Dunia imekuwa inapitia katika nyakati za mabadiliko mengi kutokana na historia inavyoeleza. Historia inaturudisha nyuma kuona namna baadhi ya wanyama walivyotoweka na jinsi hata pia matukio ya kijiografia yalivyoathiri sana viumbe kwa wakati huo. Ni mabadiliko makubwa sana mpaka sasa ambayo yapo wazi kabisa yakionekana na yaliyosalia.Lakini pia maendeleo ya mawasiliano na teknolojia yamefanya kwa kipindi cha muda mfupi sana cha dunia ikue kwa kasi na kufanya baadhi ya mambo yapishwe nyuma na kasi kubwa ya maendeleo ya sayansi na teknolojia. Na mabadiliko haya moja kwa moja yanagusa watu na watu wanaoguswa sana hapa ni wale wajasiriamali kwa upana wake namna gani wanaweza kufaidika na kasi kubwa hii ya mabadiliko ya teknolojia inayojizidisha (exponential technology).

Waandishi wawili wa kitabu hiki “Dkt. Peter Diamandis na Steven Kotler” wanaeleza namna vile teknolojia ambavyo imefanya mambo kuwa rahisi na kasi kubwa zaidi tafauti na hapo siku za kale, ni wazi namna ya kutengenezwa kwa simu janja (smart phones) kumeleta mapinduzi makubwa sana katika dunia tuishi leo na huenda ijayo, sasa hivi watu wamekuwa na nafasi ya kuweza kumiliki simu na kuzitumia kwa namna ya ushawishi mkubwa sana tofauti na wakati wa nyuma. Leo kwa mfano mdogo tu, tunaona namna habari zinavyoweza kusambaa kwa haraka sana sababu ya uwepo wa interneti ambao ni matokeo ya maendeleo ya teknolojia ya mawasiliano. Hivi ndivyo nguvu ya teknolojia inayojizidisha ifanyavyo kazi kwa kasi kubwa na kwa haraka kuathiri dunia na jamii za watu ndani yake.

Ndani ya kitabu hiki Dkt. Peter Diamandis na Steven Kotler wanasema kuna maeneo 6 mpaka 7 ambayo kasi ya ukuaji wake ni mkubwa sana na kuonyesha ndani ya kipindi cha miaka mingine ijayo kutoka sasa, basi maeneo haya yatabadili sana mambo katika Uso wa Dunia. Maeneo kama ya mitandao yatazidi kupanuka na kuenea zaidi, vitambuzi (sensors), teknolojia ya maroboti, werevu wa kisasa “artificial intellegience”, biolojia, utabibu wa kijidijitali ( digital medicine and nanotechnology ). Hivi ndivyo ambavyo haya maeneo yatazidi kutanuka mbali na tuonavyo sasa.

Hivyo kama mjasiriamali na mfanyabiashara ni muhimu sana kufuata namna teknolojia inakoenda katika kuhakikisha bidhaa, huduma, viwanda vyote vinakuwa katika nafasi ya uelekeo wa teknolojia inavyojizidisha siku hadi siku. Kama namna vile baadhi wanyama kwa kipindi cha historia walitoweka sababu ya mabadiliko, basi hata sasa ni rahisi sana kuachwa kwa wafanyabishara au wajasiriamali kwa maeneo yao tofauti kupitwa sababu ya kushindwa kwenda na kule Dunia inakoelekea katika teknolojia. Mfano unaopendwa kuchukuliwa kuhusu athari ya mabadiliko ni ule wa Kampuni ya kwanza ya uchapishaji picha “Kodak” umekuwa ukitumika sana namna ambavyo ilijikuta ikipoteza ushindani kwa kutokwenda na wapi uelekeo wa teknolojia ya kasi kuwepo.

Karibu tujifunze mambo 25 ambayo waandishi wameandika namna gani tunaweza kukua na kutengeneza utajiri na kisha matokeo chanya kwa Dunia yakatokea.

Hichi ni kitabu muhimu sana kufanyia kazi yale ambayo waandishi wameandika ili kutanua safari nzima ya ujasiriamali wa kuangalia miaka ijayo itakuaje katika sura ya teknolojia ya kujizidisha (Exponential Technology)

1. Katika miaka ya zamani katika historia ni makundi makubwa kama wafalme, watawala na hata mafarao walokuwa na nafasi ya utatuzi wa matatizo makubwa ya kidunia na hivyo kufanikiwa sana. Maana kadri unapotatua matatizo makubwa duniani ndivyo unapopata nafasi kubwa sana ya kufanikiwa na kuathiri kwa ukubwa zaidi maana wanaohitaji majibu ya matatizo au mahitaji ni wengi na wanazaliwa kila siku watu wapya. Lakini nafasi hii ya kufanya hivi bado ipo hata sasa kwa kupata nafasi ya kuwa na teknolojia, akili komavu za watu, vitabu na hata mashine ambavyo ni vifaa katika utatuzi wa matatizo makubwa ya kidunia

2. Njia pekee kubwa ya mtu kutengeneza kiasi cha fedha bilioni ni kutatua tatizo la mtu aliye na bilioni. Na hapo ndipo ndoto za watu na wafanyabiashara na wajasiriamali wanaweza kutumia nafasi hii kutengeneza njia na kufanya makubwa kupitia fursa ya teknolojia. Mifano ya watu wakubwa ambao wamewekeza sana katika teknolojia kama Lary Page wa Google [ Jukwaa kubwa maarufu duniani la kuruhusu utafutaji wa chochote kihusicho taarifa, picha, picha mjongeo na kadhalika], Elon Musk wa Space X na Tesla Motors [ haya ni magari yaendeshwayo kwa umeme], Richard Branson wa Virgin Group of Companies , na Jeff Bezos wa Amazon.com [ Kampuni kubwa ya uuzaji bidhaa mtandaoni] wamepiga hatua kubwa sana ya mabilioni ambayo ni nafasi kubwa pia kwa watu wengine kufikiri kwa ukubwa huo na kuathiri dunia katika uchanya.

3. Usipokuwa tayari katika Dunia ya teknolojia na maendeleo makubwa yanayotokea kila siku. Jua kuwa huna muda mrefu wa kuendelea kudumu katika biashara na mwisho ni kuanguka au kufa kibiashara. Mfano wa Kodak ndio unaonyesha namna kutokubadilika kwake kulifanya ife kibiashara kutokana na mabadiliko ya picha za kidijitali kuwepo na utokeaji wa magunduzi ya simu zilizokuwa na kamera.

4. Kama vile namna ya mlipuko wa bomu kitendo chake kikemikali kinapofanyika kwa kujizidisha ndivyo ilivyo katika ukuaji wa teknolojia unavyokwenda kasi siku hadi siku. Na njia ya kwanza kabisa ya kufanya bidhaa au huduma ianze kukua kwa kasi ni kubadilishwa na kuwa katika mfumo wa kidijitali, mfano picha kuwekwa katika “App kama Instagram” kumefanya ipate umaarufu sana duniani na athari yake ni kubwa sana na imetokea kuwa jukwaa linalotumiwa na watu kujitangazia bidhaa au biashara.

5. Mwandishi anagusia maeneo 6 ya Ukuaji wa kujizidisha katika teknolojia unavyoanza na namna mambo yanavyokua kwa ukubwa na kuathiri dunia, anaziita kwa D 6 (The 6 D’s of Exponentials)

“Digitalization” [ Ujidijitalishaji ]

Kipindi cha kale watu walikuwa wakibadilishana mawazo kwa njia ya usimuliaji hadithi kabla ya magunduzi ya karatasi na kiwanda cha kuchapa. Kadri muda ulivyosogea ndivyo mambo hubadilika na kufika mabadiliko ya kuhama picha za mkanda “nega” hadi kufika katika mfumo wa digitali, kuhamia mfumo huu kumefanya soko lake kushuka la KODAK, na huku upande mwingine ukikua sana. Kila kitu kinapowekwa katika mfumo huu kinakuwa na nafasi kubwa sana ya kujizidisha kwa kutumia uwepo wa interneti pia.

Deception (Udanganyifu)

Mfano mzuri ni ule ule wa Kodak, ni hatua ambayo mabadiliko ya kuingia kwa mfumo digitali unakuwa unaenda pasipo kuwa na athari za wazi zinazoonekana na hivyo si rahisi kuona kwa hatua hii inaharibu kitu.

Disruption (Vurugu)

Ni hatua ambayo magunduzi mapya yanapotafuta soko jipya na athari huanza kuonekana hapo ndivyo kidogo kidogo Kodak ikaanza kushituka baada ya magunduzi ya Steven Sassoon. Na ndivyo biashara zisizo taka kubadilika huanza kuachwa na ushindani wa mbunifu mpya kuingia kwa mfumo mzuri.

Demonetization

Pale unapoondoa fedha katika mlinganyo basi ndo anguko la biashara hiyo. Ndivyo Kodak ilivyojikuta katika anguko baada ya watu kuacha kununua picha za nega ndio kufa kwake. Hivi ndivyo katika biashara nyingi hufa

Dematerialization

Kitendo cha fedha kutotumika katika kupata bidhaa au huduma hiyo. Kitendo cha kuwepo kamera za digitali zikapelekea kuja kwa simu janja ambazo zina kamera ambayo ni bure na haina gharama. Hivyo moja kwa moja anguko na kushuka kwa kamera katika mauzo. Hivyo pia kitendo cha simu kukusanya kamera, maktaba za vitabu, taa, kirekodi sauti, ramani, kikokotozi kumefanya kushuka kwa vifaa hivyo kama kila kimoja kingeuzwa kivyake

Democratization ( Uhuru wa kimawazo )

Kwa hatua hii hata kushirikishana picha kuna huru na kwa haraka zaidi. Hakuna gharama za kupiga picha, au kuchapa. Kila mtu ana huru wa kushirikishana picha kupitia majukwa ya mtandaoni siku hizi.

6. Watu wote wakuu na waloweza kufanya makubwa hata sasa athari yao kidunia inaonekana ni kuwa na lengo moja la kuwa na MAONO MAKUBWA. Watu wote walikuwa na wamekuwa hivyo wakifanya katika kuathiri Dunia. Mifano hai ya Bill Gates, Ellon Musk yatosha kuonyesha kwa namna gani wamekuwa na maono makubwa. Pia kwa eneo letu la nyumbani Watu kama Salim Bakhresa, Mo Dewji, Dkt. Reginald Mengi [ Marehemu kwa sasa, aliacha tawasifu yake I CAN, I MUST, I WILL- The Spirit of Success ] wanaongoza na sifa kubwa ya kuwa na Maono makubwa ambayo hugusa Maisha ya jamii kwa upana wake.

7. Makampuni au biashara nyingi zinaishia kuanguka na kufa sababu ya kukosa kuwa na picha ya wapi ndani miaka fulani watakuwa wapi? Au picha ya miaka 10 au 20 ijayo watakuwa wapi, kwa kuwa wengi huendelea kufanya na kutatua matatizo kama walivyofanya siku za nyuma na hatimaye kushindwa kwenda na kasi ya mabadiliko. Hii ilifanya Kodak ijikute ikishindwaa kuendana na kasi ya mabadiliko sababu ya kushindwa kuona mbali zaidi.

8. Teknolojia ya uchapishaji (3D.) inakua sana kwa kasi ikiwa katika hatua mojawapo ya teknolojia inayojizidisha siku hadi siku. Na inaambatana na ukuaji mkubwa wa mtandao na vitambuzi ikiwa ni mjumuiko wa viashiria na taarifa ambavyo ni ulinganifu wa interneti na ubongo wa binadamu ulivyo.

9. Kuna zaidi ya simu janja bilioni 7 [Kwa rekodi za 2019 na 2020] zilizopo ambazo zina viambatanisho vya vifaa vitambuzi kama mguso (touch screens), vipaza sauti, kamera na kadhalika. Na ukuaji wa teknolojia ya simu unazidi kwenda kasi sana huku kukiwa na matokeo mbalimbali ya simu kama iPhone na vifaa vingine kama iPads.

10. Dunia inaelekea katika zama za Utambuzi wa kisasa (Artificial intelligence) ambapo vifaa vimetengenezwa na kupata uwezo wa kuwasiliana na watu katika mitandao. Utakuwa umewahi kuona au kuzungumza na mtu katika mtandao kwa njia ya majibizano na ukadhani pengine ni mtu halisi lakini kumbe ni programu ambazo zimeweza kuchukua uwezo wa kuwasiliana na kujibu pale utafutapo huduma hasa katika mitandao.

11. Licha kukua kwa sayansi ya kufundisha vifaa kama komputa kuweza kuwasiliana bado eneo la akili ya hisia itakuwa tatizo kufikika kwa vifaa hivi kuliweza hilo liwepo.

12. Utengenezaji maroboti ni teknolojia inayokua kwa kasi sana duniani na kutabiri hofu KUBWA sana miaka inayokuja. Maroboti yamekuwa yakitumika viwandani, na hata katika huduma za kiafya kama upasuaji kwa nchi zilizoendelea kwa wingi. Kukua huku kwa matumizi ya roboti kunaendelea kuhatarisha namna mambo yatakayokuwa Duniani wakati ujao.

13. Sayansi ya vinasaba na biolojia ya matengenezo (genomics and synthetic biology) imezalisha madawa na hata kuathiri katika vyakula kwa utengenezaji wa bidhaa mbalimbali. Teknolojia ya ukuzishaji mimea, upatikanaji wa chanjo unazidi kushika kasi kadri muda unavyosogea kila siku.

14. Mirejesho katika huduma za kibiashara au huduma zozote zile za kiujuzi kwa wateja ni njia bora sana ya kuongeza ubunifu na kuongeza matoleo tofauti tofauti kufanya wateja wapate thamani zaidi na waone kuthaminiwa katika kuhudumiwa. Mfano kama vifaa vya kieletroniki mfano, televesheni, komputa na hata simu zimekuwa na matoleo tofauti ili kukuza uhitaji wa wateja wao. Hii mbinu ya mirejesho imeendelea kuzidisha biashara mbalimbali kote duniani. Tumia njia hii kupata mrejesho wa huduma zako kwa wateja wako ili ukuze na kukua kwa ukubwa na kuathiri dunia kwa upande chanya. Toa matoleo tofauti tofauti ya bidhaa zako au huduma.

15. Katika kuongeza ufanisi wa kazi kwa watu Duniani kote. Hili utaona namna kuongeza fedha kulipwa kwa watu kumekuwa kunaongeza hamasa na nguvu kwao kufanya zaidi. Licha Fedha na Kupandishwa madaraja ni hamasa ya nje (external rewards) lakini imeonyesha bado haitoshi kutoa hamasa ya kweli, kwa sababu kuna wengine licha kupata fedha na kulipwa bado utendaji kazi unakuwa si wa kifanisi. Hivyo hamasa ya ndani imekuwa inaonyesha namna imekuwa inaleta matokeo bora zaidi pale wanaofanya kazi wanapoona lipo kusudi, kuheshimika na ustadi katika kazi zao.

16. Kukua kwa Google na kufikia mamilioni ya watu Duniani kumekuwa na kanuni 8 za kibunifu ambazo unapoweza kuzitumia nawe katika maisha yako, biashara na maeneo mengine basi utapiga hatua kubwa sana na kufikia hatua ya kuathiri dunia katika tija.

  • FOKASI kwa Watumizi wa bidhaa au huduma zako ( Focus on the User )

Biashara inayojenga msingi wake katika kuona wateja wanataka nini inakua haraka sana. Na hii ndio siri kwa wafanyabiashara wakubwa Lary Page na Richard Branson kujenga Biashara ambazo mteja ni kiini katika mduara (Building customer -centric businesses)

  • SHIRIKISHA kila kitu ( share everything )

Katika Dunia yenye mwingiliano wa wingi wa maarifa na nafasi kwa kila mmoja. Huu ndio wakati mzuri wa kuachwa watu waweze wenyewe kubuni na kuzalisha mawazo. Mfano mzuri ni namna FACEBOOK ilivyo ambavyo watu wamekuwa huru kutumia na kushirikisha wingi wa maarifa na taarifa.

  • TAFUTA mawazo kila sehemu ( Look for ideas everywhere )

Uwepo wa kusanyiko la watu na namna wanavyoweza kuzalisha mawazo ni kama namna ya CROWDSOURCING jinsi inavyoweza kuzalisha mawazo, ufahamu, bidhaa na huduma.

  • FIKIRI kwa Ukubwa na Anza Kidogo ( Think Big but Start Small )

Unaweza kuanza kidogo na kuathiri kundi dogo la watu, na lengo lako kubwa ni kuathiri mabilioni ya watu katika milongo mingi (Inaweza kuwa miaka 10 mpaka miaka 50, 100).

  • Usishindwe kamwe Kushindwa ( Never Fail to fail )

Shindwa mara nyingi, jifunze haraka na upige hatua kubwa mbele.

  • Uwe Mjenzi wa Taswira kubwa ya Ukionacho ndani miaka ijayo, Jazwa na Taarifa sahihi ( Spark with imagination, Fuel with data )
  • Uwe Jukwaa ( Be a Platform )

Ukiangalia makampuni mengi makubwa ambayo yamekuja kwa kasi na kutengeneza mabilioni ya fedha ni kwa sababu ya kutengeneza majukwaa, mfano UBER, INSTAGRAM, tafuta jukwaa lako.

  • Uwe na lengo/Mkakati

Lengo ndio msingi wa kuendelea mbele kwa makampuni makubwa na biashara yoyote ile yenye kutaka kupiga hatua kubwa sana.

17. Kusoma kwa kufanya ni njia bora sana ya kutengeneza mtiririko wa ubora katika kuleta matokeo bora ya ufanyikaji kazi wowote ule wa kitu. Elimu ya Montessori ni elimu inayosifika Duniani kote kwa kuongoza katika elimu inayogusa mtiririko unahohusisha mifumo mingi ya hisi kwa pamoja (Multiple sensory streams at once). Unapofanya kwa mikono ndipo unapoufanya ubongo ukupe nafasi ya kuhusisha mifumo hisi yote kwa mara moja. Na hii inashika umakini na kufokasi kitu kwa wakati huo.

18. Moja ya siri ya kukua kwa ukubwa na ukaathiri Dunia ni kuhusisha nguvu ya pamoja ya watu wenye maono makubwa mamoja, urafiki wenye tija na maarifa bora. Na hii ndio siri iliyo wazi sasa kwako kuwa Apollo Program ilitokea kwa kuunganisha nguvu ya mambo haya kwa pamoja.

19. Njia nzuri ya kutabiri kesho yako ni kuitengeneza mwenyewe. Sentensi hii ni muhimu kwa kila mmoja ikiwa inataka kutufikirisha na kutuhitaji tuwe na picha kubwa ya kesho zetu katika biashara na maisha namna gani dunia itaathirika kwa uchanya.

20. Dunia inaathiriwa sana na watu wachache ambao hufikiri kwa ukubwa na wakawa tayari kuchukua hatua za hatari (TAKING GREAT RISKS). Mwandishi anataka tujifunze kwa watu 4 ambao wamegusa na kubadilisha Dunia katika kubadili namna tunahitaji kufikiri kitofauti na kwa ukubwa zaidi.

ELLON MUSK na maisha Safari ya Mars

Huyu ndiye Tesla wa karne hii kwa namna ya uwezo mkubwa sana wa kutengeneza utajiri wa mabilioni katika makampuni yake makubwa kama vile Space X, Tesla Motors na Solar Cities. Ufikiri wake huu na namna shauku yake kubwa ya kusafirisha watu kwenda katika sayari Mirihi (Mars) ambayo imekuwa na nafasi ya viumbe hai kuweza kuishi huko. Mbali ya kuzaliwa Pretoria nchini Afrika ya Kusini lakini anaonyesha historia yake namna kupenda kwake kufikiri zaidi kwa namna vitu vinavyofanya kazi ? (How things work). Na hii ndio siri kubwa ya mabilionea kuzidi kufanikiwa kwa kujua uhalisia wa mambo.

SIR RICHARD BRANSON na Virgin Groups

Kutoka katika hali ya chini. Sir Richard Branson ni moja ya watu wenye utajiri mkubwa sana na wingi wa makampuni mengi zaidi ya 400 anayoyaongoza ambayo yapo katika chapa yake ya Virgin na shauku yake kubwa inaonyesha namna ambavyo anatumia nafasi ya kuwekeza katika biashara ya usafiri wa anga na kutumia fursa katika kufanya mambo makubwa sana kunavyotanua soko lake.

JEFF BEZOS na Amazon.com

Alizaliwa huko New Mexico mwaka 1964, na kwa orodha ya Forbes ni tajiri asiyekosa kuwa 10 bora za matajiri wakubwa Duniani [ingawa zimekuwa zikipanda na kushuka]. Ni mtu aliye na kazi nyingi sana na hufika wakati anatafuta namna ya kutunza muda katika upigaji mswaki wake. Huyu ndiye muasisi na mtu aliyewekeza katika uuzaji wa bidhaa kama vitabu akiwa na chapa yake ya Amazon. Na mafanikio yake makubwa ni sababu ya mikakati mikubwa miwili ya Kufikiri kwa malengo ya mbali (long-term thinking) na kufikiri kwa mteja kama kiini katika mduara (customer ~ centric thinking).

LARY PAGE na Google Search

Alizaliwa huko Michigani mwaka 1973 toka katika kuzaliwa kwake ni kama asili katika familia yao ya upenzi mkubwa juu ya komputa. Mama yake Grolia alikuwa ni Profesa wa Sayansi ya Komputa huko huko Michigani na Baba yake Carl alikuwa mtafiti katika sayansi ya komputa na Utambuzi wa kisasa (Artificial Intelligence). Naye ni tajiri asiyekosa katika 20 bora za matajiri Duniani na matajiri 10 vijana Duniani kulingana na machapisho kama Forbes. Ugunduzi wake wa Google umefanya utafutaji wa maarifa uwe rahisi sana na kumtengenezea mabilioni ya fedha. Amekuwa ni mmoja wa watu ambao wamefanya watu watoke katika kufikiri kawaida na kuona mambo katika sura ya kitofauti.

Watu hawa mashuhuri wanatia sana hamasa kujifunza kwa kina maisha yao, vitabu vilivyoandikwa kuhusu wao na kutembelea baadhi ya mahojiano walowahi kuyafanya katika mitandao ya kijamii.

21. Kutengeneza jukwaa kwa ajili ya kuzalisha mawazo mengi inahitaji pawe na jumuia moja ambayo itakuwa tayari katika kuwa na muda na kuona namna gani watatua matatizo au kuunganisha mawazo pamoja na kuleta utatuzi.

22. Jamii inaathiriwa kwa upande chanya pale inapokuwa pamoja na inahusika moja kwa moja kwa kila mmoja katika kukutana na kujadili mambo mbalimbali, mahojiano na matamasha yanayowaleta pamoja kujadili mambo yanagusa maisha yao ya kila siku

23. Njia ya kutoa “TUZO” na zawadi kwa watu ni njia bora ambayo inaweza ikatumika katika kutatua matatizo mbalimbali na kuhamasisha ubunifu na magunduzi. Kwanini tuzo au zawadi zinafanya kazi. Mosi inampa mtu kutoa uwezo wake mkubwa wa ndani wa kibunifu, utambulisho na kumpa fedha mtu. Hivyo utatuzi wa changamoto kubwa katika jamii yoyote ile unaweza kupata majibu pale mashindano ya atakayekuja na majibu kupewa tuzo au zawadi

24. Uaandaji wa tuzo unavuta wafadhili na ni njia ya kufanya kitu au jambo hilo lianze kufuatiliwa na umma. Tuzo zinasaidia katika kubadili mtizamo wa watu juu ya mambo yalivyo huku pakiwepo nafasi ya kutengeneza soko kwa yule atakayekuwa kashinda baada ya uaandaji wa tuzo wa kishindani (The power of incentive competitions).

25. Neno la mdomo ni njia moja nzuri sana ya kukuza jamii. Na hivi ndivyo mbinu ya kufanya biashara au bidhaa ienee kwa watu wengi zaidi. Maana watu hushawishika kwa kitu au bidhaa ambayo kila mtu akiizungumzia.

Hiki ni kitabu kizuri ambacho kinaendelea kuwa mwongozo mzuri wenye maelezo ya kiundani zaidi namna ambavyo teknolojia inavyoenda kasi na kuathiri mambo mengi katika maisha ya sasa na hapo baadaye.

Vitabu vingine ambavyo mwandishi huyu Daktari ni “Abundance: The Future Is Better Than You Think” na “The Future Is Faster Than You Think; How Converging Technologies Are Transforming Business, Industries, and Our Lives (Exponential Technology Series)

Mchambuzi
Dkt. Raymond N Mgeni, raymondpoet@yahoo.com  +255 676 559 2211