Watu wengi wamekuwa wanashindwa kufanya maamuzi yenye manufaa kwao, hasa pale maamuzi hayo yanapokuwa muhimu na magumu.

Hiyo inatokana na kutoyapa uzito wa kutosha maamuzi hayo na kutengeneza mazingira yatakayosaidia maamuzi hayo yawe bora.

Wengi wanaruhusu hali fulani ziingilie maamuzi yao kitu kinachofanya yasiwe bora.

Kuna makosa matatu ambayo watu wamekuwa wanayafanya wakati wa maamuzi na yanawagharimu.

Kosa la kwanza ni kuruhusu hisia ziwatawale wakati wa kufanya maamuzi. Tunajua siku zote hisia zikiwa juu basi fikra zinakuwa chini, hivyo maamuzi yoyote ambayo mtu anayafanya kwa hisia huwa siyo sahihi kwa sababu anakuwa hajafikiri kwa kina.

Kosa la pili ni kuruhusu usumbufu na kelele za wengine kumvuruga mtu wakati wa kufanya maamuzi. Chochote unachosikia, kina nguvu ya kuyumbisha maamuzi unayotaka kufanya.

Kosa la tatu ni kutokuwa na maarifa sahihi, hasa kukosa takwimu za kumwongoza mtu katika kufanya maamuzi. Wengi wanaishia kufanya maamuzi muhimu kwa mazoea ya nyuma, wakati vitu vingi vinakuwa vimeshabadilika.

Huwezi kukwepa kabisa mambo haya matatu, hisia zinakuja hata kama huzitaki, kelele za wengine zitakuzunguka kila mara na mazoea ni magumu kuvunja.

Muhimu ni kujua wakati unapohitaji kufanya maamuzi magumu na kuhakikisha hali hizo tatu unazizuia zisiathiri maamuzi yako.

Jitambue wakati hisia zako ziko juu na jizuie kufanya maamuzi yoyote. Subiri mpaka hisia zimetulia, liangalie jambo jinsi lilivyo kisha lifanyie maamuzi.

Pia pata utulivu mkubwa wakati wa kufanya maamuzi. Unaweza kupokea ushauri wa wengi uwezavyo, unaweza kusikiliza shuhuda na hadithi za wengine, lakini unapofika wakati wa kufanya maamuzi, jipe utulivu mkubwa. Jua maamuzi unayafanya kwa ajili yako na matokeo yake utakabiliana nayo wewe na siyo mwingine yeyote.

Na muhimu zaidi, pata maarifa sahihi kabla hujakimbilia kufanya maamuzi, jua takwimu sahihi, jua yale ya msingi kabisa kwenye swala husika kabla hujafanya maamuzi. Kuwa makini sana hapa, hatuzungumzii maoni yako au ya wengine, bali tunauzungumzia ukweli, lazima uujue ukweli jinsi ulivyo kabla hujakimbilia kufanya maamuzi yoyote yale.

Tukizingatia haya, tutaweza kufanya maamuzi ambayo ni bora kabisa na hata tukikosea, tutajua namna bora ya kubadili na kuboresha.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha