Rafiki yangu Mpendwa,
Sisi binadamu siyo wakamilifu, tuna madhaifu mengi ambayo hatuna namna ya kuyabadili. Huo ndiyo ukweli, ambao hakuna mtu yeyote anayeweza kuukataa.
Lakini sasa, mafanikio makubwa yanataka mtu awe na ukamilifu kwenye kile anachotaka kufanikiwa. Mafanikio hayajali kabisa hali yetu sisi binadamu kuwa na udhaifu. Mafanikio yanataka ukamilifu, wa kila kinachohitajika kwenye mafanikio kuwepo.
Ukiacha mafanikio kutaka ukamilifu, hali yetu ya kutokukamilika imekuwa inatumika kama kisingizio cha kufanya mambo yasiyo na tija. Watu wamekuwa wanafanya mambo yanayowakwamisha, kwa makusudi kabisa na kusingizia kwamba ni udhaifu wa kibinadamu.
Tunajua jinsi ambavyo mafanikio makubwa na visingizio haviwezi kwenda pamoja. Ni lazima uchague kama unataka kupata mafanikio makubwa na kuyapambania au kama unataka kujipa visingizio ili kujiridhisha licha ya kuyakosa mafanikio.
Kama unachotaka ni mafanikio makubwa, ni lazima pia uwe na ukamilifu ambao mafanikio hayo yanataka uwe nao. Pamoja na asili yako ya kukosa ukamilifu, yale maeneo ambayo yanajenga mafanikio makubwa unayoyataka ni lazima yawe na ukamilifu unaohitajika.
Kwenye hii #BaruaYaKocha unaenda kujifunza kuhusu ukamilifu unaohitajika na maeneo ambayo ni lazima uwe na ukamilifu kama unataka kupata mafanikio makubwa kwenye maisha yako. Kwa jinsi ukamilifu umekuwa unazungmziwa, unaweza kuona ni kitu kigumu kufikiwa, lakini kwenye barua hii utaona jinsi inavyowezekana kabisa.

1. Kuwa Na Kitu Kimoja Kamilifu Kwenye Maisha Yako.
Kuna vitu vingi unavyofanya kwenye maisha yako, lakini siyo vyote vitakavyokupeleka kwenye mafanikio makubwa unayoyataka. Mafanikio ya aina yoyote ile huwa yanatokana na vitu vichache sana, huku kukiwa na kimoja ambacho ndiyo kinabeba sehemu kubwa ya mafanikio ambayo mtu unayataka.
Inapokuja kwenye mafanikio makubwa, yanataka mtu afanye kwa viwango vya juu sana kitu kimoja anachokuwa amechagua. Kwenye kitu hicho, mtu hapaswi kabisa kutafuta usawa au mlinganyo na vitu vingine. Kitu hicho kinapaswa kuwa ndiyo kipaumbele namba moja kwenye maisha yake na kuwa tayari kupuuza mengine yote ili kufanyia kazi hicho.
Hicho ndiyo kitu kinachokuwa kinahitaji ukamilifu ili mafanikio makubwa yapatikane kama yanavyohitajika. Kitu unachokuwa umechagua lazima ukifanye kwa ukamilifu, huku ukiendelea kukiboresha kadiri unavyokwenda. Unapaswa kufanya kila kinachopaswa kufanyika bila ya kuacha chochote kwa sababu zozote zile.
Kile unachokuwa umechagua kufanikiwa, hakihitaji sababu wala visingizio bali kufanywa kwa ukamilifu wake. Hakijali kama umechoka au hujisikii kufanya, kinapaswa kufanywa na lazima ukifanye.
Huwezi kuwa na ukamilifu kwenye mambo yote, lakini unaweza kupambania ukamilifu kwenye kitu kimoja. Na ukamilifu huo haimaanishi kwamba hutakosea, bali inamaanisha wewe utafanya kila kinachohitajika kufanyika na hata ukikosea utaboresha na kurudia kufanya.
Kadhalika ukamilifu kwenye jambo unalochagua haimaanishi utapata matokeo unayotaka kwa wakati unayataka. Unaweza kupambania ukamilifu kwenye kitu hicho na bado usipate matokeo unayoyataka. Lakini hilo halimaanishi uache kufanya, badala yake unapaswa kuendelea kufanya kwa ukamilifu zaidi.
Ukishachagua kitu kimoja unachotaka kikupe mafanikio makubwa, hicho ndiyo kinapaswa kumeza maisha yako yote. Unapaswa kukifanya kwa namna ambayo wengine wataona unajitesa au umepotea. Hicho ndiyo kiwango cha ukamilifu unachopaswa kukipambania ili upate mafanikio makubwa unayoyataka.
Ni lazima uwe tayari kufanya kitu hicho wakati wote. Usahau hata kula kwa sababu umemezwa na kitu hicho. Ukose usingizi kwa sababu ya kufanya kitu hicho. Na zaidi, uachane na starehe na anasa zote na kuwa na hobi moja tu, kufanya hicho kitakachokupa mafanikio.
Chini ya hayo uliyojifunza hapo ni kukosa ukamilifu. Kufanya kitu huku ukiangalia muda wa kumaliza kukifanya, kufanya huku ukiwa na hobi nyingine zinazokusumbua ni kukosa ukamilifu.
Ukamilifu kwenye kitu unachokuwa umechagua unaanzia kwenye wewe kufanya na siyo kwenye matokeo unayopata. Ukamilifu ni wewe kufanya kila kinachopaswa kufanyika, kwa namna ambayo kinapaswa kufanywa, wakati ambapo kinapaswa kufanywa na kurudia hivyo wakati wote. Chochote tofauti na hivyo ni kukosa ukamilifu na kujizuia kufanikiwa.
2. Kuwa Na Siku Na Muda Kamilifu Wa Kufanya Kitu Chako Kamilifu.
Sababu kubwa ambayo watu wamekuwa wanaitoa ya kushindwa kukamilisha wanayopaswa ni muda. Watu wamekuwa wanalalamika kwamba mambo ya kufanya yamekuwa ni mengi, lakini muda wa kuyafanya umekuwa mchache.
Lakini unapoangalia kwa karibu, unagundua watu wote duniani tuna muda sawa. Waliofanikiwa wana masaa 24 kwa siku na walioshindwa pia wana muda huo. Kama watu wote wana muda unaolingana, lakini matokeo yao yanatofautiana, muda hauwezi kuwa tatizo. Tatizo kubwa linaweza kuwa matumizi sahihi ya muda ambao mtu anao.
Ili kupata mafanikio makubwa unayoyataka, ni lazima uwe na muda kamilifu, ambao utautumia kufanya kitu kamilifu ulichochagua. Unajua ukisema ukipata muda utafanya kitu fulani, unajidanganya. Hakuna siku yoyote ambayo utapata muda, muda tayari upo, ni wewe utenge muda wa kufanya unachopaswa kufanya.
Ili uweze kutenga muda na kufanya yanayopaswa kufanyika, ni lazima uchague ukamilifu kwenye muda. Na ukamilifu huu wa muda upo kwenye pande mbili, muda wa siku na siku ya wiki.
Kwenye muda wa siku, kila siku yako tenga muda ambao ni kamilifu. Kwenye muda huo kamilifu, fanya yale tu yanachochangia kwenye mafanikio makubwa unayoyataka. Hupaswi kufanya kitu kingine chochote kwenye muda huo uliotenga. Muda unaotenga kila siku kwa ajili ya mafanikio yako makubwa unapaswa kuwa muda takatifu, ambao hutauvuruga na kingine chochote. Pangilia yote utakayoyafanya kwenye muda huo na yafanye kama ulivyopanga.
Muda mzuri wa siku wa kuutumia kikamilifu ni wa asubuhi. Pangilia muda wako wa asubuhi kwa ajili ya kutekeleza mambo muhimu yanayochagia kukupa mafanikio makubwa unayoyataka. Asubuhi ni nzuri kwa sababu dunia inakuwa bado imelala hivyo usumbufu unakuwa mdogo. Na unapokuwa umeamka mapema kuliko wengine, unapata utulivu wa kukutosha kufanya kwa ukamilifu kile ulichochagua. Kiwango cha chini kabisa cha kutenga kwenye siku kwa ajili ya ukamilifu wa mafanikio ni saa moja, usikubali kugawa masaa yako yote ya siku kwenye vitu vingine na ushindwe kutenga hata saa moja kwa ajili ya mafanikio yako makubwa. Unaweza kutenga muda mwingi uwezavyo, ila usipungue saa moja.
Kwenye siku ya wiki, unapaswa kutenga siku moja kwenye wiki ambayo utaitumia kikamilifu. Kwenye siku hiyo ya wiki, unapaswa kuitumia kutekeleza yale tu yanayochangia kwenye mafanikio makubwa unayoyataka. Unaitumia siku hiyo kama tayari umeshapata mafanikio makubwa unayoyataka na hakuna kinachokusumbua. Siku nyingine zote za wiki ziishi kama ambavyo umekuwa unaishi, ila kwa siku moja, maisha yako yanapaswa kuwa tofauti kabisa, yanapaswa kuwa na ukamilifu mkubwa.
Unapaswa kuchagua siku ya wiki ambayo unajua unaweza kupuuza mambo mengine yote na isiwe na madhara makubwa kwako. Ikiwa siku ya wiki ni vizuri, ikishindikana chagua hata siku ya mwisho wa wiki, ambapo kwa wengi inakuwa mapumziko. Kwa siku unayochagua, ipangilie tangu unapoamka mpaka unapoenda kulala. Panga ratiba kamili ya kila kinachopaswa kufanyika na muda wa kukifanya. Ukishapanga, fuata kile ulichopanga bila ya kubadili au kuyumbishwa kwa namna yoyote ile.
Kuiishi siku nzima kikamilifu linaweza kuwa zoezi gumu sana, lakini unapaswa kujikumbusha ni siku moja tu kati ya siku 7, hivyo una siku 6 za kuishi vile unavyotaka. Hiyo siku moja inaweza kuonekana kama siku ya kifungo gerezani, lakini ni lazima uikamilishe ili uweze kupata mafanikio makubwa unayoyataka. Usigawe siku zako zote za wiki kwenye mambo yote, tenga siku moja kwa ajili ya mafanikio yako makubwa.
Endelea kusoma #BaruaYaKocha hapa; #BZK126; Tumia Huu Ukamilifu Kupata Mafanikio Makubwa Kwenye Maisha Yako