pia kupata wewe haimaanishi ni mpaka mwingine akose, dunia ina utele wa kuweza kumpa kila mtu kila anachotaka bila ya yeyote kukosa. Ondokana na dhana ya ushindani kwamba wengine wakipata wewe umekosa. Kazana kupata unachotaka na jua wengine nao watapata wanachotaka.

SURA YA 6; JINSI UTAJIRI UNAVYOKUJA KWAKO.

Utajiri unakuja kwako kwa njia ya thamani. Unapaswa kutoa thamani kubwa zaidi ya matumizi kuliko thamani ya fedha ambayo mtu anakupa. Ili kupata zaidi lazima uwe tayari kutoa zaidi.

Usiwalangue watu, wala usitumie mbinu kuwashawishi wanunue kitu ambacho hakitawasaidia. Wape watu kitu ambacho kitakuwa na msaada kwenye maisha yao na wewe utaweza kupata kile unachotaka.

SURA YA 7; SHUKRANI.

Tumeona kwamba kuna mfumo wa fikra ambao unatupa kila ambacho tunakifikiri kwa muda mrefu. Njia pekee ya kushirikiana na mfumo huu ni kuwa na shukrani.

Kwa kushukuru, mfumo huu wa fikra unajua kwamba upo tayari kupokea zaidi na hivyo kukuwezesha kupata zaidi.

Usiwe mtu wa kulalamika au kukosa shukrani, mara zote shukuru na utaweza kupata zaidi. Shukuru kwa kidogo na utafungua milango ya kupata kikubwa zaidi.

SURA YA 8; NAMNA FULANI YA KUFIKIRI.

Hatua muhimu ya kupata kile unachotaka ni kujua kwa hakika nini hasa unachotaka. Huwezi kupata kile usichokijua, hivyo lazima ujue kwa undani kile unachotaka na kukifikiria kwa ukamilifu wake ndiyo uweze kukipata.

Unapaswa kutengeneza picha kwenye fikra yako ya kile unachotaka, kwa namna unavyokitaka kisha weka picha hii kwenye fikra zako mara nyingi. Kila unapokuwa na muda ambao huna kazi, tumia muda huo kufikiria picha hiyo na kujiona tayari umeshapata kile unachotaka.

Unapoifikiria picha ya kile unachotaka, unapaswa kuwa na imani kwamba tayari umeshakipata kwa namna unavyokitaka. Ona kama tayari unacho. Kwa njia hii, mfumo wa fikra unaoongoza dunia utakuwezesha kupata kile unachotaka.

SURA YA 9; JINSI YA KUTUMIA MATAKWA YAKO.

Katika kutumia sayansi ya kupata utajiri, hupaswi kutumia matakwa yako kwa kitu chochote kilichopo nje yako. Usitumie nguvu ya matakwa yako kuwaendesha wengine kama unavyotaka wewe.

Sayansi ya kupata utajiri haitaki wewe uingilie maisha ya wengine, na pale unapofanya hivyo, kwa kutumia matakwa yako kuingilia maisha ya wengine, unaharibu mfumo mzima unaopaswa kutengeneza utajiri kwako. Kadiri unavyohangaika na ya wengine, ndivyo unavyopoteza ya kwako.

Tumia nguvu ya matakwa yako katika kufikiri na kutenda kwa namna ambayo itakuwezesha wewe kupata kile unachotaka. Na katika kuweka nguvu ya matakwa yako kwenye kupata utajiri, usijihusishe kwa namna yoyote na umasikini, usiufikirie umasikini, usitake kujua kwa nini watu ni masikini na wala usisome au kusikiliza vitu vinavyoeleza kuhusu umasikini. Ukatae umasikini kabisa na fikra zako zielekeze kwenye namna bora ya kufikiri ili kutengeneza utajiri.

SURA YA 10; MATUMIZI ZAIDI YA MATAKWA YAKO.

Huwezi kutengeneza na kutunza maono ya utajiri kama unahamisha mawazo yako kwenda kwenye picha inayokinzana mara kwa mara. Hupaswi kufikiria kitu kinachopingana na utajiri unaotaka kwenye maisha yako. Muda wako wote fikiria ile picha ya utajiri uliyojitengenezea.

Usizungumzie kuhusu umasikini uliokuwa nao au wazazi wako waliokuwa nao, usizungumzie kuhusu hali mbaya ya uchumi au mabaya yoyote yanayoendelea. Hata kama mambo ni magumu kiasi gani, hayo yanapita, hayadumu milele. Hivyo usiharibu fikra zako kwa kuyafikiria au kuyazungumzia.

Peleka mawazo na akili zako zote kwenye utajiri na ipe picha unayotaka kufikia na waache wengine wahangaike na hayo mengine.

SURA YA 11; NAMNA FULANI YA KUTENDA.

Fikra zina nguvu kubwa sana ya kuumba, pale unapofikiri kwa namna fulani, unatumia nguvu ya mfumo wa fikra unaoongoza dunia katika kukuletea kile unachotaka. Lakini kile unachotaka hakitatokea kwa muujiza, badala yake kitatokana na matendo na hatua unazochukua.

Ipo namna fulani ya kutenda ambayo inakuwezesha kupata kila unachotaka kwenye maisha yako. Na bila ya kuchukua hatua kwa namna fulani, hata kama ungekuwa na fikra bora kiasi gani, hazitaweza kuleta unachotaka.

Chochote unachokitaka sasa, kipo kwenye mikono ya wengine, na ili hao wengine wakupe hicho unachotaka, lazima wewe uwape kwanza kile wanachotaka. Hivyo lazima uwe na namna bora ya kuchukua hatua, namna inayoendana na fikra ulizonazo na kuchukua hatua ukiwa na imani na uhakika wa kupata unachotaka na utakipata.

Unapaswa kuchukua hatua sasa, kwa kuweka nguvu zako zote kwenye kile unachofanya kwa wakati huo, usifikirie kuhusu jana wala kesho, badala yake fikiria kuhusu kile unachofanya kwa wakati husika, hili litakuwezesha kufanya vizuri kile unachofanya.

SURA YA 12; HATUA ZENYE UFANISI.

Kama pale ulipo sasa hapakuridhishi, kama unataka kupiga hatua zaidi kwenye maisha yako na kwa kile unachofanya, unapaswa kukua zaidi ya pale ulipo sasa. Unapaswa kuijaza ile sehemu uliyopo sasa kiasi kwamba hakuna tena nafasi kwa ajili yako na hivyo inakubidi ukue zaidi.

Chochote unachofanya sasa kifanye kwa viwango vya juu sana kuliko ilivyozoeleka. Na unapofanya kwa viwango vya juu, mfumo wa fikra unaoendesha dunia utakupeleka kwenye hatua za juu kuliko hapo ulipo sasa.

Kila siku fanya kile unachopaswa kufanya bila ya kuahirisha, na kifanye kwa ufanisi mzuri. Usifanye kitu chochote kwa haraka au njia ya mkato. Mafanikio kwenye maisha ni kufanya vitu kwa ufanisi wa hali ya juu.

Kwa kila hatua unayochukua, kuwa na picha ya matokeo unayotaka kupata na fikiria picha hiyo mara zote. Hili litaweka fikra zako kwenye kile unachofanya na utaweza kupata matokeo bora.

SURA YA 13; INGIA KWENYE BIASHARA SAHIHI KWAKO.

Biashara au kazi yoyote inayo uwezo wa kutengeneza utajiri mkubwa kwa mtu yeyote. Lakini siyo kila aina ya biashara au kazi itaweza kutengeneza utajiri kwako.

Utapata utajiri na kufanikiwa kwa kuingia kwenye kazi au biashara ambayo inaendana na wewe. Biashara ambayo inatumia vipaji na uwezo mkubwa uliopo ndani yako.

Utafanikiwa zaidi kwa kufanya kile unachopenda na unachojali, kwa sababu utafanya kwa kupenda na siyo kufanya kama kazi.

Jua kipi unapenda na kujali na jua vipaji na uwezo mkubwa uliopo ndani yako kisha chagua kazi au biashara inayoendana na vitu hivyo. Hii ndiyo itakayokuletea utajiri mkubwa.

SURA YA 14; MWONEKANO WA UKUAJI.

Kwa kazi au biashara unayoifanya, usifanye kwa mazoea au kufanya vile vile kila wakati. Badala yake fanya kwa ukuaji kila siku. Kila siku kazana kupiga hatua kubwa zaidi ya ulizopiga siku zilizopita.

