2442; Barabara lazima zifagiliwe.

Pata picha kama hakungekuwa na watu wanaofanya usafi kwenye barabara tunazotumia.

Au hakuna watu wanaoondoa takataka kwenye mazingira yetu.

Au hakuna watu wanaolima chakula tunachohitaji sana.

Kwa hakika maisha yangekuwa magumu, bila ya kujali mtu una fedha kiasi gani.

Ninachotaka kusema hapa ni hiki, kila kazi ambayo watu wanafanya ina umuhimu mkubwa.
Na pia ina uwezo wa kumfikisha mtu kwenye mafanikio makubwa.

Asije mtu akakuambia huwezi kufanikiwa kwenye kitu fulani, mpaka kwenye kitu fulani pekee.

Watu wamekuwa wakihangaishwa sana kukimbizana na kila aina ya fursa mpya inayojitokeza, kwa kuona hiyo ndiyo yenye uhakika wa mafanikio.

Uhakika wa mafanikio haupo kwenye fursa ya aina fulani.
Bali upo kwenye namna unavyofanya chochote unachoamua kufanya.

Mafanikio yapo kwenye chochote unachojitoa kweli kukifanya na kukipa kipaumbele kikubwa katika kukifanya.
Mafanikio yapo kwenye kile unachofanya kwa viwango vya juu kabisa na kutoa thamani kubwa kwa wengine.

Haijalishi ni kitu gani, bali inajalisha unakifanyaje kitu hicho.

Hatua ya kuchukua;
Kwa chochote unachofanya, jiulize ni thamani ipi hasa unayoitoa kwa wengine kwenye hicho unachofanya. Kisha jiulize unawezaje kuitoa thamani hiyo kwa wingi zaidi na kwa wengi zaidi. Fanyia kazi majibu unayopata ili uweze kupata mafanikio makubwa.

Tafakari;
Kama bado unakimbizana na kila fursa mpya ukiamini mafanikio ndiyo yapo huko, jua unajipoteza na kujichelewesha. Chagua kile ambacho uko tayari kujitoa kweli kukifanya na chenye thamani kwa wengine, kisha kifanye kwa viwango vya juu kabisa.

Kocha.