Nikikuuliza maisha ni nini unaweza kunipa majibu mengi sana ambayo yote yanaweza kuwa sahihi kulingana na mtazamo wako. Kuna wanaosema maisha ni safari, wengine wanasema maisha ni vita na hata wengine wanasema maisha ni zawadi.

  Bila ya kujali unayaelezea vipi maisha binadamu wote duniani tunaishi. Tunaishi maisha ambayo yanafanana ila tofauti ni viwango vya maisha yetu. Kuna watu wanaonekana kuishi maisha wanayoyafurahia na wanapata kila wanachotaka kwenye maisha. Kwa upande mwingine kuna watu wanaishi maisha wasiyofurahia, wamekata tamaa na wanasubiri tu siku ya kufa.

  Je wewe uko upande upi wa maisha? Unaishi maisha ambayo unayafurahia na unatamani kesho ifike ama unaishi maisha unayoona ni kisirani na hutaki hata kuisikia kesho kwa sababu unajua haina tofauti na leo? Unaishi maisha yaliyokuchosha na kila siku unajikuta unalalamika tu ila wenzako wanayafurahia maisha?

  Bila ya kujali umri, kipato, elimu na hata rangi binadamu wote tunaingia kwenye makundi mawili ya maisha. Kuna kundi la kwanza ambalo waliopo kwenye kundi hilo wanayafurahia maisha, wanapata kile wanachotaka na wanatamani kesho ifike ili waendelee na maisha yao ya furaha. Kuna kundi la pili ambalo waliopo kwenye kundi hilo wamekata tamaa na maisha yao na wanaishi maisha magumu ambayo wameshayachoka. Katika kundi hili kuna wengine wameshakufa ila bado wanatembea(soma hapa). Kwa bahati mbaya sana kundi hili la pili ndio lina watu wengi sana.

          LIFE GAME

  Ni nini kinaleta tofauti ya makundi haya? Ni hela, utajiri au ujanja? Unaweza kukimbilia kusema ni hela ila upo mbali sana na ukweli. Kuna siri kubwa sana ya maisha ambayo wanaofurahia maisha wanaijua na wanaoishi maisha wasiyofurahia hawaijui. Huenda na wewe hujaijua siri hiyo mpaka sasa ndio maana maisha yako bado ni magumu. Hapa utaijua siri hiyo na kama utaanza kuifanyia kazi utaona mabadiliko makubwa kwenye maisha yako.

  Siri kubwa sana kwenye maisha ni kwamba MAISHA NI MCHEZO. Hiyo ndio siri ambayo mpaka sasa ulikuwa hujaijua. Maisha ni mchezo na ili uweze kucheza mchezo huu ni lazima ujue sheria zake. Kila mchezo unasheria zake na mchezaji anapokwenda kinyume anapata adhabu fulani. Hata maisha yako hivyo hivyo, kama hujui sheria za mchezo huu mkubwa unaishia kupata adhabu na kutofurahia mchezo huu.

  Tofauti ya wanaofurahia maisha na wasiofurahia ni kwamba wanaofurahia wanazijua sheria za huu mchezo na wasiofurahia maisha hawajui hata kama sheria zipo, wamejikuta tu uwanjani. Kutokujua sheria za mchezo huu mzuri kumefanya watu wengi kutoweza kuucheza na kujikuta wakitazama wengine ambao wanaucheza vizuri sana.

  Ni mara ngapi umekuwa ukitamani maisha ya wengine? Ni mara ngapi umekuwa ukiona watu fulani wanafanikiwa kwenye kila wanachofanya ila wewe unashindwa? Hao unaowaangalia ndio wanaucheza mchezo vizuri kwa kuwa wanazijua sheria. Na kwa kuwa wewe huzijui sheria umeishia kuwa mtazamaji kwenye mchezo huu. Tena kwa bahati mbaya zaidi unalipia kuwa mtazamaji kwenye mchezo huu kwa sababu ni gharama sana kwako kama hujui sheria za huu mchezo.

  Kama ilivyo kwenye mpira wa miguu ambapo kuna watu wachache(wasiozidi 22) wako uwanjani wanacheza na kuna maelfu ya watu wamezunguka kuwatazama ndivyo maisha yalivyo.

 

  Kwa nini wewe huzijui sheria za mchezo huu?

  Kwa bahati mbaya sana hakuna popote kwenye maisha yetu ambapo tunafundishwa sheria za mchezo huu. Sio kwenye mfumo wa elimu wala kwenye malezi ya familia. Jamii ndio kabisa haijui hata kama huu mchezo upo. Kutokana na kutokufundishwa kokote wachache waliojua siri za mchezo huu walizijua kwa kupitia njia ngumu. Kwa kujaribu na kushindwa na kujaribu tena na tena bila ya kukata tamaa walizijua sheria mbalimbali za mchezo huu.

  Hakuna sehemu yoyote hasa kwenye mfumo wa elimu ambapo unafundishwa sheria hizi muhimu za mchezo huu; kuweka malengo na jinsi ya kufikia, jinsi ya kupambana na nyakati ngumu kwenye maisha yako na kuzivuka, jinsi ya kujihamasisha na kutokata tamaa, jinsi ya kutengeneza utajiri, jinsi ya kuwa na nidhamu nzuri ya muda na fedha, jinsi ya kupambana na changamoto za maisha na jinsi ya kutumia mazingira, vipaji na uwezo mkubwa ulio nao kuboresha maisha yako.

  Hakuna sehemu yoyote kwenye elimu umewahi kuambiwa kwamba wewe una uwezo mkubwa sana ndani yako na unaweza kufanya chochote unachotaka kufanya na kuwa vyovyote unavyotaka kuwa. Hujaambiwa kwamba hata kama umekosa vitu gani ukiweza kutumia akili yako tu unaweza kubadili maisha yako yakawa bora na ukayafurahia sana.

  Mambo hayo yote yaligunduliwa na waliojifunza sheria hizi kupitia njia ngumu. Na uzuri ni kwamba hawakuwa wachoyo na kutunyima maarifa haya. Wamekuwa wakitushirikisha maarifa haya mazuri na hata mpaka sasa japo wengi wao wamekufa bado tunaishi na maarifa yao. Maarifa hayo yameandikwa kwenye vitabu mbalimbali ambavyo vimewasaidia watu wengi sana kubadili maisha yao. Vitabu hivyo ndivyo nimekuwa nikiwatumia wanachama wa mtandao huu wa AMKA MTANZANIA.

  Pia maarifa hayo ndiyo nimekuwa nikiyaandika kwenye makala mbalimbali hapa AMKA MTANZANIA. Hebu na wewe uchukue hatua sasa ya kujifunza sheria za mchezo huu muhimu kwako na uanze kuufurahia. Weka utaratibu wa kusoma japo makala moja kila siku kwenye mtandao huu wa amka mtanzania. Usitake kusoma zote kwa wakati mmoja hutozimaliza maana ni nyingi sana. Hata kama umekuwa unazisoma mara kwa mara hebu chagua makala chache urudie kuzisoma ili uendelee kujifunza zaidi.(Anza na makala hizi zilizosomwa sana mwaka 2013)

  Pia kama unataka kujifunza sheria hizi jiwekee utaratibu wa kujisomea japo kitabu kimoja kwa mwezi. Tenga nusu saa au saa moja kwa siku ya kujisomea kitabu na ndani ya mwezi mmoja utakuwa umemaliza kusoma kitabu kimoja. Ndani ya mwaka utakuwa umemaliza kusoma vitabu 12, maisha yako yatakuwa mara 12 bora zaidi ya yalivyo sasa. Kupata vitabu hivi tafadhali bonyeza hapa na uweke email yako kisha utaingia kwenye utaratibu wa kutumiwa vitabu. Kupata vitabu vya nyuma bonyeza hapa na uweze kupata maelezo ya kitabu husika na ukidownload.

  Amua leo kuacha kuwa mtazamaji kwenye mchezo huu muhimu sana kwako. Amua kuingia uwanjani na kila mtu akushangilie wewe. Fanya hivyo ukiwa unazijua sheria za mchezo huu. Na njia pekee ya kuzijua sheria hizo ni kusoma makala mbalimbali hapa AMKA MTANZANIA na kujisomea vitabu mbalimbali unavyotumiwa ama ambavyo ulishatumiwa.

  Nakutakia kila la kheri na nikuhakikishie hakuna linaloshindikana kama kweli utaamua.