AMKA MTANZANIA imekuwa na utaratibu wa kuwatumia vitabu wasomaji ili kujifunza na kujihamasisha zaidi. Vitabu ambavyo huwa vinatumwa ni vitabu vilivyoandikwa kwa lugha ya kiingereza.
Tokea kuanza kwa zoezi hili kuna watu wamekuwa wakiwasiliana na mimi kunieleza changamoto kubwa inayowazuia kusoma vitabu ninavyotuma. Changamoto hiyo ni lugha ya kiingereza. Hivi majuzi nilikuwa natoa memory kadi zenye AUDIO BOOKS(vitabu vilivyosomwa), watu wengi sana walikuwa wanazihitaji kadi zile ila lilipokuja swala la lugha kuna baadhi walishindwa kuagiza kadi.
Kitu hiki kimekuwa kinaniumiza sana kwa muda mrefu, kwa sababu watu wanania ya kweli ya kujisomea na kujifunza ila lugha inawapa changamoto. Nimekuwa nikifikiria sana ni jinsi gani tunaweza kusaidiana kutatua changamoto hii. Wapo wengi ambao wameomba vitabu hivi nivitafsiri kisha niwapatie, ni wazo zuri lakini kuna changamoto kubwa ya hatimiliki na muda wa kufanya hivyo.
Njia pekee inayoweza kuwasaidia wale wote ambao lugha hii ya kiingereza imekuwa changamoto kwao ni kujifunza kiingereza. Kujifunza kiingereza kutakusaidia katika mambo mengi na sio kujisomea tu. Kama unafanya biashara au unataka kufanya biashara basi huna budi kukijua kiingereza. Hii ni lugha ya kimataifa na ili uweze kufikia anga za kimataifa ni muhimu kuijua lugha hii japo kwa mbali. Tunajisifu kiswahili ndio lugha ya taifa, lakini kiingereza kimekuwa ndio lugha ya mawasiliano katika taasisi mbalimbali nchini kwetu.
Unawezaje kujifunza kiingereza?
Bado nafikiria mfumo mzuri wa kuweza kufundishana yale mambo ya msingi kwenye lugha hii kwa njia ya mtandao. Wakati naendelea kufanya hivi haimaanishi wewe ukae tu na kulalamika kwamba hujui lugha hii, kumbuka kwenye AMKA MTANZANIA huwa hatulalamiki bali tunachukua hatua. Anza kuchukua hatua leo hii na sasa hivi ya kujifunza lugha hii ya kiingereza. Sio kazi ngumu kama unavyofiki, ila inahitaji ufanye mazoezi ndio uweze kuelewa. Ni njia zipi utatumia kujifunza mwenyewe?
1. Kusoma vitabu vyenye tafsiri ya kiswahili na kiingereza.
Kuna baadhi ya vitabu huwa vinakuwa na tafsiri ya lugha hizi mbili, sizungumzii kamusi. Kwa mfano vitabu vya dini, biblia au korani mara nyingi huwa kuna vya kiswahili na vya kiingereza. Kama wewe ni mkristo nunua biblia ya kiswahili na ya kiingereza au kama ukipata moja yenye lugha zote mbili itakuwa vizuri zaidi. Kama wewe ni muisilamu fanya hivyo pia. Baada ya kuwa na vitabu hivi, tenga muda kila siku wa kusoma fungu moja au mafungu kadhaa kwa lugha zote mbili kwa kuanza na kiswahili kisha kwenda kwa kiingereza. Japo kiingereza cha vitabu vya dini ni kigumu, ukianza kufanya hivi utaanza kuona mwanga.
2. Angalia filamu zenye tafsiri ya maneno.
Njia nyingine nzuri ya kujifunza kiingereza ni kuangalia filamu ambazo zina tafsiri ya lugha kwa maandishi. Kwa mfano karibu kila “bongo muvi” ina tafsiri ya maneno ya kiingereza ambayo inaonekana kwenye kioo. Angalia na kusikiliza wanayoongea kisha linganisha na maneno yaliyoandikwa chini. Kuna wakati huwa wanakosea ila kuna vingi bado unaweza kujifunza.
Hata kwa kuangalia filamu ya kiingereza tupu na kulinganisha matendo wanayofanya na maneno wanayozungumza unaweza kujifunza mambo mengi.
3. Fuatilia habari za lugha ya kiingereza.
Anza kufuatilia habari zinazotolewa kwa njia ya kiingereza. Nunua na soma magazeti yanayoandikwa kwa lugha ya kiingereza, sikiliza redio za kiingereza na angalia taarifa za habari zinazosomwa kwa lugha ya kiingereza. Kwa njia hii kuna vitu vingi sana unaweza kujifunza kuhusu lugha hii.
4. Fuatilia maongezi yaliyotafsiriwa.
Kuna maongezi mengi ambayo yametafsiriwa kutoka kiingereza kwenda kiswahili. Kwa mfano huwa kuna mahubiri mbalimbali ambapo mmoja anaongea kiingereza na mwingine anatafsiri kwa kiswahili. Ukifuatilia kwa makini utaweza kujifunza mambo mengi sana kwenye lugha hii ya kiingereza.
5. Tumia mtandao wa intaneti.
Kwenye mtandao wa intaneti kuna sehemu nyingi sana ambazo wanafundisha lugha hii ya kiingereza. Baadhi ya mitandao kama Alison, unaweza kujifunza lugha hii na kuelewa vizuri. Unatakiwa kuwa na ufuatiliaji wa hali ya juu la sivyo unaweza kuachia njiani. Kufungua mtandao huu wa Alison bonyeza maandishi haya. Pia unaweza kutumia huduma ya Google translator, japo nayo haipo makini sana kwenye kutafsiri. Kuingia kwenye google translate bonyeza haya maandishi kisha litakuja boksi ambalo unaandika sentensi ya kiswahili na upande mwingine inatafsiriwa moja kwa moja kwenda kiingereza
6. Jiunge na darasa linalofundisha kiingereza.
Kuna sehemu nyingi sana ambazo wanafundisha kiingereza maarufu kama “English Course”. Kwa kujiunga na programu kama hizi utajifunza lugha hii kwa urahisi sana, na madarasa mengi yanafanyika wakati wa jioni au usiku. Hivyo kama upo karibu na eneo ambalo madarasa haya yanaendeshwa unaweza kujiunga na kujifunza lugha hii ya kiingereza. Kwa walioko Dar es salaam ubalozi wa uingereza kupitia kitengo cha British Councel wanatoa msaada mzuri sana kwa wanaotaka kujifunza lugha hii ya kiingereza. Unaweza kuwatembelea na kujua jinsi ya kujifunza kiingereza kutoka kwao.
7. Fanya mazoezi ya kuongea na kuandika.
Kujifunza lugha hii bila ya kufanya mazoezi ni ndoto. Hata ujifunze kwa njia gani kama hutofanya mazoezi ni vigumu sana kuweza kuijua lugha hii vizuri. Kuanzia sasa weka utaratibu wa kusema au kuandika sentensi moja ya kiingereza kila siku, endelea kuongeza kidogo kigogo kila siku mpaka ufikie uwezo wa kueleza hadithi fupi kwa kiingereza. Tafuta mtu anayeweza na anayependa kuongea lugha hii halafu uwe unafanya nae mazungumzo mara kwa mara. Utaona ujasiri wako unaongezeka na uelewa wako wa lugha hii unakuwa mkubwa zaidi. Wakati unafanya mazoezi usiogope kukosea, utakosea sana na hiyo ndio njia ya kujifunza.
Kwa sasa anza kutekeleza haya machache niliyokushauri, fanya hivyo kila siku. Mimi bado naandaa mpango mzuri wa kufundishana lugha hii kupitia mtandao na ukishakamilika nitawashirikisha.
Naomba nikupe moyo kwamba lugha hii sio ngumu kama wengi tunavyofikiri, hofu kubwa uliyojiwekea kwamba mimi siwezi lugha hii ndio inakuzuia kujifunza nakuielewa. Kama ukiamua kujifunza kwa njia nilizoshauri baada ya muda mfupi utaona mabadiliko makubwa.
Watoto wa miaka mitano wanaozungumza kiingereza baada ya kupelekwa shule za michepuo ya kiingereza sio kwamba wana akili sana ya kushika lugha hii ila ni kwamba wamezoeshwa kuzungumza lugha hii. Naamini hata mtu ambaye hajaenda shule kabisa anajua maana ya maneno “I LOVE YOU, I MISS YOU” na mengine mengi kwa sababu yanatumika mara kwa mara. Hivyo na wewe jifunze lugha hii kwa kuitumia mara kwa mara.
Nimeingia kwenye hiyo Web site ya Alison mkuu, nimekuta michanganuo mingi nimeshindwa kujua nichague njia ipi itakuwa rahisi kwangu kujua kingereza. Naomba nipe njia rahisi mkuu ili niichague mkuu. TUPO PAMOJA.
LikeLike