Ni mwonekano huu wa ukuaji ndiyo unaowavutia watu kwako. Watu wanapenda kujihusisha na wale ambao wanakua zaidi, wanatoa thamani kubwa zaidi kila siku.

Mazoea yanaharibu na kuua kabisa kile ambacho kipo ndani ya mtu. Lakini ukuaji unakuza zaidi kile ambacho kipo ndani ya mtu.

SURA YA 15; UKUAJI BINAFSI.

Ili kuvutia utajiri kupitia kile unachofanya na ili kuziona fursa mpya kila mara, lazima wewe binafsi uwe unakua. Kwa chochote unachofanya sasa, hata kama ni kidogo kiasi gani, unapaswa kukua zaidi ya kitu hicho.

Hata kama upo kwenye kazi au biashara ambayo ni ndogo, ifanye kama kubwa na tekeleza majukumu yako kwa ukubwa. Tekeleza majukumu yako kwa ufanisi wa hali ya juu na wahudumie watu kwa namna ambayo inaongeza thamani kubwa kwao.

Kadiri unavyokua wewe, ndivyo kile unachofanya kinavyokua na ndivyo utajiri unavyokuja kwako kwa wingi na kwa haraka.

SURA YA 16; TAHADHARI NA HITIMISHO.

Watu wengi watakataa kwamba hakuna sayansi ya kupata utajiri kwa kufikiri na kutenda kwa namna fulani. Wataendelea kuamini kwamba kuna uhaba wa utajiri na kwamba ili watajirike lazima serikali na taasisi mbalimbali zibadilishwe kwanza.

Lakini huu siyo ukweli hata kidogo. Ni kweli serikali na taasisi mbalimbali zinaweza kuwa zinawafanya watu wawe kwenye umasikini, lakini ni watu hao wanakuwa wamechagua wenyewe kukaa kwenye umasikini. Kama watu hawa watainuka kwa pamoja, na kuanza kufikiri na kutenda kwa namna fulani, hakuna serikali wala nguvu yoyote inayoweza kuwazuia wasiwe matajiri.

Nguvu ya kutengeneza utajiri mkubwa ipo ndani yako, na hata kama nje ni pagumu kiasi gani, unayo nguvu ya kuvuka ugumu wowote. Unachohitaji ni kuishi misingi uliyojifunza kwenye kitabu hiki, kufikiri kwa namna ya kuvutia utajiri, kutenda kwa njia ambayo italeta utajiri, kukua binafsi, kuwa na shukrani na kutoa thamani zaidi kwa wengine.

SURA YA 17; MUHTASARI WA SAYANSI YA KUPATA UTAJIRI.

  1. Kuna mfumo wa kufikiri ambao kutoka ndani yake vitu vyote vinatengenezwa na ambao kwa uhalisia wake unaruhusu, kupenyeza na kuujaza ulimwengu wote.
  2. Fikra kwenye mfumo huu inazalisha ile taswira inayotengenezwa na fikra.
  3. Mtu anaweza kutengeneza vitu kwenye fikra zake na kwa kuziweka kwenye mfumo huu wa kufikiri kile anachofikiri kinaumbwa.
  4. Ili kufanya hivi, mtu anapaswa kuondoka kwenye fikra za ushindani na kwenda kwenye fikra za ubunifu. Vinginevyo hataweza kuendana na mfumo wa fikra ambao mara zote upo kwenye hali ya ubunifu na siyo ushindani.
  5. Mtu yeyote anaweza kuendana na mfumo huu wa fikra kwa kuwa mtu wa shukrani kwa baraka ambazo amezipata. Shukrani inaunganisha fikra za mtu na mfumo wa fikra unaoendesha ulimwengu.
  6. Mtu lazima atengeneze picha ya kifikra ya vitu anataka kuwa navyo na kuifikiria picha hii mara zote huku akiwa na imani kwamba ataipata na kushukuru kwamba mfumo wa fikra unamwandalia mazingira ya kupata kile anachotaka. Tumia muda wako wa mapumziko kufikiria picha ya utajiri unaotaka kuwa nao na mfumo wa fikra utaipanga dunia kwa namna ambayo itakuletea kile unachotaka.
  7. Mfumo wa kufikiri unafanya kazi kupitia njia za asili za ukuaji na za kijamii. Kila ambacho kinafikiriwa kwa muda mrefu kwa imani na bila ya shaka, ndiyo kinacholetwa kwenye uhalisia.
  8. Ili kupokea kile ambacho mtu anataka, lazima mtu achukue hatua kwa namna fulani ambayo inamwezesha kujaza pale alipo sasa. Lazima afanye zaidi, lazima atoe thamani kubwa kwa wengine kuliko thamani anayopokea na lazima akue zaidi na akuze zaidi kile anachofanya.
  9. Mtu yeyote atakayefuata maelekezo haya, kwa imani na bila ya mashaka, kwa hakika atapata utajiri. Na utajiri atakaopata utakuwa sawa na ukubwa wa fikra na maono yake na uimara wa imani yake pamoja na wingi wa shukrani zake.

Rafiki, hiyo ndiyo sayansi ya kutengeneza utajiri mkubwa kwenye maisha yako, ambayo inahusisha vitu vikuu viwili, FIKRA na KUCHUKUA HATUA. Mwaka huu 2019 tengenea utajiri mkubwa kwenye maisha yako kwa kutumia sayansi hii. Jifunze misingi hii na iishi kwenye kila siku ya maisha yako na hakuna kitakachoweza kukuzuia usipate utajiri mkubwa unaotaka.

#2 MAKALA YA JUMA; MAMBO 19 YA KUFANIKIWA 2019.

Rafiki, kwenye juma hili la kwanza la mwaka 2019, tumekuwa na makala ya mambo 19 ambayo unapaswa kuyafanya kila siku ya mwaka huu 2019 ili uwe mwaka wa mafanikio makubwa sana kwako.

Kama hukupata nafasi ya kusoma makala hiyo, na kuyajua mambo hayo 19 hakikisha unasoma sasa na kuyajua, kwa sababu ni mambo muhimu mno.

Soma makala hiyo hapa; Fanya Mambo Haya 19 Pekee Kila Siku Na Mwaka 2019 Utakuwa Wa Mafanikio Makubwa Sana Kwako.

Pia mwaka huu 2019, kila siku anza siku yako kwa kuingia www.amkamtanzania.com na utapata makala nzuri sana za kukuwezesha kuianza siku yako ukiwa na maarifa na hamasa ya kufanya makubwa zaidi.

#3 TUONGEE PESA; MBINU YA KUONGEZA KIPATO 2019.

Rafiki, kama mwaka 2018 haukuwa vizuri kwako kwa upande wa kipato, ninayo mbinu nzuri kwako ya kuongeza kipato chako kwa mwaka huu 2019.

Mbinu hiyo muhimu ni kuanza kujiongeza wewe kwanza. Kabla kipato chako hakijakua, anza kukua wewe.

Ukweli ni kwamba, kipato chako hakiwezi kukua kukuzidi wewe, hivyo lazima ukue kwanza kama unataka kipato chako kikue.

Na unakua kwa kuongeza maarifa kuhusiana na kile unachofanya na hata kwenye fedha kwa ujumla.

Eneo muhimu kwako kufanyia kazi na kukua kwa mwaka huu 2019 ni UWEZO WAKO WA KUTENGENEZA KIPATO. Hakikisha unakuza zaidi uwezo huu.

Kwenye kazi au biashara unayofanya, hakikisha unatoa huduma bora sana mwaka huu 2019 kuliko ulivyokuwa unatoa mwaka 2018. Hakikisha unatoa thamani kubwa zaidi ya matumizi kuliko ile unayochukua kwenye fedha.

Kama wewe utakua, kipato chako kitakua pia. Lakini kama utabaki vile ulivyo, ukifanya kwa mazoea, kipato chako kitaendelea kubaki kilivyo na kwa kuwa maisha yanaenda kwa kasi, basi kipato kitazidi kuwa shida kwako.

Jawabu unalo, kukuza kipato chako, anza kukua wewe binafsi.

#4 HUDUMA NINAZOTOA; ZAWADI BORA ZAIDI KWAKO KWA MWAKA HUU 2019.

Rafiki, na hapa naongea na wale marafiki ambao kila mwaka wamekuwa wanasema watajiunga na KISIMA CHA MAARIFA lakini mwaka unaisha na hawafanyi hivyo. Nawajua wengi ambao wamekuwa wananiahidi hili, kwamba mwaka ukianza najiunga, na mwaka unaanza na kuisha hawajiungi.

Rafiki, nataka leo ujipe zawadi bora sana kwa mwaka huu 2019 na zawadi hiyo ni kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA leo hii. Usiendelee kusubiri tena, chukua fedha uliyonayo, hata kama ilikuwa akiba muhimu kiasi gani na jiunge.

Kama huna fedha kabisa omba na hata kusanya michango kwa watu wako wa karibu na jiunge. Fanya chochote utakachohitaji kufanya ili upate ada ya kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA ili mwaka huu 2019 ukawe mwaka wa tofauti kabisa kwako.

Ada ya kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA ni tsh 100,000/= (laki moja). Namba za kulipia ili kujiunga ni MPESA; 0755 953 887 au TIGO PESA 0717 396 253, kama unatumia AIRTEL MONEY au mitandao mingine, tuma moja kwa moja kwenda TIGO PESA namba 0717396253.

Karibu sana kwenye KISIMA CHA MAARIFA rafiki, na ninakuhakikishia mwaka 2019 utakapokuwa unaisha, utajishukuru sana kwa hatua hii uliyochukua.

Na nimeshauhakikishia hili, kama mpaka mwaka 2019 unapoisha utakua hujaona matokeo ya tofauti kwenye maisha yako, basi nijulishe na nitakurejeshea ada uliyolipa. Hili nakuambia kwa uhakika na wala usiwe na shaka yoyote.

#5 TAFAKARI YA KUFIKIRISHA; KAULI YA KUANZA 2019 KAMA 2018 HUKUFIKIA MALENGO ULIYOJIWEKEA.

“Failure is simply the opportunity to begin again, this time more intelligently.” – Henry Ford

Rafiki, huenda kuna malengo ambayo ulijiwekea mwaka 2018 lakini ukashindwa kuyafikia. Huenda jambo hilo limekuumiza na hata kufika hatua ya kuona huna haja ya kuweka malengo makubwa 2019.

Napenda kukupa kauli hii nzuri kutoka kwa Hendry Ford, anza mwaka na kauli hii na nenda nayo mwaka mzima; kushindwa ni fursa ya kuanza tena, ukiwa na akili zaidi kuliko mwanzo.

Anachotuambia Ford ni kwamba unaposhindwa, jifunze nini kimepelekea ukashindwa, ili unapoanza tena usirudie yale yaliyopelekea ukashindwa kwa mara ya kwanza.

Hivyo mwaka 2019 usiwe mwaka wa kushindwa kwako, bali uwe mwaka wa kujifunza na kuanza upya ukiwa na akili na uelewa zaidi.

Ishi kwa kauli hii kila siku na mwaka huu 2019 utakuwa wa mafanikio makubwa sana kwako.

Rafiki, pokea tano hizi za juma la kwanza la mwaka 2019 na ambazo ni tano utakazotumia kwa mwaka mzima wa 2019. Endelea kuzitumia kama rejea ya kwenda kwa mwaka wako huu 2019. Jiunge na KISIMA CHA MAARIFA kama bado, ishi misingi ya SAYANSI YA UTAJIRI, kua wewe ili kipato chako kikue na kila unaposhindwa, jifunze na uwe mjanja zaidi.

Mwaka huu ukawe bora sana kwako kwa sababu najua huu ni mwaka wa vitendo kwako.

Makala hii imeandikwa na Kocha Dr Makirita Amani.

Dr. Makirita ni Daktari wa binadamu, Kocha wa mafanikio, Mwandishi na Mjasiriamali.

Dr. Makirita anaendesha mafunzo ya mafanikio kwa wale waliojitoa hasa kufanikiwa kupitia program ya KISIMA CHA MAARIFA.

Kama bado hujajiunga na KISIMA CHA MAARIFA, tuma sasa ujumbe wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA kwa njia ya wasap namba 0717 396 253 (tumia wasap tu)

Kupata huduma nyingine za ukocha tembelea www.amkamtanzania.com/kocha

Kupata vitabu vizuri vya kusoma tembelea www.amkamtanzania.com/vitabu