3067; Imani, Ujuzi, Kazi.

Rafiki yangu mpendwa,
Kuna kanuni chache sana za mafanikio.
Lakini zimekuwa zikipinduliwa pinduliwa na kuishia kuonekana kama ni nyingi na ngumu.
Hilo huwa linawakatisha tamaa wengi na kushindwa kufanikiwa.

Maneno matatu yaliyopo hapo juu, siyo mageni kuyasikia.
Na hata maana za maneno hayo unazijua vizuri kabisa.

Lakini leo nataka niyapindue pindue maneno hayo na uone jinsi yalivyo mafiga matatu muhimu ya kupata chochote unachotaka kwenye maisha yako.

IMANI.
Kupata chochote unachotaka kwenye maisha yako, kunaanza na imani kali sana na isiyoyumbishwa kwamba utapata kile unachotaka.
Hata ukiwekewa bastola kichwani na kuambiwa ukiamini kwenye kile unachotaka risasi inafyatuka na usipoamini haifyatuki, wewe umaamini bila ya shaka.
Unatakiwa ujiamini sana na uamini sana kwenye kile unachotaka kiasi cha watu kukuona umechanganyikiwa.
Na kipimo kizuri cha imani yako kwako na kwa ndoto zako ni watu kuona umechanganyikiwa.
Yaani kama hakuna watu wana wasiwasi na wewe juu ya utimamu wako wa akili, hujiamini na wala huamini kwenye ndoto zako vya kutosha.

UJUZI.
Ili upate chochote unachotaka kwenye maisha yako, kwanza lazima ujue kwa hakika nini unachotaka, kisha ujue jinsi unavyoweza kukipata.
Lazima ujue kwa hakika ni hatua zipi unazopaswa kuchukua ili upate unachotaka.
Na hapa huhitaji kuja na uvumbuzi wowote mpya.
Badala yake ni kuangalia yale waliyofanya ambao wameshapata unachotaka na wewe kuyafanya.
Mafanikio huwa yanaacha alama.
Ili kufanikiwa, angalia yale waliofanikiwa wanafanya na wewe uyafanye.
Huo ni ujuzi muhimu sana ambao usipokuwa nao utakwama sana.

KAZI.
Nidhamu kali ya kazi inahitajika sana ili mtu uweze kupata kile unachotaka.
Kufanya kazi kwa juhudi kubwa hakukwepeki kama mtu unayataka mafanikio makubwa.
Kazi ndiye rafiki wa kweli ambaye ukiambatana naye utapata mazuri.
Pamoja na umuhimu mkubwa wa kazi kwenye mafanikio, wengi bado wamekuwa wanajaribu kuikwepa.
Wengi wamedanganyika kwa njia za mkato ambazo zimewapotezea muda na fedha.

Unahitaji kufanyia kazi vitu vyote vitatu kwa pamoja ndiyo uweze kupata matokeo makubwa na bora sana.
Hayo ndiyo mafiga matatu ya kupika mafanikio, likikosekana hata moja, inaathiri sana mafanikio ambayo mtu anaweza kuyapata.

Kama mtu atakuwa na UJUZI na kuweka KAZI ila akakosa IMANI, matokeo atakayopata yanakuwa madogo ukilinganisha na ambayo angepata kama angekuwa na vyote vitatu.

Kama mtu atakuwa na IMANI na UJUZI ila akakosa NIDHAMU YA KAZI, ataonekana mwenye ahadi hewa, kwa sababu chochote anachoahidi hakikamiliki.

Kama mtu atakuwa na IMANI na NIDHAMU YA KAZI lakini akakosa UJUZI, atahangaika sana na kuchoka, lakini kila wakati atakuwa anabadili kile anachofanya. Hapa ndipo penye wale wa kubadili fursa kila wakati, ambao leo watakuja na fursa fulani, ila kesho wataachana nayo kabisa na kuwakuta wakinadi fursa nyingine ya tofauti.

Unahitaji mafiga yote matatu ili kupika mafanikio makubwa.

Safari ya ubilionea.
Kwanza lazima UAMINI bila ya shaka yoyote kwamba utakuwa bilionea.
Imani yako inapaswa kuwa kali sana kiasi cha watu kuona kama umechanganyikiwa hivi.
Yaani imani yako inapaswa kuwa kama vile umeingiwa na pepo la aina fulani.
Usipoamini, huwezi kudumu kwenye hii safari kwa muda mrefu.

Pili UJUE mchakato kamili wa kufika kwenye ubilionea. Jua kwa hakika kila unachopaswa kufanya ili uweze kufikia ubilionea.
Na kwa bahati nzuri sana, tayari mchakato kamili tunao, ambao umeeleza kila hatua za kuchukua na jinsi ya kuzichukua.
Safari yetu ya ubilionea ni kupitia kujenga BIASHARA na kufanya UWEKEZAJI.
Kwenye biashara tunajenga MFUMO, TIMU na WATEJA.
Huku kwenye uwekezaji tukifanya kwenye MASOKO YA MITAJI na MALI.
Hatua za kuchukua kwenye kila eneo zimeelezwa kwa kina kwenye vitabu BILIONEA MAFUNZONI na CHUO CHA MAUZO.

Tatu lazima uweke KAZI kwa nidhamu ya hali ya juu sana.
Kazi inayohitajika kwenye hii safari ni nje kabisa ya mazoea.
Masaa ya kufanya kazi kwa siku ni mengi (angalau 16) na siku za kufanya kazi kwa wiki ni nyingi (6 mpaka 7) huku wiki za kazi kwa mwaka zikiwa zisizopungua 50 kati ya wiki 52 za mwaka.
Kwenye miaka sasa, siyo chini ya miaka 10.
Kama kwa kusoma hizo namba kwenye ufanyaji kazi unaona ni kitu kigumu, upo sahihi, siyo rahisi, hivyo lazima ujitoe sana.
Ingekuwa rahisi kila mtu angekuwa ameshaupata ubilionea na ungekosa thamani.

Mafiga matatu; IMANI, UJUZI, KAZI, jijengee yote kwa uhakika ili uweze kupika chakula kitamu ambacho ni mafanikio unayoyataka kwenye maisha yako.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe