2809; Rahisi kufanya.
Ukichunguza kwa makini, utagundua kwamba matatizo yote ambayo umewahi kuwa nayo kwenye maisha, chanzo chake ni kukimbilia vitu rahisi kufanya.
Hii ni asili yetu binadamu, huwa hatupendi vitu vigumu.
Hivyo kila mara tunatafuta kilicho rahisi.
Na huko pia ndipo tunapotengeneza matatizo mengi tunayokuwa nayo kwenye maksha.
Hata hali ya umasikini na kutokufanikiwa, chanzo chake kikuu ni kupenda kufanya vitu rahisi.
Kwa sababu ukiangalia, waliofanikiwa na walioshindwa wote wana muda sawa na wanaweza kuwa wanafanya kitu cha aina moja.
Tofauti inatokana na hali ya kutafuta urahisi au ugumu.
Wanaoshindwa wanatafuta urahisi, kitu ambacho wengi wanakitafuta pia na hivyo kinakosa thamani.
Wanaofanikiwa wanakabiliana na ugumu, kitu ambacho wachache ndiyo wanakikubali na hivyo thamani yake kuwa kubwa.
Kupata mafanikio makubwa kwenye maisha yako, achana kabisa na urahisi. Ondokana na mkumbo wa wengi kutafuta njia za haraka na za mkato za kufanikiwa.
Wewe angalia njia sahihi ni ipi na ikabili hiyo bila ya kujali ugumu wake.
Mara zote fanya kile kilicho sahihi na siyo kilicho rahisi.
Kushindwa, kukosea, kutapeliwa na hata kuanguka mara nyingi kunasababishwa na kukimbilia vitu rahisi badala ya kuhangaika na vitu sahihi.
Rahisi huwa haina thamani, hivyo usijihangaishe nayo kama unataka mafanikio makubwa.
Hatua ya kuchukua;
Kabla hujafanya kitu chochote, jiulize kwanza kama ni rahisi au sahihi. Kwa nini unasukumwa kukifanya? Ni kwa sababu ndiyo kitu sahihi au ndiyo kitu rahisi? Mara zote, kilicho sahihi huwa siyo rahisi na kilicho rahisi huwa siyo sahihi.
Wewe unachotaka ni kufanya kilicho sahihi mara zote, maana hicho ndiyo kitakachoyajenga mafanikio yako.
Tafakari;
Kama mafanikio yangekuwa rahisi kama wengi wanavyodanganyana, kila mtu angekuwa tayari ameshafanikiwa.
Kama kungekuwa na njia rahisi na ya uhakika ya kufanikiwa, njia hiyo isingekuwa siri kabisa, maana kila mtu angeitumia.
Ukweli utabaki pale pale, kuhangaika na vitu rahisi ndiyo kikwazo namba moja cha mafanikio.
Ili kufanikiwa, usitafute vitu rahisi kufanya, badala yake tafuta vitu sahihi kufanya.
#LetsBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining
#WeAllGonnaMakeIt
#WorkHardAndYouWillSucceed