#SheriaYaLeo (314/366); Dhibiti hisia zako za majigambo.

Majigambo ni nguvu ambayo ipo ndani ya kila mmoja wetu.
Nguvu hiyo inatusukuma kutaka kutaka vitu zaidi ya tulivyonavyo, kutambulika na wengine na kuunganika na kitu kikubwa.

Tatizo halipo kwenye nguvu yenyewe, kwani inaweza kutumika kuchochea matamanio yetu. Tatizo lipo kwenye kudhibiti nguvu hiyo.

Mara nyingi majigambo hutufanya tujione sisi ni bora kuliko wengine. Kutokana na sifa tunazopokea, tunadhani tunaweza kufanya kila kitu. Na hilo linapelekea kujikuta tunajaribu kufanya mambo mengi tofauti tofauti ili kupata sifa zaidi.
Lakini kwa kutawanya sana nguvu zetu, hatupati matokeo makubwa na hivyo tunakosa sifa tulizotegemea kupata.

Hupaswi kuzima nguvu hiyo ya majigambo iliyo ndani yako. Badala yake unapaswa kuidhibiti vyema, kwa kuielekeza kwenye vitu vichache ambavyo ni vikubwa na muhimu.
Chagua lengo ambalo ukiliwekea nguvu zako zote na kukifikia litakupeleka hatua kubwa zaidi.

Utaligawa lengo hilo kwenye hatua ndogo ndogo na katika kufanyia kazi hatua hizo hutaruhusu usumbufu wowote kukuingilia.
Unaweka umakini wako wote kwenye kile unachofanyia kazi, hali itakayopelekea ukifanye kwa viwango vya juu kabisa.

Mwisho wa siku kilicho muhimu siyo masaa uliyotumia kufanya kitu, bali umakini ambao umeweka kwenye kukifanya kitu hicho.
Unapoweka umakini mkubwa, hata kama ni kwa muda mfupi, unapata matokeo ambayo ni bora kabisa.

Matokeo makubwa unayopata na maendeleo binafsi unayokuwa unapata vinakidhi vizuri hisia zako za ufahari kuliko kuhangaika na mambo mengi ambayo huyakamilishi kwa tija.

Sheria ya leo; Usijiruhusu nguvu za majigambo kukuhangaika na mambo mengi kwa wakati mmoja. Peleka nguvu hizo kwenye mambo machache muhimu ambayo utayapa umakini mkubwa na kupata matokeo bora.

#NidhamuUandilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji