Sikiliza hapa;
Rafiki yangu Mpendwa,
Nimekuwa nakukumbusha sababu kuu mbili za maamuzi yote tunayofanya sisi binadamu. Sababu hizo zikiwa ni furaha na uhuru. Tunafanya maamuzi ili kuwa na furaha na kuwa huru zaidi. Hayo ndiyo mahitaji yetu ya msingi kabisa binadamu, ambayo tukiyatimiza, mengine yote yanakuwa sawa.
Lakini sasa, cha kushangaza, maamuzi mengi tunayoyafanya yanatukwamisha kwenye kupata matokeo hayo mawili. Tunafanya maamuzi ambayo yanatunyima furaha na yanatukosesha uhuru. Kwa bahati mbaya sana, wakati tunafanya maamuzi hayo tunadhani yatatupa vitu hivyo. Ni mpaka matokeo yanapokuja kuonekana ndiyo tunagundua kwamba tumepoteza vitu hivyo badala ya kuvipata.
Kibaya zaidi, kila tunapokazana kurekebisha makosa tuliyofanya, tunazidi kupotea zaidi. Tunapofanya maamuzi na kujikuta tumekosa furaha na uhuru, tunakimbilia kufanya maamuzi mengine ili kubadili hali hizo. Lakini matokeo yake ni tunazidi kukosa furaha na uhuru.
Hayo yote yamekuwa yanatokea kwa sababu namna tunavyofanya maamuzi yetu mengi siyo sahihi. Tunafanya kwa kuiga na kwa mazoea, kitu kinachopelekea tupate matokeo yale yale ambayo ndiyo tusiyoyataka.
Kwenye barua hii naenda kukuonyesha utumwa ambao umeuchagua mwenyewe, licha ya kuwa na uwezo wa kuishi kwa uhuru kamili kadiri ya unavyotaka. Kwa chochote unachoona ni kikwazo kwako, wewe mwenyewe ndiye uliyekisababisha.

1. Kila Unachofanya Ni Hiari Yako.
Hakuna kitu ambacho huwa kinanishangaza kama mtu mzima anapokuwa analalamikia kitu chochote kwenye maisha yake.
Unalalamika kwamba kazi unayoifanya huipendi na haikulipi vizuri, lakini ni wewe mwenyewe unayeamka kila siku asubuhi na kwenda kwenye kazi hiyo.
Unalalamika kwamba biashara unayofanya imegeuka kuwa mateso kwako, imechukua maisha yako yote na haikulipi vizuri. Lakini ni wewe mwenyewe unayeendelea kuifanya biashara hiyo kila siku, tena kwa namna ambavyo umekuwa unaifanya.
Unalalamikia mahusiano mbalimbali uliyonayo, jinsi watu wamekosa uaminifu, wanakukwamisha na kukuangusha. Lakini ni wewe mwenyewe umekuwa unawapa watu hao nafasi za kukukwamisha.
Unapolalamika, unaonyesha kwamba wewe ni mtumwa, ambaye maisha yako yanaamuliwa na watu wengine na wewe huna nguvu yoyote ya kubadili hilo.
Lakini unapokuja kuangalia kwenye uhalisia, uko huru kabisa kubadili chochote ambacho hakipo vile unavyotaka wewe. Hakuna mtu yeyote anayekulazimisha wewe ufanye kitu chochote.
Kesho unaweza kuamka na kukataa mambo yote ambayo unaona kwako hayako sawa na hakuna baya lolote litakalokutokea, zaidi ya wewe kuwa huru zaidi.
Inashangaza sana jinsi watu wengi wanachagua kuwa kwenye utumwa wa kulalamikia mambo mbalimbali, wakati wao wenyewe ndiyo wanaofanya maamuzi ya kuwa kwenye mambo hayo.
Najua unasema siyo rahisi kiasi hicho kufanya maamuzi ya haraka kwenye mambo unayolalamika, kwa sababu bado unayategemea sana kwenye kuyaendesha maisha yako.
Naelewa kabisa, kwamba pamoja na kutokuipenda kazi au biashara unayofanya, ndiyo inakuwezesha kuendesha maisha. Pamoja na watu kutokuaminika, ndiyo wanaokusaidia kwenye mambo muhimu unayofanya.
Pamoja na utegemezi huo ulionao kwenye mambo yanayokukwamisha, bado siyo sababu ya wewe kukaa kwenye hali ya utumwa. Bado ipo ndani ya uwezo wako kutengeneza uhuru wako kamili ili uyafurahie maisha unayoishi.
2. Wewe Ndiye Unayewajibika Na Maisha Yako.
Sisi binadamu tumetengeneza taasisi mbalimbali ambazo zina athiri namna tunavyoendesha maisha yetu. Taasisi hizo zinaanzia kwenye familia, jamii, mashirika, dini na siasa. Taasisi hizi huwa zinajipambanua kama zipo kwa ajili ya kutusaidia tuwe huru. Lakini lengo halisi la taasisi hizo ni kuwa na madaraka juu yetu, kututawala.
Na taasisi hizo hazina uwezo wa kututawala kwa mabavu, ni mpaka sisi wenyewe turidhie kutawaliwa nazo. Na hapo ndipo taasisi hizi zinapotafuta njia rahisi ya sisi wenyewe kukubali kuwa chini ya utumwa wake.
Kitu kikubwa ambacho taasisi hizi zimekuwa zinafanya ni kutuonyesha kwamba kuna adui anatukwamisha na taasisi hiyo ndiyo njia pekee ya kumshinda huyo adui. Kwa kifupi taasisi hizo zinatupa watu wa kuwalaumu pale mambo yetu yanapokuwa tofuati na tulivyotarajia.
Kwenye dini tunaambiwa shetani ndiye anayetukwamisha kuwa na maisha huru na ya furaha. Hivyo tunapaswa kusimama na dini ili kumwangusha shetani na maisha yetu yatakuwa mazuri.
Kwenye siasa tunaambiwa ni chama tawala au chama cha upinzani ndiyo kinatukwamisha kuwa na maisha huru na ya furaha. Kwamba tukiungana na upande sahihi, tutaweza kuangusha upande usio sahihi.
Mivutano hiyo imekuwepo miaka na miaka na haijawahi kubadili chochote. Zaidi imekuwa inatengeneza tabaka kubwa la watu wa chini ambao wanatawaliwa na tabaka dogo la watu wa juu ambao wanatawala.
Tabaka la juu linajua kabisa kwamba kile ambacho tabaka la chini linaaminishwa siyo sahihi. Hakuna yeyote anayewazuia watu kupata wanachotaka isipokuwa wao wenyewe. Lakini wakiwaambia watu huo ukweli, taasisi zao zitakosa nguvu ya kuwatawala watu.
Fikiria kwenye dini uambiwe hakuna shetani yeyote anayekukwamisha, ni uvivu na uzembe wako ndiyo umekuwa unakukwamisha. Badili tabia na jenga nidhamu sahihi na utapata matokeo. Kama njia ndiyo hiyo, utakuwa unaihitaji dini kwa ajili ya nini?
Fikiria mwanasiasa asimame jukwaani na kuhutubia akisema ninyi wananchi kafanyeni kazi na mtoe thamani kubwa ili mpate kulipwa. Na mkishalipwa, sehemu ya hayo malipo mtatuletea sisi ili tuyatumie kuendesha maisha yetu vile tunavyotaka na sehemu tutumie kuwapa huduma za msingi. Utaona umuhimu gani wa kumpigia kura mwanasiasa wa aina hiyo?
Hiyo mifano miwili ndiyo uhalisia ulivyo, lakini tumehadaiwa sana kwa kupewa maadui wa uongo ambao ndiyo tunaona wanatukwamisha.
Ukweli ni kwamba wewe mwenyewe ndiye unayewajibika na maisha yako. Haijalishi unaambiwa nini na taasisi mbalimbali zinazotaka kukutawala, maisha yako hayatabadilika mpaka pale utakapokubali kuwajibika.
Uhuru wako unaanza na wewe kupokea wajibu wa maisha yako. Hilo liko ndani ya uwezo wako kabisa, huhitaji ruhusa ya yeyote ndiyo utekeleze.
Wala huhitaji kuzipinga na kuzikataa taasisi zilizopo, na ambazo upo. Endelea nazo, lakini usinunue uongo ambao taasisi hizo zinakuuzia. Wewe shika hatamu ya maisha yako, kubali kuwajibika kwa maisha yako na pambana kujenga aina ya maisha unayoyataka.
Endelea kusoma #BaruaYaKocha hapa; #BZK086; Kwa Nini Umechagua Huu Utumwa Kwenye Ulimwengu Unaoweza Kuwa Huru?