Rafiki yangu mpendwa,
Tunaishi kwenye zama ambazo mabadiliko makubwa yanatokea kwa kasi.

Mabadiliko hayo yamewaacha nyuma watu wengi ambao hawakuwa tayari kuendana nao.

Lakini pia mabadiliko hayo yamewapoteza wengi, ambao walidhani misingi mbalimbali ya maisha imebadilika.

Yapo maandiko yanayosema hakuna kitu kipya chini ya jua.
Kwamba yote tunayoyaona mapya ni maboresho tu ya vitu ambavyo tayari vipo.

Na kauli hiyo ina ukweli mkubwa ndani yake, hasa inapokuja kwenye misingi muhimu ya maisha.

Dunia inaendeshwa na kanuni za asili ambazo hakuna mabadiliko yoyote yameweza kuziathiri.

Na maisha yetu pia yanaathiriwa na kanuni hizo za asili ambazo hazibadiliki.

Inapokuja kwenye fedha, biashara na uwekezaji, watu wamedanganyika sana na mabadiliko yanayoendelea na kudhani misingi mikuu nayo imebadilika.



Leo tunakwenda kukumbushana misingi muhimu ambayo kamwe haitakuja kubadilika kwenye maeneo hayo matatu.

Fedha; kipimo cha thamani.

Fedha ndiyo kipimo kikuu cha thamani kwenye maisha.
Kiasi cha fedha unacholipwa, kinaendana na thamani unayotoa kwa wengine.
Kama unataka kuongeza kipato chako, unatakiwa kuanza kwa kuongeza thamani yako.
Na mtu anapokuja kwako akikuambia ana fursa ya kupata fedha kwa haraka bila ya kufanya kazi, muulize ni thamani gani unatakiwa kutoa?
Kama hataweza kukujibu kwa uwazi, kimbia, unataka kutapeliwa.
Kwa sehemu kubwa, thamani ya fedha inapimwa kwa kazi ambayo mtu anapaswa kuweka. Hivyo hakuna njia ya mkato ya kupata fedha bila kutoa thamani.

Biashara; uzalishaji wa thamani.

Biashara ni mabadilishano ya thamani kwa fedha. Unafanya biashara pale unapowapa watu thamani ambayo wanaridhika kuilipia.
Kwenye biashara, watu wanakupa fedha pale wanapoona thamani wanayoipata ni kubwa kuliko gharama wanayolipa.
Huo ndiyo msingi mkuu wa biashara, ambao ni kuzalisha na kubadilishana thamani.
Kutokana na mabadiliko yanayoendelea, watu wamejaribu kuja na njia za mkato za kulipwa bila kuzalisha thamani na matokeo yake yameishia kuwa anguko kubwa.
Haijalishi dunia itabadilika kiasi gani, bado watu hawatakuwa tayari kukupa fedha kama hakuna thamani unayowapa.
Wape watu thamani na watakuwa tayari kukupa fedha.

Uwekezaji; ukuzaji wa thamani.

Tuna masaa 24 tu kwenye siku zetu.
Na tuna miaka michache sana hapa duniani.
Kama tutategemea kufanya kila kitu kwa muda na nguvu zetu wenyewe, tutakwama.
Tunahitaji kuwa na njia ya kuweza kukuza zaidi thamani tuliyonayo bila ya sisi kuhusika moja kwa moja.
Uwekezaji ndiyo njia kuu ya kukuza thamani bila ya kukutegemea wewe moja kwa moja.
Ni njia ya kuifanya fedha ikufanyie kazi hata kama umelala.
Hapa kwenye uwekezaji ndipo wengi sana wameumizwa kwa kudhani mabadiliko yanayoendelea yamebadili na eneo la uwekezaji.
Watu wamedanganywa kuna uwekezaji wa haraka ambao unakua kwa kasi kubwa.
Watu wanaaminishwa wanaweza kulala masikini na kuamka matajiri.
Uwekezaji wa kweli unahitaji muda kukua thamani.
Ukiambiwa kuna uwekezaji wa haraka na unaokua kwa kasi, shtuka, unataka kutapeliwa.

Rafiki, umejionea wazi hapo kwamba mabadiliko yote yanayoendelea duniani hayawezi kuathiri eneo la thamani.
Kipimo cha thamani kitaendelea kuwa fedha.
Uzalishaji wa thamani utaendelea kuwa biashara.
Na ukuzaji wa thamani utaendelea kuwa uwekezaji.
Jenga misingi yako kwenye thamani na utaweza kupata chochote unachotaka kwenye maisha yako.

Pata na usome kitabu cha ELIMU YA MSINGI YA FEDHA ambacho kitakupa mkakati wa kuongeza kipato, kudhibiti matumizi na kufanya uwekezaji ili uweze kujijengea uhuru wa kifedha.
Wasiliana na namba 0752 977 170 kupata nakala yako ya kitabu sasa.

Rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Muuza Matumaini,
Mwanafalsafa ya Ustoa,
Mkuu wa Chuo Cha Mauzo,
Kocha Dr. Makirita Amani
amakirita@gmail.com
http://www.amkamtanzania.com / http://www.t.me/amkamtanzania
http://www.utajiri.tz / http://www.t.me/utajiritz
http://www.mauzo.tz / http://www.t.me/chuochamauzo