2940; Namba mbaya kwenye biashara.

Rafiki yangu mpendwa,
Ipo namba ambayo ni mbaya sana kwenye biashara na ambayo unapaswa kuiepuka kama unataka kujenga biashara yenye mafanikio makubwa.

Namba hiyo ni moja.
Kuwa na kitu chochote kimoja kwenye biashara ni hatari kubwa.
Inakuweka kwenye utegemezi mbaya na unaokuwa kikwazo kwa ukuaji.

Usiwe na mfanyakazi mmoja pekee kwenye biashara, kwani akikuambia anaacha kazi, biashara yako itaathirika sana.
Kuwa na mfanyakazi zaidi ya mmoja ili lolote linalotokea kwa mmoja lisiathiri biashara.
Tukiwa hapo kwa wafanyakazi, asiwepo mfanyakazi mmoja pekee ambaye ndiye anaweza kufanya kitu fulani. Bali kila kitu kiweze kufanywa na mfanyakazi zaidi ya mmoja. Hiyo itaondoa kukwamishwa pale mmoja anapokuwa na changamoto, kwani mwingine anaweza kufanya majukumu yake.

Usiwe na mteja mmoja pekee au anayetegemewa sana na biashara. Kwani mteja huyo akisema anaondoka, biashara inatikisika sana. Au hata akitaka mabadiliko ya bei, biashara haitakuwa na namna bali kukubali, kwa kuwa ina utegemezi mkubwa kwake.
Jenga biashara yenye wateja wengi na hata mteja awe mkubwa kiasi gani, kuondoka kwake kusiathiri sana biashara.
Hili ni muhimu kuzingatia, kwa sababu ni rahisi kujisahau kutafuta wateja wapya pale unapokuwa na mteja mmoja au wachache wakubwa wanaoleta faida kubwa.
Usipate usingizi kama biashara yako inategemea mteja mmoja.

Usiwe na njia moja tegemezi ya kufanya chochote kwenye biashara. Iwe ni masoko, mauzo, kuajiri n.k. Kama kuna njia moja pekee unayotegemea kwenye kukamilisha mambo muhimu kwenye biashara, utajikwamisha. Kwa mfano kama njia pekee ya kupata wateja ni matangazo kwenye mitandao ya kijamii, siku ikitokea shida kwenye njia hiyo unakosa kabisa wateja.

Usiwe na kifaa kimoja cha msingi kwenye biashara, ni kujiweka kwenye hali ya kukwamishwa haraka.
Kwa mfano kama biashara yako inahusisha matumizi ya kompyuta kama zana kuu, usiwe nayo moja. Kwani inapoharibika au kuwa na changamoto, itaathiri sana biashara.
Kadhalika simu, gari, mashine ya kuchapa na vifaa vingine, kama ndiyo cha msingi kabisa kwenye biashara, kiwepo zaidi ya kimoja.
Hata kama humilili vifaa hivyo, angalau uweze kupata kifaa cha kutumia pale unapokuwa na uhitaji.

Hakuna kitu ambacho huwa kinanishangaza kama mwandishi ambaye ana kompyuta moja pekee.
Na mbaya zaidi, kazi zake zote zinakuwa ndani ya kompyuta hiyo.
Ni kujiandaa kukwamishwa, maana kuna siku kompyuta hiyo itasumbua na utaweza kupoteza kila kitu.
Kwa mwandishi, hata kama huwezi kumudu kuwa na kompyuta zaidi ya moja, basi usiache kazi zako kwenye kompyuta moja. Badala yake hifadhi kazi zako zote kwenye mtandao, kiasi kwamba ukitumia hata kompyuta ya mtu mwingine utaweza kuzifikia na kuendelea kuzifanyia kazi.

Kuwa na utegemezi kwenye kitu chochote kimoja kibiashara ni kujiandaa kushindwa. Kwani kitu hicho kimoja unachokitegemea huwa kinakuangusha pale unapokuwa na uhitaji mkubwa.
Kwenye maeneo yote muhimu ya biashara yako, kuwa na kitu zaidi ya kimoja unachotumia, hata kama siyo vyote unavyomiliki wewe.
Unachopaswa kuepuka ni usikwamishwe na chochote kinachoshindwa kwenda vile kinavyopaswa kwenda.

#NidhamuUandilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe