2440; Shabiki wako namba moja…

Wewe ndiye unayepaswa kuwa shabiki wa kwanza kwako mwenyewe.

Unapaswa kujikubali sana na kujishabikia kwenye yale makubwa ambayo unayafanya.

Usiwe shabiki wa wengine au wa michezo mbalimbali kabla hujawa shabiki wako mwenyewe.

Usifurahie ushindi wa wengine unaowashabikia na kuona kama ni ushindi wako wakati wewe binafsi hakuna ushindi unaopata kwenye maisha yako.

Nguvu zote ambazo umekuwa unazitumia kushabikia mambo mbalimbali, zipeleke kwenye kujishabikia wewe mwenyewe.

Ushabiki una nguvu sana, ukiutumia vizuri utaweza kufanya makubwa sana.

Ushabiki unateka hisia na kukuwezesha kuweka juhudi kubwa na kupata matokeo makubwa pia.

Hakuna anayechoka kushabikia, hivyo unapokuwa shabiki namba moja kwako, huchoki.

Kuwa shabiki wa kwanza kwako ili uweze kufanya makubwa kwenye maisha yako.
Kwa sababu ndani yako kuna uwezo mkubwa mno kuliko unavyoutumia sasa.

Huuoni wala kuufikia uwezo huo kwa sababu juhudi zako umepeleka kwenye kushabikia mambo na watu wengine.
Kuwa shabiki wako mwenyewe na utaona mengi zaidi unayoweza kufanya.

Hatua ya kuchukua;
Yatafakari maisha yako na angalia ni ushabiki gani mkubwa ambao umekuwa nao. Angalia ni vitu au watu gani unaowashabikia kweli, ambapo upo tayari kuacha chochote ili kushabikia.
Chagua sasa kuhamishia nguvu hiyo ya ushabiki kwako mwenyewe. Kuwa shabiki namba moja kwako mwenyewe, jiamini, jikubali na jisukume ili uweze kufanya makubwa zaidi.

Tafakari;
Unakubalije kuwa shabiki mkubwa wa michezo au watu wengine wakati siyo shabiki wako mwenyewe? Anza kwa kujishabikia wewe mwenyewe ili uweze kufanya makubwa kwenye maisha yako.

Kocha.