Rafiki yangu mpendwa,
Ushauri maarufu sana inapokuja kwenye swali la kazi au biashara gani mtu afanye umekuwa ni mtu afuate shauku yake.

Watu wamekuwa wanashauriwa wafanye kile wanachopenda na mafanikio yatakuwa yao.
Ushauri huu umekuwa unafanya wengi waamini kwamba kama bado hawajafanikiwa, ni kwa sababu hawajajua wanachopenda.

Cal Newport hakubaliani na ushauri huo maarufu. Na hilo lilianza pale alipohitimu masomo ya chuo kikuu na kuanza kujiuliza afanye nini.
Aliamua kufanya utafiti kwa kuangalia wale waliofanikiwa sana kwenye kazi au biashara walizofanya na kulinganisha na ushauri wa fanya unachopenda.

Majibu aliyopata kwenye utafiti wake yalimshangaza, kwani yalionesha waliofanikiwa hawakuanza na kile wanachopenda. Na pia aliona wengi walioanza na wanachopenda, hawakuweza kufanikiwa.

Hapo ndipo alipoandika kitabu alichokiita So Good They Can’t Ignore You: Why Skills Trump Passion in the Quest for Work You Love. Kwa tafsiri rahisi anaeleza jinsi mtu anaweza kuwa bora sana kwenye kile anachofanya kiasi kwamba hakuna anayeweza kumpuuza.

Kwenye kitabu hiki, Cal anatuonesha kwa tafiti na mifano kwamba mafanikio kwenye kazi au biashara siyo matokeo ya kufanya unachopenda, bali ni matokeo ya kujenga ujuzi adimu na wenye thamani ambao unakupa fursa za kufanya kazi na wengi zaidi.

Utangulizi kutoka kwenye kitabu.

Kwa kipindi kirefu, ushauri maarufu kwenye kazi umekuwa ni fuata kile unachopenda. Watu wamekuwa wanashauriwa wafanye kazi wanayoipenda na watakuwa na furaha kwenye maisha.

Lakini mwandishi Cal Newport aliona kuna udhaifu mkubwa kwenye ushauri huo. Katika kuangalia maisha yake binafsi na ya wengine, aliona wapo watu wanaopenda kazi wanazofanya na wapo ambao hawazipendi.
Katika kutafiti zaidi, aligundua kinachowatofautisha watu hao siyo namna wanavyopenda wanachofanya, bali namna walivyobobea kwenye kile wanachofanya.

Alichoona ni kwamba mtu akiwa na ubobezi kwenye kile anachofanya, akiweza kukifanya kwa ubora wa hali ya juu na upekee kabisa, anafanya kazi  nzuri, anapata fursa nzuri na anayafurahia maisha yake pamoja na kuipenda kazi yake.

Kwenye kitabu hiki Cal anavunja ushauri huo maarufu wa fanya unachopenda na badala yake anashauri uwe bora sana kwenye chochote unachofanya.

Sheria nne za kufuata ili kufanikiwa kwenye kazi au biashara unayofanya.

Kwenye kitabu hiki, Cal ameshirikisha sheria nne za kufuata kwenye kuchagua kile unachofanya, kukibobea na kupata fursa nzuri zaidi kwenye kitu hicho.

Sheria ya kwanza ni kuepuka kama ukoma ushauri wa kufanya unachopenda. Cal anaita hii ni nadharia ya shauku.
Anaonesha jinsi nadharia hii ilivyo hatari kwa sababu siyo wote wanaoweza kujua wanachopenda na siyo vyote mtu anapenda vinaweza kuwa kazi au biashara nzuri kwake.
Kwa kuijua sheria hii, utaweza kuona kwa nini wengi hawafanikiwi kwenye kile wanachofanya.

Sheria ya pili ni kujijengea mtaji wa ujuzi, kwa kuwa na ujuzi ambao ni adimu na wenye thamani kubwa.
Hapa ndipo Cal anatuonesha jinsi tunavyoweza kuwa bora sana kiasi kwamba hakuna anayeweza kutupuuza. Hii ni dhana ambayo Cal anaiita mtaji wa ujuzi ambao ukishakuwa nao, fursa zinakuwa nyingi kwako.
Kwa kuijua sheria hii utaweza kuona kwa nini huwa kuna watu wanapata kazi nyingi wakati wengine hawana kazi kabisa.

Sheria ya tatu ni kukataa kupandishwa cheo. Hapa unaweza kuona sheria hii inapingana na lengo la kufanikiwa kwenye kile unachofanya. Kwamba kama lengo ni kufanikiwa na umeshajijengea ujuzi ambao wengine wanauona na kuukubali na kuamua kukupa vyeo zaidi, kwa nini ukatae?
Kwenye sheria hii Cal anatuonesha jinsi mafanikio kwenye kazi au biashara yanategemea kiwango cha uhuru ulionao kwenye kile unachofanya.
Anatuonesha pia kwamba jinsi tunavyojijengea mtaji wa ujuzi, ndivyo wale wanaonufaika na tunachofanya wanavyotaka kutudhibiti zaidi.
Kwenye sheria hii Cal anatuonyesha vikwazo vya kuvuka ili kuepuka kupoteza uhuru.

Sheria ya nne ni kuhusu maono. Kwenye ushauri ambao wengi wanapokea wamekuwa wanashawishiwa kuanza na maono na kisha kuyapambania. Hapa pia Cal anaenda kinyume, kupitia tafiti na mifano ya waliofanikiwa, anaonyesha jinsi ilivyo muhimu kuanza kujijengea mtaji wa ujuzi kabla hujajiwekea maono utakayofanyia kazi.
Kwenye sheria hii utajifunza jinsi ya kujiwekea maono sahihi baada ya kuwa na mtaji wa ujuzi.

Karibu sana rafiki usome uchambuzi kamili wa kitabu SO GOOD THEY CAN’T IGNORE YOU ili uweze kujifunza misingi ya kuwa bora kabisa kwenye chochote unachofanya kiasi kwamba watu wanakung’ang’ania ufanye nao kazi kitu ambacho kitakupa fursa nzuri, uhuru na kuweza kuyafurahia maisha yako.

Uchambuzi kamili wa kitabu hiki unapatikana kwenye channel ya SOMA VITABU TANZANIA, jiunge kwa kufungua www.t.me/somavitabutanzania kisha bonyeza Join Channel.

Karibu kwenye mjadala wa vitabu.
Rafiki yangu ambaye ni mpenzi wa kusoma vitabu, nakukaribisha kwenye kipengele kipya cha mjadala wa vitabu ambacho kitakuwa kinaruka hewani mubashara mara moja kila wiki.

Kipindi kinaitwa KUTOKA VITABUNI na kila wiki tutajadiliana moja kwa moja kwa sauti kitabu kimoja ambacho kimechambuliwa kwenye channel ya SOMA VITABU TANZANIA.
Ili uweze kushiriki mijadala hii unapaswa kuwa mwanachama wa channel ya Telegram ya SOMA VITABU TANZANIA na uwe kwenye telegram. Kuwa mwanachama fungua www.t.me/somavitabutanzania kisha jiunge.

Kipindi cha kwanza cha KUTOKA VITABUNI kitakuwa leo siku ya jumatano, tarehe 30/06/2021 kuanzia saa mbili kamili usiku saa za Afrika Mashariki. Kuwa hewani muda huo ili uweze kushiriki mjadala moja kwa moja.
Pia hakikisha umesoma uchambuzi wa kitabu cha SO GOOD THEY CAN’T IGNORE YOU ili uwe na mambo ya kuchangia wakati wa mjadala.
Karibu sana tujadiliane yale yaliyo kwenye vitabu, tujifunze na kuweza kuchukua hatua sahihi ili tupige hatua kwenye maisha yetu.

Rafiki yako anayekupenda sana,
Kocha Dr Makirita Amani.