2464; Unapokuwa huna pa kuanzia.

Kuna kichekesho kimoja, lakini cha kweli, ambapo kikosi cha jeshi kilikuwa kimezungukwa pande zote na maadui.

Wanajeshi wakaenda kwa mkuu wa kikosi kumpa taarifa kwamba wamezingirwa pande zote na adui, walimweleza wakiwa na hofu kubwa kwa sababu hawakujua hata wanawezaje kujiokoa.

Mkuu wa kikosi alipopata taarifa hizo akatabasamu na kuwaambia, vizuri sana, hilo linamaanisha tunaweza kushambilia upande wowote tunaotaka.
Maana hatuna tena haja ya kutafuta adui amejificha wapi, yupo kila upande.

Kuna wakati kwenye maisha yako unapitia hali ya aina hiyo, kila kitu kinakuwa hovyo kabisa kiasi kwamba hujui wapi pa kuanzia.
Ukigusa kitu kimoja kinaharibu kitu kingine na kingine na kingine.

Katika hali kama hiyo ni rahisi kukata tamaa na kuona hakuna unachoweza kufanya, huna popote pa kuanzia.

Unapojikuta kwenye hali hii, usikubali kukata tamaa, maana unaweza kuanzia popote, kufanya kilicho sahihi na kuendelea nacho mpaka matokeo yatakapokuwa mazuri.

Wakati unaanza kufanyia kazi kitu, kinaweza kuzidi kuwa hovyo kuliko kilivyokuwa awali. Mpaka unaweza kudhani unaharibu zaidi kuliko kutengeneza.

Unachopaswa kuelewa ni mambo huwa ya hovyo zaidi kabla hayajawa mazuri. Usiangalie sana ni matokeo gani unayopata, wewe angalia zaidi ni hatua zipi sahihi unazochukua.

Kama unachofanya ni sahihi, ni swala la muda tu kabla hujaanza kuona matokeo mazuri. Hivyo kuwa na uvumilivu na endelea na mchakato.

Hatua ya kuchukua;
Ni mambo gani yanayokusumbua sasa mpaka unaona huna pa kuanzia? Chagua leo kuanzia popote na fanya kilicho sahihi bila kuacha mpaka utakapopata matokeo mazuri.

Tafakari;
Hakuna sehemu nzuri kama pale unapokuwa chini kabisa, maana sehemu pekee ya kwenda ni juu. Hivyo unapojikuta uko chini, jipongeze, maana sasa uelekeo wako ni mmoja tu, kwenda juu.

Kocha.