3137; Hivi kesho jua litachomoza?

Rafiki yangu mpendwa,
Hebu fikiria kama hilo ndiyo swali ambalo ungekuwa unajiuliza kila siku kabla ya kulala, iwapo jua litachomoza au la.
Fikiria ingebidi ujiulize hivyo kwa sababu jua linakuwa halieleweki, kuna siku linachomoza na kuna siku halichomozi kabisa au linachelewa.
Unadhani maisha yako yangekuwa sawa na yalivyo sasa?
Kwa hakika majibu ni hapana.

Kuchomoza na kuzama kwa jua kila siku ni kitu ambacho tuna uhakika wa kutokea kwake.
Hivyo mipango yetu yote tunaiweka kulingana na hali hiyo.
Na tunapanga hivyo kwa kujiamini, kwa sababu tuna uhakika wa huo mwenendo wa jua.

Kadhalika vitu vingine vingi kwenye asili vinaenda kwa mfumo huo, uhakika wa kutokea kwake.
Vitu vyote ambavyo tuna uhakika wa kutokea kwake, huwa tunavitegemea kwa uhakika.
Huwa hatuwi na wasiwasi wowote kuhusu kutokea kwake, kitu kinachotupa utulivu mkubwa.

Moja ya vitu ambavyo sisi binadamu tunavipenda sana ni uhakika.
Chochote ambacho tunaweza kuwa na uhakika nacho, tunakithamini zaidi.

Hilo pia linaenda hivyo kwa watu.
Watu ambao tunaweza kuwa na uhakika nao na kuwategemea kwenye yale wanayopaswa kufanya, ni watu ambao huwa tunawathamini zaidi.

Kwenye dunia ambayo ina uhaba mkubwa wa watu ambao wanaweza kutegemewa kwa uhakika, kuwa hivyo ni faida kubwa sana kwa mtu na njia itakayompa mafanikio makubwa.

Asilimia 99 ya watu hawawezi kutegemewa kwa uhakika kwenye jambo lolote lile.
Ni watu ambao hawawezi hata kutimiza mambo waliyoahidi wao wenyewe.
Na pale wanapopewa jukumu lolote la kukamilisha, wanalikamilisha kwa kiwango cha chini sana, kama hata watakamilisha kabisa.

Ni asilimia 1 tu ya watu ndiyo wanaoweza kutegemewa kwa uhakika kwenye jambo lolote lile.
Hawa ndiyo wanaotekeleza kila wanachopanga na wakipewa jukumu wanakamilisha kama wanavyotegemewa.
Na ni asilimia hiyo 1 ndiyo wanaopata mafanikio makubwa kwenye maisha yao.

Njia pekee ya wewe kuweza kuingia kwenye asilimia 1 ya watu wanaofikia mafanikio makubwa kwenye maisha yao ni kutengeneza hali ya kuaminika na kutegemewa kwa uhakika na bila shaka yoyote.
Hapo unapaswa kuwa kama jua, mambo yako yote yanategemewa kwa uhakika.
Unatimiza kila unachoahidi mara zote.
Unahudhuria kwenye mambo yote kama unavyotegemewa.
Na unazalisha matokeo makubwa mara zote kwa uhakika kabisa.

Kuweza kutegemewa kwa uhakika mara zote kutakutofautisha sana na wengi ambao hawaeleweki nini wanafanya kwenye maisha yao.
Wengi wanaahidi vitu ila hawatekelezi na hilo wala haliwaumizi kwa namna yoyote.
Mahudhurio yao kwenye maeneo wanayotegemewa kuwa huwa siyo ya uhakika, sababu za kutokuhudhuria huwa ni nyingi.
Na matokeo wanayozalisha ni ya chini sana, kama hata watazalisha matokeo kabisa.
Unaweza kujionea mwenyewe kwa nini watu wengi hawajafanikiwa na hawataweza kufanikiwa.

Hilo linakuacha wewe na njia moja ya uhakika ya kuweza kupata mafanikio yoyote makubwa unayotaka kuyapata.
Njia hiyo ni KUWEZA KUTEGEMEWA KWA UHAKIKA MARA ZOTE.
Timiza kila unachoahidi, kwa kwenda hatua ya ziada.
Hudhuria zaidi ya unavyotegemewa kuhudhuria, mara zote kwa wakati na hata pale unapokuwa na sababu ambazo zingeweza kukuzuia usihudhurie.
Mara zote zalisha matokeo bora kabisa, zaidi ya inavyokuwa inategemewa.

Mambo hayo matatu ya kuzingatia hayaangalii umri wako, jinsia wala kiwango chako cha elimu.
Na ndiyo maana watu wa kila aina wanafanikiwa, bila ya kujali umri, jinsia au elimu.

Ufunguo wako wa mafanikio makubwa na ya uhakika upo kwenye mikono yako, ambapo ni KUTEGEMEWA KWA UHAKIKA.
Jijengee sifa ya kutegemewa kwa uhakika bila ya shaka yoyote ile na utaweza kupata chochote unachotaka.
Kuwa kama jua, tegemewa kwa uhakika kwenye mambo yako yote.
Ni sifa nzuri sana ya kuwa nayo kwenye zama ambazo wengi hawawezi kutegemewa kwa uhakika kwenye jambo lolote lile.

Kuweza kutegemewa kwa uhakika kunayafanya maisha ya watu wengine kuwa rahisi.
Watu wanapenda kujihusisha na wale wanaoyafanya maisha yao kuwa rahisi.
Hivyo unajionea hapo jinsi njia ya mafanikio makubwa ilivyo ya uhakika.
Siyo rahisi, lakini inawezekana.

Moja ya njia za kujijengea sifa ya kutegemewa kwa uhakika bila ya shaka yoyote ni kuwa na mchakato ambao tunaufuata mara zote kwa msimamo bila kuacha.
Kwa kuuweka mchakato wetu huo wazi kwa watu wote na kuutekeleza mara zote bila kuacha, kunakujengea sana sifa hiyo ya kutegemewa kwa uhakika.
Unapoenda hatua ya ziada katika kutekeleza mchakato wako hata pale mazingira yanapokuwa magumu, kunakujengea imani na heshima kubwa sana.

Unapoweza kutekeleza kila unachoahidi, kwa kufanya kila neno lako kuwa ndiyo sheria ambayo huivunji.
Kwa kuhudhuria mara zote na kwa wakati bila kuruhusu sababu au visingizio vyovyote kuwa kikwazo.
Ukiwa unazalisha matokeo bora zaidi kadiri unavyoendelea kwenda.
Kinachokuwa kimebakia ili kupata chochote unachotaka ni muda tu.
Hakuna kingine chochote kinachoweza kuwa kikwazo kwako.

TEGEMEWA KWA UHAKIKA NA BILA YA SHAKA YOYOTE na utaweza kupata chochote unachotaka kwenye maisha yako.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe