Makala hii ni kwa wale ambao siyo wanachama wa KISIMA CHA MAARIFA.

Kwenye KISIMA CHA MAARIFA tulishaacha kuanza mwaka mpya tarehe moja mwezi Januari, badala yake tunauanza mwaka mpya wa mafanikio wiki ya kwanza ya mwezi Novemba.

Hivyo wakati kwa watu wa kawaida leo ni siku ya mwaka mpya, kwa wanachama wa KISIMA CHA MAARIFA tayari mwaka umechanganya, na umechanganya hasa maana tulishaweka mipango na kuanza utekelezaji wake mapema.

Kwa wale ambao hamjapata nafasi ya kuwa kwenye KISIMA CHA MAARIFA, leo nina ujumbe mfupi sana kwenu, kwa sababu ninyi pia ni marafiki zangu na ninawajali sana, hivyo kila wakati nawashirikisha maarifa yanayowawezesha kufanya maamuzi sahihi ya kufika kwenye mafanikio makubwa.

Kwa kuwa leo na siku chache zijazo utakuwa kwenye hali ya hamasa ya juu kwa mwaka mpya 2021, ninataka nikutahadharishe vitu muhimu mno, ili usije kuupoteza mwaka huu kama ambavyo umekuwa unafanya kwenye miaka mingine.

Kila mwaka tarehe kama hizi umekuwa unasema MWAKA MPYA MAMBO MAPYA, unaanza na hamasa kubwa malengo na mipango mbalimbali, lakini wiki tatu baadaye unakuwa umerudi kwenye mazoea yako ya nyuma na kusubiri tena mwaka mwingine mpya ufike.

Sitaki hilo litokee tena kwako mwaka huu 2021, nataka huu ukawe mwaka wa alama kwako na uweze kushika hatamu ya maisha yako bila ya kusubiri siku fulani kama ya leo.

Yafuatayo ni mambo 10 muhimu ya kuzingatia mwaka huu 2021 ili uwe bora na wa kipekee sana kwako.

1. Usitabiri chochote kuhusu mwaka huu, hakuna mwenye uwezo wa kutabiri jambo lolote kwa uhakika wa asilimia 100. Mwaka 2020 umetupa funzo kubwa, wakati unaanza wengi walitabiri mengi, lakini hakuna aliyeweza kutabiri janga la Covid 19 na jinsi lingeitikisa dunia.

Hivyo badala ya kupoteza muda wako kutabiri chochote kile, kuwa tayari kukabiliana na kila kitakachokuja na kuhakikisha unaendelea na safari ya maisha bila ya kuanguka na kukata tamaa.

2. Punguza mambo ya kufanya na siyo kuongeza. Kila mwaka umekuwa unaongeza mambo ya kufanya, unajiambia mwaka huu nitafanya hiki au kile. Mwaka huu 2021 kuwa tofauti, tayari una mengi ya kufanya, hivyo huu ufanye mwaka wa kupunguza mambo unayofanya.

Chukua kalamu na karatasi, orodhesha mambo yote ambayo umekuwa unafanya kila siku kwa mwaka 2020 ulioisha. Kisha kwa kila jambo angalia lina mchango gani kwako kukufikisha kwenye mafanikio makubwa. Kwa yale uliyokuwa unafanya na hayajachangia chochote, jiambie hutayafanya mwaka 2021.

Kipimo kizuri cha kutumia ni AFYA, HEKIMA NA UTAJIRI. Kama kuna kitu umekuwa unafanya na hakichangii kwenye hayo matatu, acha kukifanya 2021. Na hapo kuna mengi utayapunguza, mfano mitandao ya kijamii, kufuatilia habari, kubishana, kuwa na chuki na vinyongo na wengine, kufuatilia maisha ya watu n.k.

Ukishapunguza ya kufanya, unakuwa na muda zaidi wa kuweka kwenye yale yanayochangia kukufikisha kwenye mafanikio.

