Rafiki yangu mpendwa,
Hata uwe umetingwa kiasi gani, kila siku lazima utenge muda na kula chakula.
Sijawahi kukutana na mtu anayesema kwa wiki nzima hajala chakula kwa sababu hajapata muda.

Huo ni upande mmoja wa kulisha mwili wako.
Lakini upo upande mwingine wa kuusafisha. Kila siku lazima uusafishe mwili wako na kuuvalisha mavazi ili kuusitiri.
Hujawahi kutoka nyumbani ukiwa uchi kwa sababu huna muda wa kuvaa.

Ni muhimu kwako kula kila siku na hivyo unatenga muda wa kula, hata iweje huwezi kutotenga muda huo.
Ni muhimu kwako kuoga na kuvaa nguo kila siku na hivyo unatenga muda wa kufanya hivyo.
Pamoja na kulalamika mambo ni mengi na muda ni mchache, hujawahi kukosa muda wa kufanya hayo muhimu kabisa kwako.

Lakini kipo kitu kimoja chenye umuhimu kwako kama hivyo viwili nilivyoshirikisha hapo juu, ila umekuwa hukipi uzito wa kutosha.
Kitu hicho ni kulisha na kusafisha akili yako.

Kama unavyoulisha mwili wako chakula, unapaswa pia kuilisha akili yako chakula. Na chakula cha akili ni usomaji wa vitabu.
Kama unavyousafisha mwili wako na kuuvalisha mavazi,  ndivyo pia unapaswa kuisafisha akili yako na kuivalisha. Chakula na mavazi ya akili ni usomaji wa vitabu.

Kwa maana hiyo basi, kama husomi vitabu maana yake unatembea na akili yenye utapiamlo.
Kama husomi vitabu unatembea na akili chafu na iliyo uchi.
Haishangazi kwa nini matatizo na changamoto mbalimbali zinakuandama.

Mwili ukikosa chakula unakuwa dhaifu na kushambuliwa na magonjwa mbalimbali.
Akili ikikosa maarifa inakuwa dhaifu na kudhambuliwa na changamoto mbalimbali.

Kama unataka kuwa imara, iweze kukabiliana na kila aina ya changamoto inayokuja kwako na kuishinda, basi lisha akili yako maarifa sahihi.

Abraham Lincoln amewahi kusema akipewa masaa 6 ya kukata mti, atatumia masaa manne kunoa shoka lake. Kwa sababu anajua shoka likiwa kali, kazi itakuwa rahisi. Shoka ni akili yako, inoe kupitia usomaji ili uweze kufanya vizuri kile unachofanya.

Na jenerali Jim Mattis akasema kama hujasoma mamia ya vitabu ni sawa na mtu asiyejua kusoma na kuandika, utakuwa dhaifu na changamoto zitakuangusha kwa sababu uzoefu wako mwenyewe haukutoshi kupambana kwenye haya maisha.

Mimi mwenyewe, kutoka ndani ya nafsi yangu, huwa ninaamini kabisa mtu ambaye hasomi vitabu ana mtindio wa ubongo. Haiwezekani mbele yako kuwe na njia ya uhakika kabisa ya kukusaidia kupata unachotaka halafu huitumii na ukawa na akili sahihi.

Ujumbe mkuu hapa rafiki yangu ni soma vitabu.
Siri za mafanikio zimefichwa kwenye vitabu.
Changamoto yoyote unayokabiliana nayo sasa majibu yake yako kwenye vitabu.
Hamasa unayohitaji ili kujituma zaidi kila siku ipo kwenye vitabu.

Usikubali kuendelea na maisha ya sasa ambayo yanakuwa magumu kwako kwa sababu hujanoa shoka lako.
Usikubali kuendelea kujipa sababu kwamba husomi vitabu kwa sababu huna muda wa kusoma, unao sana au huna fedha za kununua, vingi unavipata bure kabisa.

Kila siku soma angalau kurasa kumi za kitabu.
Kurasa nne unapoamka, kurasa tatu unapokula mchana na kurasa tatu kabla hujalala.
Kama huwezi kusoma kurasa 10 tu za kitabu kila siku, mbegu ya mafanikio makubwa haipo ndani yako na utataabika sana na haya maisha.

Karibu upate vitabu mbalimbali vya kusoma kwa kufungua www.amkamtanzania.com/vitabu na www.t.me/somavitabutanzania

Na kama unahitaji kusimamiwa kwa karibu ili uweze kusoma vitabu na kuyatumia maarifa unayopata kuboresha maisha yako, tuwasiliane kwa wasap 0717 396 253.

Rafiki yako anayekupenda sana,
Kocha Dr Makirita Amani.