Rafiki yangu mpendwa,
Kila mtu anapenda kupata mafanikio makubwa kwenye maisha.
Lakini cha kushangaza, ni asilimia ndogo sana ya watu ndiyo wanaofanikiwa.

Hiyo haijalishi mazingira, elimu, utaifa au rangi.
Kwenye jamii yoyote ile, asilimia 10 ndiyo wenye mafanikio huku asilimia 90 wakiwa hawajafanikiwa.
Na zaidi, asilimia 1 wana mafanikio makubwa kuliko asilimia 99 iliyobaki.

Je nini kinatengeneza hali hiyo?
Kuna njama zinazofanywa ili kuwazuia wengi wasifanikiwe na wachache tu ndiyo wafanikiwe?

Ukiiangalia na kuisikiliza jamii, unaweza kuona kama kuna njama zinazoendelea.
Lakini unapokwenda kuyaangalia maisha ya waliofanikiwa na wanaoshindwa, mambo yanakuwa hadharani.

Kuna mengi sana yanayowatofautisha wanaofanikiwa na wanaoshindwa.
Lakini kuna moja kuu ambalo ndiyo lenye nguvu zaidi.
Yaani kwa hilo moja, litaamua kama utafanikia au utashindwa.

Kabla hatujaona hilo kuu linaloamua mafanikio, hebu jipe mfano halisi, labda wako mwenyewe au wa watu unaowafahamu.

Huenda ukishasikia kilimo cha matunda fulani kinalipa (tikiti, nyanya n.k), ukaenda kulima na kupata hasara, ukaona umefanganywa.

Ukasikia ufugaji wa aina fulani ndiyo habari ya mjini (kuku, bata, sungura, kware n.k), ukaingia kufuga, ukakutana na changamoto, mifugo kufa na soko kutokuwa vizuri, ukaacha.

Ukasikia biashara ya pesa za mtandaoni (forex, bitcoin n.k) inalipa sana, ukaingia kufanya, ukaliwa hela zako zote. Ukaona umetapeliwa.

Ukaendelea hivyo na kila fursa mpya unayoisikia inakuvutia na unaona hiyo ndiyo mwisho wa shida zako zote.
Lakini unapoingia, mambo yanakuwa tofauti na ulivyotegemea na unaishia kuanguka vibaya.

Rafiki, siyo kwamba fursa nilizotaja hapo juu hazifai au haziwezi kukufikisha kwenye mafanikio.
Nimekuwa nakuambia kwenye kila fursa unayoisikia, ina uwezo wa kukufikisha kwenye mafanikio makubwa.

Lakini tu na ni rudie, LAKINI TU kama utakuwa na kitu kimoja muhimu; UNG’ANG’ANIZI.
Ung’ang’anizi ndiyo mhimili mkubwa kwako kupata mafanikio yoyote unayotaka.
Kama huna ung’ang’anizi, ninaweza kukuhakikishia bila ya shaka yoyote kwamba hutaweza kufanikiwa.

Kila fursa unayoisikia, hutaingia tu na kuanza kuchuma faida mara moja.
Lazima upite kwenye moto mkali kwanza, lazima ukutane na magumu sana kabla hujapata neema.

Asili huwa ina utajiri wa kutosha, lakini huwa inagawa utajiri wake kwa kumpima kwanza mtu kama amejitoa kweli kuupata utajiri huo. Na kama akiupata ataweza kuutunza vizuri.

Ndiyo maana biashara yoyote utakayoingia utakaribishwa na hasara.
Na kilimo au ufugaji wowote utakaoingia kwa mara ya kwanza utapoteza sana.

Hilo ni darasa na mtihani, ambao lengo lake ni kuchuja wale wenye mioyo myepesi, wale wanaotamani tu mafanikio na hawajajitoa kweli kuyapata.

Ukiweza kuvuka madarasa na mitihani hiyo, ambayo kwa kweli ni mingi, basi dunia itakuzawadia mafanikio ya kila aina.
Watu watasema una bahati au njama fulani zinazokuwezesha kufanikiwa kuliko wao, lakini kwa uhalisia huna tofauti kubwa na wao, ulichonacho ni ung’ang’anizi.

Nimekuwa nasema kila aliyefanikiwa kuna bahati fulani aliyokutana nayo kwenye safari yake ya mafanikio.
Hakuna hata mmoja anayeweza kusema mafanikio yake yametokana na yeye mwenyewe kwa asilimia 100.

Lakini bahati zinaenda kwa wale wanaodumu kwenye kitu kwa muda mrefu, kwa maneno mengine wale wenye ung’ang’anizi.

Je wewe upo tayari kung’ang’ana kwenye kile unachokitaka kwa muda gani bila kukata tamaa?
Muda wa chini kabisa ni angalau miaka 10.
Hii ya kila mwaka kuanza na kitu kipya haiwezi kuwa na manufaa kwako, zaidi tu ya kujifurahisha.

Mafanikio ya kweli ni matokeo ya kung’ang’ana kwenye kitu kwa muda mrefu.
Kujitoa kweli na kuiambia dunia nitapata ninachotaka au nitakufa nikiwa nakipambania.

Dunia huwa ina tabia ya kula njama ya kuwapa watu kile wanachotaka kama watakataa kupokea kingine cha tofauti.
Je wewe ni mmoja wa watu hao?

Kwa kumalizia tu, hili la ung’ang’anizi siyo mimi niliyeligundua, limekuwepo tangu enzi na enzi.
Aliyekuwa raisi wa Marekani Calvin Coolidge aliwahi kunukuliwa akisema; Hakuna chochote duniani kinachoweza kuchukua nafasi ya ung’ang’anizi. Kipaji hakiwezi, dunia imejaa wengi wenye vipaji ila hawajafanikiwa. Akili haiwezi, wapo wengi wenye akili sana ila hawana mafanikio. Elimu haiwezi, dunia imejaa wasomi wengi wasio na mafanikio. Ni ung’ang’anizi na maamuzi pekee vilivyo muhimu kwenye mafanikio. Kauli mbiu ya Endelea na mapambano imetatua na itaendelea kutatua matatizo mengi ya wanafamu.”

Sina cha kuongeza zaidi hapo rafiki yangu, labda nijumuishe maneno matatu; MAAMUZI, UNG’ANG’ANIZI, ENDELEA.
Amua nini hasa unataka.
Ng’ang’ana mpaka kukipata.
Endelea na mapambano.

Rafiki yako anayekupenda sana,
Muuza Matumaini Kocha Dr Makirita Amani
www.somavitabu.co.tz