3. Jijengee tabia bora kwa mafanikio. Huwa tunajenga tabia na kisha tabia zinatujenga. Asilimia zaidi ya 60 ya mambo unayofanya kila siku ni tabia, yaani unayafanya bila ya kufikiri kabisa.

Mabadiliko yoyote unayotaka kuleta kwenye maisha yako kwa mwaka 2021, anza kwa kujijengea tabia ambayo itafanya kitu hicho kiwe rahisi.

Jijengee tabia za mafanikio, zungukwa na wanye tabia sahihi na mabadiliko unayoyataka yatakuwa rahisi kwako.

4. Usihangaike na malengo, bali hangaika na mfumo. Kila mwaka umekuwa unaweka malengo na yamekufikisha wapi? Mengi sana umekuwa unaanguka, kwa sababu umekuwa unaweka malengo kwa kusukumwa na hisia na siyo kuangalia uhalisia.

Dawa ya hiyo ni kujijengea mfumo wa wewe kupata kile unachotaka. Uzuri wa mfumo ni kuwa unafanya kazi mara zote, hautegemei hamasa.

Kwa mfano kama unapanga kuandika kitabu mwaka 2021, jiwekee mfumo wa kuandika maneno angalau 500 kila siku bila kuacha hata siku moja. Kwa mwaka utakuwa umeandika zaidi ya maneno laki moja ambayo ni kitabu kikubwa.

Kama unataka kuweka akiba zaidi 2021, weka mfumo wa kukata asilimia 10 ya kila kipato chako na kuweka mahali ambapo huwezi kuigusa hata uwe na shida kiasi gani.

Chochote unachotaka kufikia, jiwekee mfumo ambao utaufuata bila kuacha na utashangaa jinsi utafanya makubwa 2021.

5. Fanyia kazi eneo lako la kifedha. Hapa kuna mambo manne muhimu sana unayopaswa kuyafanyia kazi 2021.

Moja ni kuongeza kipato chako, kupitia kazi au biashara unayofanya, kazana kuongeza kipato chako, na fanya hivyo kwa kutoa thamani zaidi.

Mbili ni kudhibiti matumizi yako, matumizi huwa yana tabia ya kukua kadiri kipato kinavyokua. Kama hutadhibiti matumizi yako, kipato kinachoongezeka kitamezwa. Jiwekee kabisa bajeti ya kila mwezi kwa mwaka 2021 na ishi kwa bajeti hiyo tu, usizidishe kwa namna yoyote ile.

Tatu ni kuwa na akiba ya dharura, ambayo inakuwezesha kuendesha maisha yako kwa miezi 6 mpaka 12 hata kama hutakuwa na kipato kabisa. Bajeti yako ya mwezi, kisha zidisha mara 6 na hicho ndiyo kiasi cha akiba ya dharura unayopaswa kuwa nayo.

Nne ni kuwekeza, fanya uwekezaji unaokua thamani na kuzalisha faida. Kama ni mgeni kabisa, anza na UTT AMIS ambapo kuna mifuko mbalimbali ya uwekezaji unayoweza kuanza kidogo na kuendelea kuwekeza mara kwa mara.

Soma kitabu cha ELIMU YA MSINGI YA FEDHA, utaweza kupata ufafanuzi wa kina wa maeneo hayo manne na hatua sahihi kuchukua.

6. Anzisha au kuza zaidi biashara yako 2021. Kama bado hujawa na biashara, mwaka 2021 ndiyo wa kuanza biashara, usikubali kuahirisha tena, anza sasa. Kama tayari upo kwenye biashara, mwaka 2021 ni wa kuikuza zaidi biashara yako, usikubali kuendelea kubaki hapo ulipo.

Pata na usome kitabu cha ELIMU YA MSINGI YA BIASHARA na uweze kupata maarifa sahihi ya kuanzisha na kukuza zaidi biashara yako.

Kupata vitabu hivyo viwili nilivyoeleza hapo huu, wasiliana na 0752 977 170 na utatumiwa au kuletewa ulipo.

7. Soma angalau kitabu kimoja kila mwezi kwa mwaka 2021. Unahitaji maarifa zaidi ili kuweza kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazojitokeza kwenye maisha. Mwaka 2020 umetufunza mengi, hatujui nini kitakuja 2021, lakini unapokuwa na maandalizi sahihi, unaweza kukabiliana na chochote.

Kusoma angalau kitabu kimoja kila mwezi kwenye maeneo ya maendeleo binafsi, fedha, biashara, falsafa na mengine kutakufanya kuwa bora zaidi. Kupata vitabu vizuri vya kusoma pamoja na chambuzi zake karibu ujiunge na channel ya SOMA VITABU TANZANIA. Kujiunga na channel hiyo fungua; www.t.me/somavitabutanzania

8. Pata muda wa kufikiri. Tumekuwa bize mno, kwa mambo ambayo hata hayana tija, kila siku unaianza na kuimaliza siku ukiwa umechoka na huoni hatua unazopiga. Yote hiyo ni kwa sababu unayaendesha maisha yako bila kufikiri, unadhani unafikiri kumbe unafuata mkumbo tu. Tenga angalau siku moja kila wiki ya kuwa na muda wa kufikiri. Kwenye siku hiyo hakikisha hakuna usumbufu wowote unaokufikia, ni wewe na fikra zako tu. Fikiri kwa kina kuhusu maisha yako, ulikotoka, ulipo na unapokwenda, kisha pima hatua unazochukua kama ni sahihi. Kama huwezi kupata siku moja kwa wiki basi hakikisha unapata siku moja kwa mwezi ya kufikiri.

9. Dhibiti vizuri rasilimali hizi mbili muhimu; muda na nguvu. Hizi ni rasilimali mbili muhimu mno na zenye ukomo, una masaa 24 tu kwa siku, hata ufanyeje, huwezi kuongeza hata sekunde moja. Nguvu zako pia zina ukomo, unapoianza siku unakuwa na nguvu kubwa, lakini kadiri muda unavyokwenda nguvu hizo zinapungua. Hivyo kabla hujaianza siku yako, weka vipaumbele vyako kwa usahihi, hakikisha muda na nguvu zako zinakwenda kwenye yale mambo yanayochangia wewe kuwa na AFYA bora, HEKIMA na kuongeza UTAJIRI wako. Hayo ni maeneo matatu ya kupima vipaumbele vyako, chochote ambacho hakichangii kwenye hayo matatu, usikubali kichukue muda na nguvu zako 2021.

10. Kuwa na mtu wa kukuzuia usitoroke. Kila mwaka umekuwa unaweka malengo lakini huyafikii, hiyo ni kwa sababu mambo yanapokuwa magumu, umekuwa unatoroka, unaachana na malengo hayo na kurudi kufanya vitu rahisi ambavyo haviwezi kukufikisha kwenye mafanikio. Mwaka 2021 chagua mtu ambaye hatakuruhusu utoroke, mtu unayemheshimu na hutaki kuvunja heshima yake, au mtu unayemlipa ambaye ukitoroka itabidi umlipe kiasi kikubwa cha fedha. Kisha mshirikishe mpango wako wa mwaka 2021 na kila mwezi mpe tathmini ya hatua ulizochukua na matokeo uliyopata. Kama umejitoa kweli kubadili maisha yako 2021, hakikisha una mtu wa aina hii, kama huna, unajidanganya tu.

Fanya mambo hayo kumi na mwaka huu 2021 utakuwa mwaka wa kuyabadili maisha yako kweli na siyo mwaka wa kupiga kelele kama ya nyuma.

Karibu sana tuendelee kuwa pamoja, nitaendelea kukushirikisha maarifa sahihi na yenye hatua za kuchukua ili uweze kufikia mafanikio makubwa kwenye maisha yako.

Rafiki, karibu upate na kusoma vitabu vizuri vya maendeleo binafsi na mafanikio kwa lugha ya Kiswahili. Pakua na weka app ya SOMA VITABU na upate maarifa sahihi. Kwa maelezo zaidi fungua; https://amkamtanzania.com/somavitabuapp

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali.