2437; Unahangaika na watu wasio sahihi…
Watu ndiyo kazi yetu kubwa kwenye maisha.
Tunahitaji kushirikiana na watu mbalimbali kwenye safari yetu ya mafanikio.
Watu hawafanani, wana sifa na tabia mbalimbali.
Wapo ambao tunaweza kwenda nao vizuri na wakawa na manufaa makubwa kwetu.
Lakini pia wapo ambao tunapokuwa nao tunasumbuana sana na hivyo kuwa kikwazo kwetu kupata kile tunachotaka.
Unapojikuta kwenye watu ambao mnasumbuana, unaweza kuona unapaswa kuwabadili na kuwadhibiti.
Unahangaika sana na hilo, lakini bado hupati matokeo ambayo unayataka.
Inapokuja kwenye watu wa kushirikiana nao kwa namna mbalimbali, unaweza kupata watu ambao ni sahihi na ushirikiano ukawa mzuri.
Au unaweza kupata watu ambao siyo sahihi na ushirikiano ukawa siyo mzuri.
Wajibu wako kwenye maisha ni kutafuta watu ambao ni sahihi kwako kushirikiana nao.
Na siyo kuhangaika kubadili au kudhibiti watu wasiokuwa sahihi.
Watu huwa hawapendi kubadilishwa au kudhibitiwa.
Hata kama utatumia nguvu na mamlaka yako kutaka kufanya hivyo, watatafuta tu namna ya kukusumbua, ili kuonyesha nao wana maamuzi yako.
Muda wako na nguvu zako ni rasilimali zenye uhaba mkubwa na unazozihitaji sana ili kufanikiwa.
Usipoteze rasilimali hizo kwa mambo yasiyokuwa na manufaa, kama kudhibiti au kubadili watu.
Badala yake chagua kuanza na watu ambao ni sahihi, watu ambao huhitaji kuwadhibiti au kuwabadili ndiyo muweze kushirikiana vizuri.
Na kama unajiambia watu sahihi hawapatikani, jua unajidanganya au una uvivu au umekosa uvumilivu katika hilo.
Yaani unataka kuniambia kwenye watu zaidi ya bilioni 7 duniani ukose wachache ambao ni sahihi kwako?
Unapokutana na watu ambao siyo sahihi, usikasirike wala kukata tamaa na kuona watu sahihi hawapatikani. Badala yake jua bado una kazi ya kuendelea kutafuta.
Na wakati unatafuta watu sahihi, hakikisha wewe mwenyewe ni mtu sahihi pia.
Kama wewe mwenyewe hujawa mtu sahihi, huwezi kupata ambao ni sahihi wa kushirikiana nao.
Hatua ya kuchukua;
Pitia mahusiano na mashirikiano yote uliyonayo na angalia yale ambayo yamekuwa na usumbufu mkubwa.
Angalia sifa za yale yenye usumbufu na linganisha na sifa za yale ambayo ni bora.
Tengeneza vigezo vya sifa na tabia utakazokuwa unaangalia kwa watu kabla ya kushirikiana nao au kuhusiana nao.
Hilo litakusaidia kupunguza watu wasiokuwa sahihi na kuongeza wale ambao ni sahihi.
Neno la kutafakari;
Kama inabidi umbadili au kumdhibiti mtu ndiyo uweze kushirikiana naye, jua huyo siyo mtu sahihi kwako, mtasimbuana sana. Anza na watu sahihi ambao hawahitaji kubadilishwa au kudhibitiwa na mtashirikiana vyema.
Kocha.
Asante Sana kocha, Kama inabidi nihangaike kumbadili mtu ili niweze kushirikiana naye huyo siyo mtu sahihi kwangu. Pamoja Sana kocha.
LikeLike
Karibu.
LikeLike