3242; Hujataka vya kutosha.

Rafiki yangu mpendwa,
Kama haupo tayari kutoa kafara na kupoteza vitu ulivyonavyo ili kupata kile unachotaka, basi jua hujakitaka vya kutosha.
Na kitu chochote ambacho hujakitaka vya kutosha, huwezi kukipata.

Kwa kitu chochote kile unachokuwa unakitaka, huwa kuna changamoto na vikwazo mbalimbali kwenye kukipata.
Kama hujajitoa kweli kupata kitu, hutaweza kuvuka vikwazo cha changamoto unazokutana nazo kwenye kukipata.

Dunia ina utele wa mafanikio na rasilimali mbalimbali ambazo watu wanakuwa wanazitaka.
Lakini duniavhuwa haipo tayari kutoa tu kwa kila anayetaka vitu hivyo.
Badala yake huwa inawajaribu na kuwapima watu ili kujua wamejitoa kiasi gani ili kupata kile wanachotaka.

Dunia inawaheshimu wale wanaotaka kitu hasa na kufanya kila wanachopaswa kufanya ili kukipata.
Na inawapuuza wale wanaotamani vitu ila hawajajitoa kweli ili kuvipata.

Kila kitu kwenye maisha huwa kina gharama zake. Na kadiri kitu kinavyokuwa kikubwa, ndivyo gharama yake inakuwa kubwa zaidi.
Dunia haiwapi watu kitu chochote kile bure, bali inawataka wakipambanie ndiyo waweze kukipata.

Kama kweli unakitaka kitu, kuwa tayari kujitoa hasa mpaka kukipata.
Na kama haupo tayari kujitoa hasa kupata kile unachotaka, usijidanganye nacho, jiambie tu wazi kwamba hukihitaji sana kisha endelea na mambo mengine.

Jinsi maisha yalivyo na vikwazo na changamoto, kujidanganya wewe mwenyewe ni kujiongezea mzigo usio na sababu.
Kama unakitaka kitu kweli kiendee kwa kujitoa hasa.
Na kama haupo tayari kujitoa hivyo, usijidanganye kwamba mambo yatatokea kimiujiza.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe