2301; Kinachokukasirisha kikutofsutishe…

Sheria ya kwanza na muhimi sana kwenye biashara ni kuwa na kitu kinachokutofautisha na wafanyabiashara wengine.

Kuwa na kitu au vitu ambavyo wateja wanavipata kwako tu na hawawezi kuvipata sehemu nyingine yoyote.

Yaani hata kama bidhaa au huduma yako itaondolewa jina na nembo, bado mteja aweze kuitambua ni yako.

Kupata mfano mzuri, angalia makampuni makubwa duniani. Cocacola hata ikiwekwa kwenye ndoo isiyo na jina au nembo yoyote, ukiinywa utajua ni Cocacola.

Iphone hata ukafuta jina na nembo, ukiishika hata kabla hujaiwasha, unajua hii ni Iphone.

Mifano ni mingi, lakini hapo umepata picha nzuri.

Sasa malalamiko ya wengi yamekuwa ni hawana cha kuwatifautisha.

Wafanyabiashara wengi wadogo na wa kati wanaofanya biashara za rejareja na kawaida huamini hawana cha kuwatofautisha, hivyo hufanya tu kwa mazoea.

Lakini hiyo ni njia ambayo biashara haiwezi kukua, kwa sababu kama hakuna ambacho wateja wanapata kwako na hawapati kwa wengine, hawatakuwa na sababu ya kuja kwako.

Kila biashara inaweza kujitofautisha na nyingine kwa kuanzia kwenye hasira.

Wewe kama mmiliki wa biashara, kuna vitu ambavyo ukienda kwenye biashara nyingine vinakukasirisha sana.
Hivyo ndiyo vitu ambavyo unaweza kuvitumia kujitofautisha.

Kwa kila biashara unayofanya au unayopanga kuanza, jiulize ni vitu gani huwa vinakukasirisha sana unapoenda kwenye biashara za wengine wanaofanya biashara ya aina hiyo.

Viorodheshe vitu hivyo kisha jenga biashara ambayo haina kero hizo kabisa. Hapo utakuwa umejenga biashara inayojitofautisha kabisa na nyingine.

Pia sikiliza maoni ya wateja wanaolalamikia biashara yako na za wengine, fanyia kazi yale wanayolalamikia na utaona jinsi biashara inaaminiwa zaidi na kuwa na wateja wengi.

Uzuri ni kwamba kila biashara huwa ina malalamiko ambayo wateja wake wanakuwa nayo. Hivyo ukiwa mdadisi mzuri, utajua malalamiko ya wengi kwenye aina yako ya biashara ni yapi na yageuze kuwa kitu cha kukutofautisha.

Ni kweli kutatua malalamiko mengi itakuingia gharama na hapo itabidi uwatoze wateja wako zaidi. Na watakuwa tayari kulipa zaidi kwa sababu wanaiona tofauti.

Kama ambavyo Tecno na Iphone zote zinafanya kazi inayolingana, lakini moja ni ghali mara kumi ya nyingine.
Ule uhakika unaopatikana kwenye moja unaifanya iwe gharama kubwa na watu kuwa tayari kulipia gharama hiyo ili kuupata.

Watu wapo tayari kulipa gharama kubwa ili kupata uhakika. Hivyo usiogope kuwekeza zaidi kwenye biashara yako kuwapa uhakika huo.

Chochote kinachokukera na kukukasirisha kwenye biashara yako na za wengine, kitumie kama sehemu ya kujitofautisha kibiashara.

Kocha.