Akiba ni kitu unachoweka wakati mambo yako yanakwenda vizuri, ili kikusaidie pale mambo yatakavyokwenda vibaya. Unapozingatia hilo, unaepuka usumbufu na gharama zisizo na ulazima. Mfano unapojikuta kwenye changamoto za kifedha, ukiwa na akiba unazitatua, ukiwa huna, unaingia kwenye mkopo ambao utakuumiza zaidi.

Unanunua mwavuli wakati wa kiangazi, ili wakati wa masika mvua isikuzuie kufanya shughuli zako. Kipindi ambacho hakuna mvua miavuli hupatikana kwa bei rahisi, lakini ukisubiri mpaka siku mvua ni kubwa na una haraka, hapo ndipo utakapouziwa mwavuli kwa bei kubwa, na hutakuwa na namna, itabidi ukubali bei hiyo.

Watu wengi wanaishi maisha yao kwa tabia ya kuzima moto, badala ya kuzuia moto usitokee, wanasubiri utokee na kukazana kuuzima, halafu wanajisifia kwa zoezi hilo la kuzima moto.

Labda nikuulize swali, kipi kizuri kwenye nyumba yako ambayo umeijenga kwa muda mrefu na gharama kubwa? Kuizuia isishike moto, au kuwa mzembe na nyumba kuwaka moto kisha ukafanya tukio la kishujaa la kuzima moto huo?

Hata kama utafanikiwa kuumiza moto, nyumba ambayo imeshashika moto siyo sawa na ambayo haijashika moto kabisa. Lazima utaingia gharama kuirudisha kwenye hali ya kawaida.

Nikuulize swali jingine rahisi, kipi kizuri kwa afya yako, kudhibiti afya yako ili usiwe na uzito wa kupitiliza, au uishi kizembe, uwe na kilo 30 zaidi ya unazopaswa kuwa nazo, kisha uje ufanye dayati ya mwezi mmoja na kuondoa kilo hizo za ziada na kujisifia kwa tukio hilo?

Utaona wazi kwamba mwili ambao umeshabeba kilo 30 za ziada siyo sawa na ule ambao haujawa na uzito huo unaopitilia. Lakini ukienda mbali zaidi, zoezi hilo la kupunguza uzito kwa haraka huwa linazaa madhara yake pia.

Mfano mwingine utasaidia tuelewane vizuri hapa, kwenye kazi yako una ripoti ya kurasa 30 za kuandika na una mwezi mzima mbele yako. Kipi bora kwako, kutenga saa moja kila siku kufanyia kazi ripoti hiyo kwa siku hizo 30 au kusubiri mpaka siku ya mwisho ukeshe ukiandaa ripoti hiyo? Unafikiri ni ripoti ipi itakuwa nzuri, iliyoandaliwa kidogo kidogo mwezi mzima au iliyoandaliwa siku moja, tena kwa mtu kukesha?

Mbadala wa maisha ya zima moto ni kujenga tabia zenye manufaa kwenye maisha yako. Badala ya kusubiri mambo yahangaike ndiyo uanze kuyabadili, unazuia mambo yasifike kwenye uharibifu.

Hapa ndipo tabia inapokuwa kama akiba, inakufanya uchukue hatua kabla hujawa na uhitaji wa kitu na hatua hizo zinakufanya usiwe na uhitaji huo.

Huo ndiyo uzuri wa akiba, ukishakuwa nayo, unajikuta huna uhitaji, lakini ukiwa huna, uhitaji unakuwa mkubwa. Mfano ukiwa na tabia ya ulaji wa afya na kufanya mazoezi, hutapata uzito uliopitiliza na hivyo hutahitaji kufanya dayati ya kupunguza uzito wa haraka. Ukianza kufanya kazi yako mapema kabla muda haujaisha, utaimaliza kazi hiyo vizuri na hutahitaji kukesha siku moja ili kuimaliza.

Kwenye maisha yako, kazana kujijengea tabia kwenye kila eneo, ili uweze kuchukua hatua sahihi kabla uhitaji haujakuwepo. Hivyo ndivyo maisha bora na yenye mafanikio yanavyotengenezwa, kwa kujenga tabia zinazokuwa na manufaa kwako kuliko kusubiri moto uwake ndiyo uuzime.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha