Watu wote ambao wamewahi kupita hapa duniani na mpaka leo bado tunawakumbuka wana sifa moja. Kuna wakati walipinga kile ambacho kila mtu aliamini na kuja na ambacho ni sahihi.

Wakati wanafanya hivyo haikuwa rahisi kwao, walikutana na ugumu, walikatishwa tamaa na hata kuhujumiwa, wapo ambao walifungwa na wengine kuuawa. Lakini hawakukubali kuacha kile walichoamini ni sahihi ambacho wengi walipinga siyo sahihi.

Chukua mfano wa Galileo Galilei, ambaye alikataa kukubaliana na kilichoaminiwa na wote kwamba jua linazunguka dunia. Alipingwa na kufungwa kwa sababu alionekana kudanganya watu. Lakini alikuwa sahihi na mpaka leo tunamkumbuka. Wale waliompinga na kumfunga hawakumbukwi leo.

Hivi unajua mashine ya kwanza ya kushona nguo ilipingwa na kuharibiwa vibaya? Hata treni ya kwanza ilipingwa sana, watu waliamini kusafiri kwa kasi zaidi ya iliyozoeleka kwa farasi itapelekea mzunguko wa damu kusimama na mtu kufa. Ugunduzi wa ndege haukuwa rahisi, watu walipinga na kuwaona vijana waliokuwa wakifanyia kazi hilo kama wamechanganyikiwa.

Kila mtu unayemjua leo, aliweza kusimama peke yake wakati dunia nzima inampinga.

Sasa tuachane na hao, tuje kwako wewe. Ni kitu gani unajua na kuamini ni sahihi, lakini jamii inakipinga? Kupitia uzoefu wako, elimu na ujuzi uliopata, ni nini unachojua ni sahihi kabisa, lakini wengi wanakwenda kinyume na hicho?

Hapo ndipo ilipo nafasi yako ya kuacha alama hapa duniani. Kwa kuchagua kusimamia kitu hicho, kutafuta kukijua kwa undani na kuonesha matokeo yake mazuri badala ya kupiga kelele na wanaokipinga au kukikosoa.

Ukiweza kusimamia hicho, kwa namna ambayo kinaongeza thamani kwa wengine, utaweza kuacha alama hapa duniani. Unaweza usiyaone matokeo yake sasa, lakini jua yatatokea tu.

Uzuri wa ukweli ni kwamba huwa hauhitaji kulazimishwa au kubembelezwa na pia hauna haraka. Huwa unabaki kuwa ukweli na hata upingwe kiasi gani, kuna siku utajidhihirisha wenyewe.

Ni ukweli upi unaoujua ambao wengi wanaupinga na kuupuuza, usimamie huo na utaweza kufanya makubwa na kuacha alama hapa duniani.

Unachopaswa kujua ni kwamba mara nyingi ukweli huwa haukubaliwi na wengi, hivyo ukiona kitu wengi wanakikubali, kuna nafasi kubwa kwamba siyo kweli. Tumia hilo katika kupima chochote unachofanya.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha