Rafiki yangu mpendwa,
Ulipokuwa mtoto, watu walipenda kukuuliza swali hili muhimu; ukiwa mkubwa unataka kuwa nani?

Na wewe ulijibu swali hilo bila ya kuona aibu au kujiwekea ukomo, ulisema chochote ulichokuwa unafikiria.

Kwa kuwa ulikuwa mtoto, watu walikubaliana na wewe, wakijua ni akili za kitoto tu, ukikua na kuujua uhalisia, utafikiri vyema.

Kadiri ulivyokua na kuendelea kuulizwa swali hilo, majibu yako yalianza kubadilika. Uliacha kusema ndoto kubwa na kusema zile zinazowezekana.
Uliacha kusema kwa kujiamini na kuanza kusema kwa kubahatisha.

Ukiwa darasa la nne ukiulizwa swali hilo unajibu kwa kujiamini nataka kuwa rubani.
Ukiwa form four ukiulizwa swali hilo unajibu nikipata hata ualimu nitashukuru.

Katika hatua hizo mbili, jamii inakuwa imefanya kazi yake kwa usahihi. Kazi ya kuua kabisa ndoto zako kubwa na kukuacha na ndoto za kawaida tu ambazo haziwezi kukupa mafanikio makubwa.

Jamii inafanya hivyo bila ya kujua, kwa sababu imejawa na watu wa kawaida, wenye ndoto za kawaida.

Leo nina habari njema sana kwako,
Leo nakwenda kukuonyesha jinsi ndoto kubwa ambazo umewahi kuwa nazo unaweza kuzifikia kwa uhakika.

Na hilo linaanza na falsafa moja rahisi na ya uhakika, falsafa ya KILA KITU KINAWEZEKANA.

Marie Forleo alipitia maisha yenye changamoto za kila aina, alifanya kila aina ya kibarua kwenye maisha yake na fedha zilikuwa changamoto kubwa kwake.
Alizama kwenye madeni makubwa na kuwa kwenye mahusiano yenye changamoto nyingi.
Lakini aliweza kutoka kwenye yote hayo na kufika kwenye mafanikio makubwa sana.
Aliyaweza yote hayo kupitia falsafa yake aliyoiita EVERYTHING IS FIGUREOUTABLE ambayo inamaanisha KILA KITU KINAWEZEKANA.

Baada ya Marie kunufaika sana na Falsafa hiyo, hajataka kuwa mchoyo nayo, bali amekuwa mkatimu na kuwa tayari kutushirikisha wote falsafa hiyo na jinsi ya kuitumia ili kufanya makubwa.
Amefanya hivyo kupitia kitabu alichoandika, kinachoitwa Everything is figureoutable

Napenda kuchukua nafasi hii kukukaribisha kwenye uchambuzi wa kitabu hiki, ili uweze kujifunza falsafa hiyo na kuitumia kufanya makubwa kwenye maisha yako.

Kupitia kitabu hiki Marie anatuonyesha jinsi kila kitu kinavyowezekana. Anatupa mbinu na hatua za kuchukua ili tuweze kufanya tunachotaka kufanya na kupata tunachotaka kupata.

KILA KITU KINAWEZEKANA.
Familia, shule, jamii na dunia kwa ujumla imekuwa inakuaminisha kwamba kuna vitu unaweza na vingine huwezi.
Huo wote ni uongo, kila kitu kinawezekana kama mtu unakitaka kweli na upo tayari kuchukua hatua sahihi ili kukipata.
Ukweli ni kwamba, hakuna anayejua uwezo mkubwa ulio ndani yetu. Hata wazazi waliotuzaa, bado hawajui uwezo mkubwa tulionao na makubwa tunayoweza kufanya.
Hivyo walitulea kwa kubahatisha, kwa namna walivyoweza.

Sasa umeshakuwa mtu mzima, ni wakati wa kuondoa kila ukomo ambao umeaminishwa na kuupokea kama ukweli.
Ni wakati wa kujua nini hasa unachotaka na kupambana mpaka kukipata.
Kupitia kitabu hiki, tunakwenda kujifunza jinsi ya kufanikisha hilo.
Uzuri ni kwamba tuna ushahidi wa kila aina wa watu ambao waliweza kufanya makubwa ambayo yalionekana hayawezekani.
Wapo walioweza kuanzisha biashara na kuzikuza licha ya kuanza bila ya kitu kabisa.
Wapo walioweza kuondoka kwenye afya mbovu.
Wapo walioweza kuondoka kwenye madeni makubwa na kufika kwenye utajiri.
Nini kinachokusumbua sana kwenye maisha yako? Majibu ya jinsi ya kutatua hilo unayapata kwenye kitabu hiki cha EVERYTHING IS FIGUREOUTABLE.

Dunia inakutegemea sana.
Unahitaji kufanya makubwa siyo tu kwa sababu yako, bali pia kwa sababu ya dunia.
Dunia inapitia changamoto mbalimbali ambazo zinahitaji watu wenye ujasiri kuweza kuzikabili.
Dunia inahitaji kuona mfano wa watu wanaoweza kufanya yale yanayoonekana kwamba yameshindikana.
Na wewe unaweza kuwa mmoja wa watu hao, ambaye utafanya makubwa yatakayokunufaisha na kuinufaisha dunia pia.
Karibu ujifunze jinsi unavyoweza kufanya makubwa kupitia kitabu hiki cha EVERYTHING IS FIGUREOUTABLE.

Uchambuzi kamili wa kitabu hiki unapatikana kwenye channel ya SOMA VITABU TANZANIA.
Karibu ujiunge na channel hiyo leo ili upate kitabu hiki pamoja na uchambuzi wake wa kina. Kujiunga na channel ya SOMA VITABU TANZANIA, fungua www.t.me/somavitabutanzania

Mjadala wa kitabu; EVERYTHING IS FIGUREOUTABLE.

Siju ya jumapili ya tarehe 01/08/2021 tutakuwa na mjadala wa moja kwa moja (live) wa kitabu hiki ambapo kila mmoja anapata nafasi ya kushirikisha aliyojifunza na hatua anazokwenda kuchukua.

Mjadala huo utafanyika kwa njia ya telegram kwenye channel ya SOMA VITABU TANZANIA.
Kushiriki mjadala huu hakikisha umejiunga na channel hiyo kwa kutumia kiungo www.t.me/somavitabutanzania
Karibu sana kwenye mjadala.

Rafiki, nikukaribishe ujiunge na channel ya SOMA VITABU TANZANIA, usome kutabu na uchambuzi wake na pia ushiriki mjadala wa moja kwa moja. Kupitia haya utajifunza mengi na hatua za kuchukua ili uweze kufanikiwa.

Rafiki yako anayekupenda sana,
Muuza Matumaini Kocha Dr Makirita Amani
www.somavitabu.co.tz