The Plague ni riwaya iliyoandikwa na Albert Camus ambaye alikuwa ni mwandishi na mwanafalsafa wa Ufaransa. Katika maisha yake Camus aliandika vitabu vingi vya riwaya na falsafa ambavyo vilikuwa na mafunzo ya kumwezesha mtu kuishi kwa misingi sahihi.

Kwenye riwaya ya The Plague, Camus ametumia mlipuko wa ugonjwa wa tauni kuonesha jinsi ambavyo jamii inaathirika kwa kupitia mateso makali na vifo na namna ambavyo kila mmoja anaweza kusaidia mapambano dhidi ya mlipuko kama huo.

Japokuwa kisa kilichotumika kwenye riwaya hii ni ugonjwa wa tauni, lakini ujumbe unalenga magumu yoyote ambayo kila jamii huwa inapitia ikiwepo ukandamizaji, hali ngumu ya maisha na hata changamoto binafsi ambazo mtu anaweza kupitia.

Camus anatuonesha kwamba hata kama unachokabiliana nacho ni kikubwa na kimekuzidi nguvu, bado kuna hatua unaweza kuchukua na zikasaidia. Tutajifunza hayo kwenye riwaya hii ambayo ina mafunzo mengi ya kijamii, kifalsafa, kidigi, kimaadili, ushirikiano na kujituma. Kwa kifupi tunajifunza jinsi ya kukabiliana na nyakati ngumu kwenye maisha bila ya kukata tamaa.

RIWAYA KWA UFUPI.

Riwaya inaelezea maisha ya mji wa Oran ulioko nchini Algeria wakati nchi hiyo ikiwa koloni la Ufaransa. Maisha ya mji huo siyo mazuri sana, kwani msongamano ni mkubwa, mazingira ni ya joto na uchafu upo kila kona. Watu wa mji huo wanaishi katika hali ya msongo, lakini hawajali sana, maana ni maisha ambayo wameshayazoea.

Inatokea hali ya kushangaza kwenye mji wa Oran, panya wengi wanaonekana kufa kwa kipindi kifupi. Panya ni wengi kiasi cha kuleta taharuki kwa watu na serikali kuweka timu ya watu wa kuokota panya wote waliokufa. Mji mzima umetapakaa panya.

Vifo vya panya vinaisha na watu wanapata ahueni, lakini kabla ya muda kupita, ugonjwa wa ajabu unaibuka na watu kuanza kufa. Dr. Rieux anafuatilia vifo hivyo na kushawishika kwamba ni mlipuko wa tauni. Serikali inasita kukubali kweli ni tauni, vifo vinaendelea kuongezeka, hospitali zinajaa wagonjwa.

Kutokana na hali hiyo, serikali inashindwa kuficha na kutangaza ni mlipuko wa tauni. Na ili kuzuia maambukizi yasifike kwenye miji mingine, inatangazwa karantini, hakuna mtu kuingia wala kutoka kwenye mji wa Oran. Watu kusikia karantini wanataharuki zaidi, wapo wanaojaribu kutoroka lakini wanashindwa, wengine wanajiua.

Katika kipindi hicho cha karantini na vifo kuwa vingi ndipo tunapojifunza kwa kina tabia za watu na hatua wanazochukua katika hali hizo. Wezi wananufaika zaidi kwa kutumia magendo, watu wa dini wanahubiri tauni ni pigo la Mungu kwa makosa ya wanadamu, huku wengine wakifanya kazi usiku na mchana kusaidia wale waliopatwa na ugonjwa huo.

Vifo vinazidi kuwa vingi, utaratibu wa kuzika maiti unakuwa mgumu kuendelea kama ulivyokuwa hivyo watu wanazikwa kwa pamoja na bila ya taratibu zilizozoeleka. Katika hatua hii watu wanakata tamaa na kuona hakuna namna wanaweza kupona.

Kikundi cha watu wachache wanaendelea kuweka juhudi kusaidia hali hiyo inayoendelea, wanafanya hivyo kama njia ya kutoa mchango wao, licha ya kwamba mlipuko wa tauni unaonekana kuwa na nguvu kubwa kuliko uwezo wao. Watu wengi wanaendelea kufa, hata kiongozi mashuhuri wa dini aliyehubiri tauni hiyo ni pigo la mungu naye anakufa.

Baada ya miezi mingi ya kuwepo kwa mlipuko huo, vifo vinaanza kupungua na watu kupata matumaini kwamba mlipuko unaisha. Maisha yanarudi kama kawaida, karantini inaondolewa. Wengi, ikiwepo waliokuwa wanapambana na tauni wamekufa kwa tauni, waliokuwa wananufaika nayo kwa kufanya magendo wanaishia kwenye mikono ya sheria.

Msimuliaji wa kisa hiki, ambayo hatumjui mpaka mwishoni anahitimisha kwa kusema kwamba tauni inaweza kuibuka eneo lolote, kwa sababu kila jamii ina tauni yake. Lakini wakati wa tauni, tunajifunza kwamba kuna mengi mazuri ya kupongeza kwa watu kuliko yale mabaya ya kushutumu. Kwamba hali ngumu zinatufanya kuja pamoja na kushirikiana kuliko kututenganisha.

Karibu kwenye uchambuzi wa riwaya hii, tujifunze mengi ili tuweze kukabiliana na magumu mbalimbali tunayokutana nayo kwenye maisha.

WAHUSIKA WAKUU.

Wafuatao ni wahusika wakuu kwenye riwaya ya The Plague.

Dr. Bernard Rieux, Huyu ni daktari wa upasuaji kwenye hospitali ya mji wa Oran, ambaye kwa kipindi chote cha tauni amekuwa mstari wa mbele kupambana nayo. Mke wake anafariki kwa ugonjwa ambao hauelezwi, ila rafiki yake aliyekuwa anapambana naye anafariki kwa tauni wakati imefika mwisho kabisa. Rieux anatufundisha kufanya majukumu yetu katika kuwasaidia watu bila ya kujali tunapitia hali gani.

Jean Tarrou, huyu alikuwa kwenye mji wa Oran wakati mlipuko wa tauni unaanza na hivyo kushindwa kuondoka. Anakuwa rafiki wa karibu wa Rieux na anakusanya timu ya watu watakaosaidia kupambana na mlipuko huo, kwa kuhakikisha mitaa iko safi. Tarrou anafariki kwa tauni wakati imefika mwisho kabisa, baada ya kuwa amepambana nayo kwa kipindi chote, akiweza kuwashawishi watu mbalimbali kuungana naye. Tarrou anatufundisha kutumia kile tulichonacho na kufanya chochote tunachoweza ili kukabiliana na hali ngumu inayokuwa inaendelea.

Father Paneloux, huyu alikuwa padri wa mji wa Oran, alikuwa maarufu kwa mahubiri yale yaliyogusa watu. Tauni ilipoanza alihubiri akisema ni pigo kutoka kwa Mungu kwa sababu ya dhambi za watu, hivyo watu wanapaswa kutibu. Baadaye anashawishiwa kujiunga na timu ya Tarrou ya kusaidia kupambana na tauni na anashuhudia kijana mdogo na asiye na hatia akifariki kwa mateso kwa tauni. Hapo anabadili mtazamo wake na kutoa mahubiri akisema tauni ni kitu ambacho kimekuja kuwaleta binadamu pamoja, kushirikiana kupambana nacho. Na yeye anafariki dunia kwa ugonjwa ambao hauwezi kuelezeka kama ni tauni au la. Paneloux anatufundisha kuepuka kutafuta majibu rahisi kwenye mambo magumu, lakini pia kuwa tayari kubadili msimamo pale tunapoujua ukweli.

Raymond Rambert, huyu alikuwa mwandishi wa Paris aliyekuwa ametembelea Oran kwa shughuli zake za uandishi. Kwa bahati mbaya, tauni inatokea akiwa mjini hapo na karantini inawekwa hivyo hawezi kuondoka. Anatumia kila njia kutaka kuondoka kwa sababu ana mchumba wake anayemsubiri sana lakini zote zinashindwa. Mwisho anatumia njia za magendo, anafanikiwa kupata nafasi ya kutoroka, lakini kabla hajakamilisha hilo, anakutana na Tarrou ambaye anamwambia sababu yake ya kutaka kuondoka haina mashiko, kwa sababu hata Dr Rieux mke wake ni mgonjwa na yuko nje ya mji huo, lakini kila siku anapambana kukabiliana na tauni. Rambert anaahirisha mpango wake wa kutoroka na kujiunga na timu ya Tarrou katika kupambana na tauni. Rambert anatufundisha kuacha kuwa wabinafsi, kuacha kujali mambo yetu wakati jamii inapitia wakati mgumu na kuna namna tunaweza kusaidia.

Joseph Grand, huyu alikuwa mfanyakazi wa serikali, lakini wa ngazi ya chini na ambaye kwa miaka mingi hajawahi kupanda cheo. Ameachwa na mke wake aliyempenda sana na pia amekuwa na wazo la kuandika kitabu, lakini kwa miaka mingi ameishia kuandika sentensi ya kwanza tu, ambayo huwa anaihariri kila mara. Anaungana na timu ya Tarrou pamoja na Dr. Rieux katika kupambana na tauni. Mwishoni anapata tauni, lakini anapona na hapo anaamua kuanza upya kuandika kitabu chake na kukikamilisha na pia kumtafuta mke wake. Grand anatufundisha jinsi ambavyo mtu wa kawaida anaweza kupambana na changamoto kubwa kwa kufanya kile anachoweza. Lakini pia anatuonesha jinsi ilivyo rahisi kuahirisha unachopanga katika nyakati za kawaida, lakini pale kifo kinapobisha hodi ndiyo unajua huwezi kuendelea kuahirisha na hivyo kufanya ulichopanga.

Cottard, huyu alikuwa jirani wa Grand lakini pia alikuwa mhalifu ambaye maisha yake yalikuwa ya kujificha wakati wa kawaida. Mlipuko wa tauni ulipoanza, kwake ilikuwa furaha, kwa sababu polisi hawakuwa wanamtafuta tena, hivyo alitumia nafasi hiyo kuendeleza uhalifu na alinufaika sana wakati huo wa mlipuko. Mlipuko unapoisha anaona hana namna ya kuendelea kujificha tena, anazua taharuki kwa kulipua risasi nyingi na mwisho kuishia kukamatwa na polisi. Cottard anatufundisha jinsi wahalifu wanavyonufaika nyakati za majanga, lakini pia tunaona jinsi manufaa hayo yasivyodumu.

M. Michel, huyu alikuwa mwangalizi wa jengo ambalo Rieux alikuwa akiishi. Mwanzo alipinga uwepo wa panya ili kulinda kazi yake, akiamini kuna mtu analeta panya na kuwaweka kwenye jengo hilo. Anakuwa mtu wa kwanza kufariki kwa ugonjwa wa tauni.

Madame Rieux, huyu ni mama yake Rieux amabye amekuja kuishi naye baada ya mke wake kuondoka kwenda kwenye matibabu. Mke wa Dr Rieux alikuwa mgonjwa wa muda mrefu na hivyo alipelekwa kwenye kituo cha matibabu nje ya mji wa Oran. Anafariki akiwa kwenye kituo hicho.

Mgonjwa wa pumu, huyu alikuwa ni mgonjwa wa Dr Rieux ambaye kila siku alimtembelea kuangalia maendeleo yake na kumpatia dawa. Mgonjwa huyu alikuwa akitabiri mambo mbalimbali kuhusu yanayoendelea kwenye mji wa Oran. Wakati panya wanaanza kuonekana alieleza siyo dalili nzuri, wakati vifo vinaongezeka kwa kasi anaeleza kwa nini watu wanakufa na kwa nini yeye ataendelea kuishi. Na hata pale tauni inapoisha na watu kushangilia anaeleza kwamba watu hawajifunzi chochote, watarudi kwenye maisha yale yale na kufanya mlipuko mwingine uwe rahisi. Mgonjwa huyu ambaye pia alikuwa mzee wa miaka 75 anatufundisha mengi kuhusu asili ya binadamu na yale yanayoendelea.

KARIBU KWENYE UCHAMBUZI.

Karibu kwenye uchambuzi kamili wa kitabu hiki cha The Plague, tukaangalie kwa ufupi visa vilivyoendelea ambavyo kuna mambo tunayoweza kujifunza na kuyatumia kwenye maisha yetu binafsi na hata maisha ya kijamii.

Kupata uchambuzi kamili wa kitabu hiki pamoja na vitabu vingine jiunge na channel ya SOMA VITABU TANZANIA kwa kufungua kiungo hiki; www.t.me/somavitabutanzania

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali.