Kutaka kuibadili dunia ni kauli ambayo imekuwa inatumiwa na watu wengi.
Wengi hujiambia ndoto yao ni kutaka kuibadili dunia, kupitia kile wanachofanya.
Lakini wengi siyo tu huwa wanashindwa, bali wanaishia kuiharibu dunia.
Dunia haihitaji kubadilishwa, dunia imekuwepo, ipo na itaendelea kuwepo.
Wajibu wetu sisi ni kuielewa dunia na kisha kuyafanya maisha yetu hapa duniani kuwa bora zaidi.
Labda nitumie mfano ili tuelewane vizuri;
Vitu vyote vipya unavyoviona hapa duniani, havijatokana na kuibadili dunia, bali kuielewa dunia.
Tukianza na uvumbuzi wa moto, haukuja kwa sababu mtu aliibadili dunia, bali ulikuja kwa sababu mtu aligundua nguvu ya msuguano inazalisha moto. Msuguano kuzalisha moto siyo kitu kipya, kimekuwepo kwenye asili wakati wote, ila utambuzi wake haukuwepo.
Kadhalika kwenye kila aina ya teknolojia, mfano maporomoko ya maji na upepo yamekuwepo wakati wote, lakini ni karne chache zilizopita ndiyo watu walipata utambuzi kwamba vitu hivyo vinaweza kuzalisha umeme.
Jua limekuwepo tangu kuwepo kwa ulimwengu, limekuwa linawaka kila siku bila kuacha, limekuwa linatumika na mimea kuzalisha chakula, lakini ni karne za karibuni ndiyo watu wameweza kupata utambuzi kwamba jua linaweza kuzalisha umeme.
Hivyo unaweza kuona hapo, unachohitaji siyo kuibadili dunia, siyo kujibadili wewe wala kumbadili yeyote, unachohitaji ni kuielewa dunia, kujielewa mwenyewe na kuwaelewa wengine, kisha kutumia uelewa huo kuyafanya maisha kuwa bora kwa kila mtu.
Mwanafalsafa na mwandishi Albert Camus amewahi kusema binadamu ndiye kiumbe pekee ambaye anakataa kuwa yeye. Hili ni kweli na liko dhahiri. Viumbe wengine wote wanakubali kuwa wao, wanajitambua wao na kisha kuendesha maisha yao kwa namna hiyo.
Lakini binadamu anakazana kuwa tofauti na alivyo na hilo ndiyo chanzo cha msongo, kukosa furaha na kukosa uhuru kwenye maisha. Unapotaka kujibadilisha, kuwa tofauti na ulivyo, ndiyo unaingia kwenye mitego mbalimbali inayoharibu maisha yako.
Kila unapofikiria kuibadili dunia, kujibadili mwenyewe au kuwabadili wengine, acha kujidanganya, fikiria kilicho sahihi ambacho ni kuielewa dunia, kujielewa mwenyewe na kuwaelewa wengine. Ukishakuwa na uelewa na ukautumia vizuri, utayafanya maisha kuwa bora kwako, kwa dunia na kwa wengine pia.
Usihangaike na mabadiliko, hangaika na kujitambua.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Ahsante Sana kocha kwa makala hii ya kurasa wa leo,kwa kweli nahitaji kujitambua mwenyewe, kujitambua mwenyewe na kuwatambua wengine vile walivyo. Badala ya kukazana kuibadili dunia, kuwa badili wengine na kujibadili Mimi mwenyewe.
LikeLike
Karibu Tumaini.
LikeLike
Asante sana kocha,kujitambua na kujiishi mimi, kwenye semina ya kisima cha Maarifa tarehe 15/11/2020 hii ilikuwa sehemu ya semina yetu, hakika semina na mafunzo ni muhimu kwetu ili kujiongezea Elimu na Maarifa ktk kuchukua hatua sitahiki ktk maisha yetu ya Mabadiliko na uchumi.
LikeLike
Vizuri sana Beatus.
LikeLike