2438; Pata Pesa Kwanza…
Huwa kuna picha huwa inazunguka mtandaoni, ikimnukuu Warren Buffett akisema; pesa siyo kila kitu, ila hakikisha unazo za kutosha kabla hujaongea huo ujinga.
Nina hakika Buffett hajawahi kusema maneno ya aina hiyo, ila ujumbe huo umekuwa maarufu kwa sababu umebeba ujumbe mkubwa na muhimu sana kuhusu fedha.
Ni rahisi kuzungumza kuhusu fedha kuliko kuzipata.
Ni rahisi kuwakosoa wenye fedha hata kama huna fedha.
Na ni rahisi kujihalalishia kukosa kwako fedha kwa maneno mbalimbali ya kujifariji.
Lakini yote hayo hayana msaada kama huna fedha.
Pata pesa kwanza kabla hujasema mengi kuhusu fedha.
Maana chochote uchosema kuhusu fedha kabla hujawa nazo ni kujidanganya na kujifariji tu.
Ni wasio na fedha ndiyo huwa wanasema mambo mabaya kuhusu fedha.
Wasio na fedha ndiyo hujifariji kwa nini hawana.
Wasio na fedha ndiyo walio tayari kuwasema vibaya wale walionazo.
Ukikutana na mtu anasema fedha siyo kila kitu au fedha hainunui furaha, jua kabisa kwamba mtu huyo hana fedha.
Kwa sababu hizo ni kauli tupu, ambazo hazijabeba maana yoyote.
Kwamba fedha siyo kila kitu, kwa hiyo? Hebu nenda na hiyo kauli kwenye mgahawa ukiwa na njaa sana halafu uone itakua rahisi kiasi gani kupata chakula kaman huna fedha.
Kwamba fedha hainunui furaha, wapi uliambiwa unatafuta fedha ili uweze kununua furaha? Maana hapo ndipo upotoshaji unapoanzia.
Kwa nini watu wachague kulinganisha fedha na furaha na siyo vitu vingine?
Tuachane na hayo maswali na kauli nyingine za kujifariji pale unapokuwa huna fedha.
La msingi kabisa ni hili, pata pesa kwanza kabla hujahangaika na wewe kutoa maoni yako kuhusu fedha.
Pambana kuzipata pesa, kwa njia halali kabisa na kuzifanya zikupatie pesa zaidi na ninakuhakikishia hutapata muda wa kuanza kuwa na maoni yasiyo sahihi kuhusu fedha.
Dalili za kwamba huna fedha na unapoteza muda wako ni kuwa na maoni hasi kuhusu fedha, kuwachukia wenye fedha na kuamini una ushauri mzuri kwa wenye fedha kuliko wanavyozitumia.
Kama una ushauri mzuri sana kuhush fedha kuliko wale waliokuzidi fedha, mbona hujautumia na wewe ukapata fedha kama wao?
Ujumbe ni huu rafiki, pata pesa kwanza, mengine yote ni kelele na kujilisha upepo kama huna pesa.
Na hilo ndiyo swali muhimu la kujiuliza kila mara kabla hujatoa maoni yako kuhusu fedha au kuwakosoa wengine kuhusu fedha. Je tayari nina fedha za kutosha? Kama jibu ni hapana, okoa muda wako kwa kwenda kuzisaka fedha na siyo kuongea ujinga kuhusu fedha.
Hatua ya kuchukua leo;
Leo jitathmini kila fikra unazokuwa nazo kuhusu fedha na kauli unazotoa kuhusu fedha. Jitathmini huwa unafikiria na kusema nini pale unapowaona watu wenye fedha kuliko wewe.
Amua leo kuachana na fikra na maoni yote yasiyo sahihi kuhusu fedha na weka kipaumbele chako kwenye kupata pesa zaidi na kizifanya zikuzalishie zaidi na zaidi.
Nini unaweza kufanya leo ambacho kitakuongezea fedha zaidi? Jipe jibu na fanya kitu hicho.
Ujumbe wa kutafakari;
Ni kweli kwamba fedha haiwezi kununua furaha, lakini pia kutokuwa na fedha hakununui furaha yoyote. Ni bora kulia ukiwa kwenye gari kuliko kulia ukiwa kwenye baiskeli.
Kocha.
Asante kwa ujumbe yakinifu kocha
LikeLike
Karibu.
LikeLike