2380; Usiangalie walipo sasa, angalia walipotoka…

Nimekuwa nasema na ninaendelea kusema kwamba ushauri mwingi unaotolewa na watu waliofanikiwa siyo ushauri sahihi kwa wale ambao bado hawajafanikiwa.

Na sababu kubwa ni mbili.
Moja ni vingi walivyofanya, siyo ambavyo jamii inaweza kuelewa, hivyo wakivieleza wataonekana ni watu wa ajabu. Hata kama siyo kinyume na sheria, lakini vinakuwa ni vitu ambavyo jamii haiwezi kuamini. Na kwa kuwa hawataki utata basi hawavisemi.
Mbili ni wakati mwingine hawajui kipi katika vingi walivyofanya kimepelekea wafanikiwa. Au wanakutana na bahati fulani ambazo hawazioni wazi.

Watu hawa hawadanganyi kwa kukusudia, bali wanadanganya bila ya kujua wanafanya hivyo.
Njia pekee ya kujifunza kwa waliofanikiwa ni kuangalia yale waliyofanya kabla hawajafanikiwa na siyo wanayofanya au kusema sasa.

Huwa kuna kauli kwamba historia huandikwa na washindi, hivyo tunachojifunza kwenye hadithi za mafanikio ni ushindi wa wachache.
Wapo wengi waliofanya kama wao na wakashindwa pia.

Somo kubwa ni kwamba, kujua ukweli kwenye mafanikio siyo rahisi kama wengi wanavyodhani.
Ingekua hadithi za mafanikio pekee zinatosha kuwasaidia watu kufanikiwa, kizazi cha sasa kingekuwa na mafanikio makubwa.
Maana hakuna asiyejua hadithi ya mafanikio ya mtu aliyetoka chini na kupambana mpaka juu.

Lakini pamoja na wingi wa hadithi za mafanikio, bado wengi hawafanikiwi kwa sababu hawajui jinsi ya kuchimba ukweli kutoka kwenye hadithi hizo.

Kwa kila hadithi ya mafanikio unayokutana nayo, usifurahie tu kusikia mtu alitoka hapa akafika pale, kazana kujua aliyofanya kabla hajafanikiwa. Mtazamo wa tofauti aliokuwa nao. Namna alifanya mambo yake. Jinsi alivyokabiliana na yote yaliyomjia.

Kwa kuzichunguza kweli hadithi za mafanikio, siyo kwa lengo la kuzikosoa, bali kwa lengo la kujifunza kwa kina, utaondoka na ya msingi ya kwenda kufanyia kazi.

Usiwe kama wengi wanaofurahia hadithi za mafanikio lakini wanaendelea kubaki walipo. Wewe ondoka na hatua za mabadiliko kwa kila hadithi ya mafanikio unayoipata, kwa kujua ukweli wa kina.

Kocha.