Katika moja ya tabia za binadamu ni ubinafsi, unaweza kukataa lakini huo ndio ukweli. Kila mtu anatumia muda mwingi kuwaza mambo yake mwenyewe, yaweza kuwa maendeleo, matatizo ama chochote kile. Kwa muendelezo wa tabia hiyo hata malengo na mipango yote anayoweka mtu inakuwa inamhusu yeye tu ama na ndugu zake. Ni wachache sana kwenye malengo na mipango yao wanaijumuisha jamii inayowazunguka. Naposema jamii inayokuzunguka namaanisha watu wote walio kwenye eneo unaloishi, mtaa, wilaya, mkoa, nchi nzima na hata bara na dunia kwa ujumla.
Tabia hii ya ubinafsi inaongezwa zaidi na mfumo wa elimu tuliopitia. Shuleni unasisitiziwa umekuja mwenyewe na utaondoka mwenyewe, mnafundishwa pamoja ila mtihani unapewa mwenyewe. Unaweza kuona ni kitu cha kawaida tu ila kina mchango mkubwa sana kwenye tabia ya ubinafsi. Ndio maana mwisho wa siku kila anaemaliza kusoma anajifikiria yeye mwenyewe na familia yake. Jamii inayomzunguka anaona haimhusu. Ni kweli inaweza kuwa haikuhusu kwa sababu kila mtu ana maisha yake, ila unayajua madhara ya wewe kuiacha jamii nyuma?
Unaweza kuwa na maendeleo sana, ukawa tajiri mkubwa ila kama jamii inayokuzunguka ina maisha magumu ama hali ngumu basi jua kabisa haupo salama.
Itakuwa vigumu kwa wewe kuishi kwa amani kwenye jamii iliyo na hali ngumu. Kwa kuwa hali yao ni ngumu na wewe una hali nzuri sana kuizidi jamii hiyo watashindwa kuvumilia na hivyo watakuchukia, na watakuibia. Unaweza kusema utawapa fedha ili wasikuibie, je utawapa kila siku? na utawapa wangapi?
Pamoja na maendeleo yako makubwa na utajiri utakaoufikia kama jamii inaykuzunguka ina hali ngumu basi wote mnawekwa kwenye kundi la maskini. Kama ilivyo kwamba Tanzania ni nchi maskini na kwa wastani watu wanaishi chini ya dola moja kwa siku. Japo kuna matajiri wakubwa sana hapa nchini lakini tunapokuja kuchukulia hali ya wananchi kwa ujumla wote tunanekana maskini.
Naandika haya kukumbushana kwamba tuwe na mipango inayokwenda sambamba na jamii inayokuzunguka. Angalia njia unayoweza kuisaidia jamii kujikwamua na hali ngumu ili uweze kuishi kwa amani na jamii yako. Hili halihitaji wewe uwagawie watu fedha, bali waoneshe picha kubwa na jinsi ya kuifikia. Ukiwawezesha wengi na hao wengi wakawawezesha wengi zaidi moja kwa moja jamii inajikwamua kutoka kwenye hali ngumu. Inawezekana, anza sasa kwa kuwa na mchango bora kwa jamii yako.
TAFADHALI WEKA MAONI YAKO HAPO CHINI KWA LOLOTE UNALOFIKIRI KUHUSIANA NA MADA HII. USIONDOKE BILA KUSEMA CHOCHOTE, MAONI YAKO NI YA MUHIMU SANA KWETU.
KAMA UMEIPENDA HII MADA TAFADHALI BONYEZA KIALAMA CHA FACEBOOK NA TWITTER KUSHOTO KWAKO KUWASHIRIKISHA RAFIKI ZAKO WA FACEBOOK NA TWITTER ILI UJUMBE HUU UWEZE KUWAFIKIA NA KUWABADILI WENGI. ASANTE SANA KWA USHIRIKIANO WAKO