“Self-reverence, self-knowledge, self-control,
These three alone lead life to sovereign power.”
— Alfred Tennyson

Kuna nguvu tatu ukiwa nazo, utakuwa na uhuru wa uhakika kwenye maisha yako.
Nguvu hizo ni;
KUJITAMBUA; Lazima kwanza ujijue wewe mwenyewe kama unataka mafanikio na uhuru. Huwezi kufanikiwa kwa kujaribu kuwa kama wengine. Upekee wako ndiyo utakaokutofautisha na wengine na kukupa mafanikio makubwa. Jitambue, kuwa wewe.
Kujaribu kuiga maisha ya wengine ni dalili ya kutokujitambua, acha mara moja.

KUJIHESHIMU; Ni lazima ujiheshimu, baada ya kujitambua, jiheshimu kama unavyowaheshimu wale unaowakubali sana. Lazima ujikubali sana wewe mwenyewe, uwe shabiki wa kwanza kwako. Hata kama watu hawana imani na wewe, anza wewe kuwa na imani na wewe. Baadaye watu hawatakuwa na namna bali kukuheshimu kama unavyojiheshimu. Usipojiheshimu mwenyewe, hakuna atakayekuheshimu.
Kupanga kitu na usitekeleze, hata kama ni kwako mwenyewe ni dalili ya kutokujiheshimu. Usiendelee kufanya hivyo.

KUJIDHIBITI; Uhuru haumaanishi kupata kila unachotaka kwa namna unavyotaka na wakati unaotaka. Uhuru haumaanishi kusikiliza kila ambacho mwili wako na akili yako vinakuambia. Vingi unasukumwa na hisia na hivyo siyo sahihi kwako.
Unahitaji kujidhibiti kama unataka kuwa huru. Uhuru wako utakuwa kwa kiwango unachojidhibiti wewe mwenyewe, jinsi unavyojizuia kufanya mengi unayosukumwa kwa mihemko.
Kutaka kupata raha ya muda mfupi bila kujali matokeo ya muda mrefu ni dalili ya kutokujidhibiti, ondoka kwenye hilo.

#JitambueJiheshimuJidhibiti
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
Ukurasa wa kusoma leo ni kuhusu majibu ya haraka, soma hapa; http://www.kisimachamaarifa.co.tz/2020/07/23/2031

Wako rafiki katika safari ya kuelekea kwenye mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,