Usifuate Ushauri Wa Watu Hawa Watatu.

  Katika safari yako ya mafanikio kwenye maisha kuna wakati unahitaji au utahitaji ushauri wa watu wengine ili kuvuka changamoto unazokutana nazo. Ushauri unaopewa unaweza kuwa mzuri na ukakusaidia sana au unaweza kuwa mbaya ukakupoteza zaidi.

  Unawezaje kujua ushauri mbaya na ushauri mzuri? Unawezaje kujua mtu anayetoa ushauru mzuri ambao utakusaidia kufikia ndoto zako? Hii ni changamoto kubwa inayohitaji busara ili kuweza kuivuka.

             ushauri2

  Inapokuja kwenye kutoa ushauri kila mtu anapenda kutoa ushauri na kama hiyo haitoshi kila mtu anapenda ushauri wake uonekane ni wa muhimu. Hujawahi kukuta watu wakijadili maamuzi aliyofanya mtu na kusema labda angefanya kitu fulani angefanikiwa zaidi, huku watu hao hawajui malengo ya wanayemuongelea? Watu wanapenda sana kutoa ushauri nakuamini ushauri wao ni muhimu.

  Kutokana na changamoto hii ya kila mtu kuweza kutoa ushauri inabidi uwe makini sana ni ushauri wa nani utakufaa. Inawezekana kuna mtu amefanikiwa kwenye hicho unachofanya au unachotaka kufanya. Kutokana na mafanikio yake makubwa basi ushauri anaokupa wewe unachukua kama sheria na huufikirii sana. Kwa mtu kuwa amefanikiwa bado hamfanyi kuwa mshauri mzuri.

  Mtu anaweza kuwa amefanikiwa sana ila kwenye kutoa ushauri akawa mbovu na kusababisha anaowapa ushauri wazidi kupotea. Ili uweze kuepuka ushauri mbaya kwenye maisha yako hapa nitazungumzia aina tatu za watu ambao usidhubutu kuchukua ushauri wao.

1. Watu ambao wanajiona wanajua kila kitu.

  Kwenye maisha kuna watu unawajua ambao huwa wanafikiri wanajua kila kitu. Jambo lolote linalozungumzwa hawakosi cha kuchangia. Watu hawa wanajua vitu juu juu na hawana uelewa wa ndani ila wanapenda sana ushauri wao uchukuliwe. Epuka ushauri wa watu hawa kwa sababu hawana uelewa mkubwa kwenye jambo lolote wanalodhani wanalijua. Kutaka kwao kujua kila kitu kunawafanya washindwe kuzama ndani na kujua mambo machache kwa undani.

  Tayari unawajua watu hawa kwenye maisha yako. Wanapokupa ushauri wasikilize, maana wengine unaweza kuwa unawaheshimu sana, ila usitekeleze ushauri wanaokupa. Ushauri wao hauna msaada mkubwa.

2. Watu Wanaokushauri uwe makini sana na ucheze salama.

  Kuna watu ni waoga sana hivyo wanapotoa ushauri kwa mtu wanaweza kutoa ushauri mzuri ila wanasisitiza kuwa makini sana na kucheza salama. Watu wa aina hii watakuogopesha kuhusu hatua kubwa unayotaka kuchukua na utashindwa kufikia mafanikio makubwa. Ili kufikia mafanikio makubwa kuna wakati inabidi uchukue maamuzi ya hatari(take risk), sasa kama mshauri wako anakuambia uogope hatari itakuwa vigumu sana kwako kufikia malengo yako makubwa. Watu wa aina hii inabidi hata usiwaambie unachotaka kufanya kwa sababu wanaweza kuanza kukukatisha tamaa hasa inapokuwa ni watu wenye ushawishi mkubwa kwako. Unakumbuka vizuri nyakati uliacha kufanya mambo kwa sababu watu walikwambia huwezi au utashindwa. Waepuke sana watu wa aina hii.

kitabu kava tangazo 150W

 

3. Watu wenye maslahi na jambo unaloomba ushauri.

  Usiombe ushauri kwa mtu ambaye ana maslahi na yambo unaloombea ushauri, atakupa ushauri ambao unamnufaisha yeye bila ya kujali wewe unanufaika au la. Kwa mfano unataka kufanya biashara halafu ukaenda kumwomba ushauri mtu anayefanya biashara unayotaka kufanya na kuonesha kwamba unataka kuifanya tena kwa eneo analofanyia yeye. Unafikiri atakujibu nini juu ya biashara hiyo? Atakwambia haina faida, sio nzuri na majibu mengine ya kukukatisha tamaa.

  Kama unayemwomba ushauri ananufaika na wewe kushindwa kwenye hicho unachoombea ushauri hawezi kukupa ushauri mzuri. Na pia kama ananufaika na wewe kufanikiwa kwa unachotaka kufanya hawezi kukupa ushauri mzuri. Tafuta ushauri kwa mtu ambae hana maslahi ya moja kwa moja kama utafanikiwa au utashindwa.

  Ushauri mbaya ni hatari kuliko kutokuwa na ushauri kabisa. Chunguza sana watu unaochukua ushauri wao, wanaweza kuwa ndio chanzo cha wewe kushindwa. Pata ushauri kwa watu wanaofanya kwa vitendo na watakaokuambia ukweli bila ya kuwa na maslahi kwenye unachofanya.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s

Create a website or blog at WordPress.com

Up ↑

%d bloggers like this: