MAKALA HII IMEANDIKWA NA IMANI NGWANGWALU WA TANGA TANZANIA.

Maisha ni kanuni ndio maana kuna mambo ambayo hata ungefanyaje huwezi kuyabadili bali yenyewe ndiyo yanayobadili maisha. Hii inamaana kwamba kwenye maisha kila kitu kinakwenda kwa kanuni zake. Kanuni hizo ndizo zinasababisha mambo kutokea katika maisha ya kila siku na zinanapokuwa zinavunjwa kuharibiwa hutokea. Kwa bahati mbaya au nzuri kanuni hizi zinamhusu kila mtu uwe unajua au hujui zinatenda kazi.

Kanuni ya kupata kile unachokihitaji katika maisha ni moja kati ya kanuni inayoongoza maisha yetu. Ni moja ya nguvu kubwa sana hapa duniani. Nguvu hii au kanuni hii hujidhihirisha katika namna tofauti kila siku katika maisha ya jinsi namna tunavyoishi.

Kanuni hii inafahamika na wengi ingawa hawajui. Mfano inajidhihirisha katika misemo mbalimbali kama vile unavuna ulichokipanda, toa fedha upate fedha, kinachotoka hurejea, na vitu vifananavyo huvutana, hii ikiwa na maana ya kwamba kwa kawaida vitu vinavyofanana vinauwezo wa kuvutana kimasafa na kimtikisiko.

Kanuni hii inapokuwa inafanya kazi ina uwezo wa kuvuta watu, kazi, neema, fedha na majibu ya mambo mengine mengi katika maisha.

Unapokuwa unamudu kutumia kanuni hii inakuwa inashangaza sana kwa sababu itafika mahali ambapo utaona yale au kila kinachotokea mara ukipatapo ni kama ndoto fulani.

Elewa ukweli huu, kila kitu ambacho binadamu anahitaji kipo na kinapatikana, kama kweli umeamua kukipata utakipata maana unakipata kile unachokizingatia katika akili yako, uwe unakitaka au la. Mawazo yako yana nguvu ya kuumba.

Kanuni hii inapotumiwa haichagui mtu, rangi, kabila au taifa inafanya kazi popote na kwa ufanisi mkubwa sana.Ili uweze kupata unachohitaji kwa kutumia kanuni hii ni lazima ujue namna ya kuweza kuitumia na kuleta matokeo chanya maishani mwako.

Hivi ndivyo kanuni ya kupata unachohitaji unavyoweza kuitumia katika maisha yako kwa kujua mambo yafuatayo:-

1. KUPANIA KIFIKRA

Inatakiwa hapa kujifunza kutofikiri mambo usiyoyahitaji, fikiria mambo ambayo unayotaka yawe ndani ya maisha yako. Unapofikiria mambo usiyoyahitaji utayapata tu hata kama hutaki. Wewe pania kufikiria mambo mazuri utaona mambo mazuri kwelikweli.

Hakikisha unafikiri na kuweka kwenye picha kitu unacho hitaji hapa pia unaweza kutumia maneno ya kujisemea katika kitu hicho (Maneno ya umiliki) au hata pia unaweza ukajiweka katika hali ya mtu anayefaidi jambo hilo.

Kitu unachokuwa unafanya bila kujijua wewe mwenyewe unapoweka picha kichwani ya jambo unalotaka liwe na kujirudia rudia unakuwa unarutubisha mawazo ya kina ambayo yana wezesha jambo liwe.Kumbuka kuna mawazo ya aina mbili mawazo ya nje na mawazo ya kina. Mawazo ya kina ni mawazo ambayo hufanya kazi saa 24 hata tukiwa tumelala.Mawazo haya hayana ‘akili’ yanafanyia kazi chochote kinachokuja kwenye ubongo kiwe kibaya au kizuri. Mawazo ya kina yanatoa majibu kwa kile unachokizingatia tu.Kama unataka kufanikiwa pania kifikra kwa kuzingatia unachotaka tu.

clip_image002

2. KUPANIA KIHISIA

Ili uvute vizuri unachokihitaji unachotakiwa hapa ni lazima hisia zako ziwe nzuri wakati wote ambapo zinakuwa hazikuumizi hata wewe. Hisia zina nguvu kubwa sana ndani yako kuliko unavyofikiria. Kama kila wakati ndani yetu tutakuwa na kiasi kikubwa na hisia hasi kama vile kujuta, hasira, uchungu, kukata tamaa, choyo, kulipiza kisasi, kijicho, huzuni na hisia kali nyinginezo. Tutaharibu kazi yoyote nzuri ambayo ilitakiwa iwe upande wetu au hutapata kile unachohitaji kama utakuwa na hisia hasi nyingi.

Wengi wetu kuwa na hisia nzuri ni kama ajali. Kwa sehemu kubwa, wengi tumezoeshwa kuwa na hisia mbaya ndio maana tunakuwa watu wabaya kila kukicha. Kwa bahati mbaya hisia hizo zinakuwa zina madhara makubwa sana kwetu mfano unapotaka kulipa kisasi anayeanza kuumia ni wewe unayepanga kulipa kisasi.Hisia mbaya wakati mwingine zinawaongoza watu mpaka kujikosoa wenyewe, kutilia mashaka uwezo wao, kutarajia maanguko na kujishusha sana mambo ambayo yanasababisha wao wenyewe kuumia sana. Ukweli ni kwamba tunatakiwa tujue namna ya kuzifanya hisia zetu ziwe nzuri ili tuweze kufanikiwa zaidi.

3. KUPANIA KIKAULI

Hapa hakuna kutoa kauli za mambo usiyoyahitaji. Toa kauli za ushuhuda wa ushindi tu kama vile umeshafanikiwa na kukipata kile unachikihitaji. Kwa kawaida kauli zina nguvu ya kubadili au kufanya mambo kuwa kama yule mwenye kutoa kauli anavyotaka iwe.

Kwa hiyo kauli au maneno yetu yanaweza kuwa chanzo cha mafanikio yetu au maangamio yetu. Kwa nini? Kwa sababu kauli zina nguvu ya kuzaa. Inategemea tu kauli gani unayoitoa. Kwa hiyo mtu anaweza kutumia kauli kwa kufanya vizuri maisha yake au kufanya uharibifu mkubwa kwenye maisha yake mwenyewe. Kwa mfano unaweza kutumia kauli kwa kulenga jambo ambalo unataka liwe katika maisha yako kwa kulitamka mara kwa mara na kufanikiwa kwa haraka kuliko ulivyokuwa ukifikiri. Hiyo yote kufanikiwa kwa jambo ambalo ulikuwa unalenga inatokana na jinsi ambavyo kauli zinaweza kuwa na nguvu katika maisha yetu.

Hapa unachotakiwa ni wewe mwenyewe kujifunza namna ya kutumia kauli zako vizuri ili uweze kupata kile unachokihitaji.

4. KUPANIA KIVITENDO

Ni lazima uwe na matendo ambayo yanaendana na mkabala wa kile unachokipenda na si kile ambacho hakipendi utaona mafanikio yanakuja yenyewe tu. Kama kweli unataka kuzibadilisha ndoto zako na kuwa kitu cha kweli, hakuna kitu kingine zaidi ya kupania kivitendo. Kuongea sana hakusaidii lolote na wala hakutakuja kukusaidia.Kitakachokusaidia wewe ni mipango inayoambatana na vitendo ndicho kitu cha msingi.

Hivi ndivyo kanuni ya kuvuta kile unachokihitaji inaweza kufanya kazi maishani mwako na ukaona matokeo chanya.Ukifanyiwa mazoezi mambo hayo manne utajikuta unamudu kuwa na utulivu mkubwa ndani mwako na utaanza kuyathibiti maisha yako na siyo kuthibitiwa na maisha.

Nakutakia mafanikio mema chukua hatua juu ya maisha yako na endelea kufatilia mtandao huu wa AMKAMTANZANIA kwa mambo mengi mazuri zaidi TUKO PAMOJA.

UNAWEZA KUWASILIANA NA MWANDISHI WA MAKALA HII IMANI NGWANGWALU KWA 0767048035.

KAMA NA WEWE UNA MAKALA NZURI ULIYOANDIKA NA UNAFIKIRI INAWEZA KUWAAMSHA WATANZANIA TAFADHALI NITUMIE KWENYE amakirita@gmail.com

MAKALA ISIWE IMEWEKWA KWENYE BLOG AU CHOMBO KINGINE CHA HABARI, IWE IMETUMIA KISHWAHILI RAHISI NA KINACHOELEWEKA NA IWE NA MANENO KATI YA 500 NA 1000 KARIBU SANA.