Hii ndiyo njia ambayo dunia imekuwa inatumia kuwahadaa watu wasifanikiwe.

Kila unapopanga na kuamua kuweka umakini wako kwenye yale muhimu zaidi kwako, hapo hapo dunia inakuja na kitu kipya na kinachoonekana kizuri, ambacho unaona hupaswi kupitwa.

Unaacha ulichopanga na kuhangaika na kitu hicho kipya, baadaye unakuja kugundua haikuwa sahihi kwako. Unapanga kurudi kwenye mipango yako, lakini hujafika mbali dunia inakuja tena na kitu kipya.

Elon Musk amewahi kuweka picha kwenye mtandao wa Twitter akionesha picha inayobeba ujumbe huu, kwamba kila anapoamua kuweka umakini kwenye mambo yake ili awe na uzalishaji mzuri, dunia inakuja na kitu cha kuhadaa. Kwenye picha alitumia mfano wa Bitcoin lakini inaweza kubeba mfano mwingine wowote.

Ni kama dunia inakupima na kukujaribu kuona umejitoa kiasi gani kupata unachotaka, kwa sababu huwa haipendi kuwapa mafanikio watu wasio na msimamo, wasiojua nini hasa wanataka na wasiokuwa tayari kulipa gharama kupata wanachotaka.

Wewe mwenyewe utakuwa umeshuhudia hili kwenye maeneo mengi ya maisha yako, kila unapopanga kuwa ‘serious’ kweli kweli na maisha yako, ndipo hapo dunia inakuja na vitu vipya na vinavyoonekana vizuri, ambavyo hutaki kupitwa.

Dawa ya hili ni kujua kwamba vitu vipya na vinavyoonekana vizuri havitaacha kuja kwako, hivyo usikimbizane navyo, badala yake pambana na kile kilicho sahihi kwako.

Jua nini unataka, jua gharama unayopaswa kulipa, jitoe kuilipa na jipe muda kisha acha kukimbizana na vitu vipya vinavyokuja kwako kila wakati.

Kadhalika kwenye usumbufu, kila wakati utasikia kuna habari mpya, habari mpasuko, burudani mpya, viwanja vipya vya kujivinjari na mengine kama hayo.

Usipoweka kipaumbele na umakini wako wote kwa vile ambavyo ni muhimu kwako, vitu vipya vinavyokuja kwako vitakuwa vinakuyumbisha na kukusumbua kila wakati.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha