3066; Acha kuongea.

Rafiki yangu mpendwa,
Kwenye hii safari ya mafanikio, kuna mafanikio ya aina mbili.

Moja ni mafanikio halisi ambapo ni mtu kupata kile anachotaka, haya huwa yanahitaji mtu kuweka kazi hasa na kwa kipindi cha muda mrefu.

Mbili ni mafanikio yasiyo halisi, ambapo ni mtu kuridhika na ndoto, malengo na mipango anayokuwa nayo, haya huwa yanahitaji zaidi maneno.

Mafanikio halisi ni watu wachache sana ambao huwa wanayapata, kwa sababu yanahitaji mtu kuweka kazi kubwa na kwa juhudi kwa muda mrefu.
Mtu anakutana na vikwazo vya kila namna, lakini kwa kuwa amedhamiria na kujitoa kweli, anapata matokeo bora kabisa.

Watu wengi wamenasa kwenye mafanikio yasiyo halisi.
Hawa ni watu ambao wakipata maarifa na taarifa zozote za mafanikio wanahamasika sana.
Hamasa wanayoipata inawasukuma kuweka malengo makubwa na mpango wa kuyatekeleza.
Inapofika kwenye kutekeleza yale waliyopanga, wanaanza kutekeleza, lakini wanapokutana na ugumu, huwa hawang’ang’anii kufanya kitu hicho.
Badala yake huwa wanatoroka na kwenda kwenye malengo na mipango mingine.
Kitu pekee wanachofanikiwa watu hao ni raha ya muda mfupi wanayoipata kwa kuweka malengo na mipango upya kila wakati.
Wanapanga na kuongea sana, lakini hakuna hatua zozote wanazokuwa wanapiga.

Rafiki, njia pekee ya kuachana na mafanikio yasiyo halisi ili uweze kwenda kwenye mafanikio halisi ni kuacha kuongea.
Kuongea sana ndiyo kitu pekee ambacho watu huwa wanafurahia kufanya kwa sababu kinawafanya wajisikie vizuri wakati hakuna walichofanya.
Watu wengi kwa kueleza ndoto na malengo makubwa waliyonayo wanajisikia vizuri sana.
Lakini habari inaishia hapo, hakuna hatua yoyote kubwa wanayokwenda kuchukua.

Kwenye safari ya mafanikio makubwa, maneno na matendo huwa yanapishana.
Wale wanaoongea sana huwa siyo watendaji wazuri na watendaji wazuri huwa siyo waongeaji sana.

Maneno mengi ni sawa na kujilisha upepo tu kwa kujifurahisha.
Hivyo kuacha kuongea kunapunguza kujidanganya kimafanikio.

Kwenye hii safari kubwa ya mafanikio, maneno hayana nafasi wala mchango wowote.
Kama huna mpango wa kuchukua hatua kwenye jambo, ni bora ukaacha kuliongelea, kwa sababu maneno hayana nguvu yoyote.
Na kama una mpango wa kuchukua hatua kwenye jambo, ni bora pia ukaacha kuliongelea na kuingia kulifanya, kwa sababu kuongea kunapoteza muda ambao ungetumia kufanya.

Kama huna mpango wa kufanya kitu, achana nacho na peleka juhudi zako kwenye kile unachochagua kufanya.
Na kama una mpango wa kufanya kitu, acha kuhangaika na maneno na peleka juhudi kwenye kukifanya.

Kama kuongea ingekuwa ndiyo kufanikiwa, kila mtu angekuwa na mafanikio makubwa.
Lakini mafanikio pekee yanayopatikana kwenye kuongea ni yasiyo halisi, yaani ya kujifurahisha tu, kama fedha za kuchora.
Unaweza kufurahia umeichora fedha vizuri, lakini jaribu kwenda kununua kitu na fedha uliyochora na hapo ndipo utagundua furaha yako ni ya kujifariji tu, haiendani na uhalisia ulivyo.

Fanikiwa kwenye uhalisia, kupitia kufanya na siyo kwa maneno ambayo hayaendani na uhalisia.
Acha kuongea na ufanye.
Kuna mengi utanufaika nayo kwenye kufanya kuliko kuongea pekee.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe