Mimi huwa nasoma angalau kitabu kimoja kila wiki na wakati mwingine nasoma vitabu viwili au zaidi ndani ya wiki moja. Sitaki kurudia ni faida gani naipata kwenye kusoma vitabu hivi kwa sababu nilishaeleza sana kwenye makala; hivi ndivyo tabia ya kupenda kujisomea ilivyoninufaisha, inawezekana hata kwako pia.

Watu wengi huwa wananiuliza napata wapi muda wa kusoma vitabu vyote hivi? Ukweli ni kwamba nina mambo mengi sana ya kufanya ila nahakikisha katika masaa 24 ya siku sikosi dakika 30 za kujisomea. Nafikiri hata wewe pia unaweza kupata dakika hizi 30 kwenye siku yako kwa sababu unapoteza muda mwingi zaidi ha huu kila siku. Au huenda unapata hizo dakika 30 ila huwezi kusoma hata kurasa tano.

Unawezaje kuzitumia dakika 30 kujisomea?

Kuna mambo mengi sana yakuzingatia kama unataka kusoma vitu vingi ndani ya muda mfupi. Baadhi ya vitu hivyo ni;

1. Muda uliotenga kwa ajili ya kujisomea. Sawa umepanga kujisomea dakika 30 lakini ni muda gani? Kama umepanga kujisomea jioni baada ya kutoka kwenye kazi zako ukiwa umechoka ni vigumu sana kufanikiwa kusoma na kuelewa. Ila ukitenga muda wa asubuhi ndio ukawa unajisomea utaona unaelewa vizuri na kukumbuka zaidi.

2. Mazingira unayosomea. Kama unasomea kwenye mazingira ambayo yana usumbufu mwingi ni vigumu sana kuweza kusoma vizuri na kuelewa. Unapotenga nusu saa hii hakikisha unakuwa kwenye eneo tulivu, tena mbali kabisa na simu. Kama unataka kusoma huku unaangalia TV au kusikiliza redio au unasoma huku unapiga hadithi au unachat itakuwa vigumu sana kwako kupata ule ujumbe uliokusudia kuupata.

3. Aina ya usomaji. Kama bado unasoma kwa mtindo uliofundishwa shule ya msingi utajikuta una mwendo mdogo sana kwenye kusoma. Hii ni kwa sababu akili yako imejifunza kusoma neno moja moja na kulielewa ndio kwenda kwenye neno jingine. Ili uweze kusoma kwa kasi yako ya kusoma inakubidi ubadili mfumo wa kujisomea.

Mfumo wa kusoma kwa kasi na kuelewa zaidi.

Kuna mifumo mingi sana ya kuweza kusoma kwa kasi, kuelewa zaidi na kukumbuka yale uliyoyasoma. Mifumo hii haitofautiani sana kwani yote inakufundisha kubadili muundo wako wa kusoma na kujenga muundo mwingine.

Kwa mfano kwa dakika 30 unazopanga za kusoma unaweza kuwa unasoma ukurasa mmoja kwa dakika moja, hivyo kwa siku unasoma kurasa 30 na kwa wiki unasoma kurasa 210, umeshamaliza kitabu kwa sababu vitabu vingi vina kurasa 200.Hii ndio kasi niliyojifunza mimi kusomea, Wakati mwingine naweza kusoma kwa kasi ya kurasa mbili kwa dakika moja.

Hata wewe unaweza kuongeza kasi yako mpaka kufikia hapo au hata zaidi ya hapo. Watu wengi waliojifunza kuongeza kasi ya kusoma wanaweza kusoma mpaka kurasa 4 au 5 ndani ya dakika moja.

Ni njia zipi unatumia kuongeza kasi yako ya kusoma.

Kuna njia nyingi sana zinazoweza kukusaidia kuongeza kasi ya kusoma. Hapa nitazungumzia chache na nitatoa kitabu ambacho kimeeelezea zaidi.

1. Acha kusoma kwa sauti.

Japo kuwa hutoi sauti unaposoma lakini umejijengea tabia ya kutamka neno kwanza wakati unajisomea, tabia hii inakupunguzia kasi yako ya kujisomea kwa asilimia 50. Huna haja ya kutamka kila neno kwenye akili yako bali unatakiwa kulielewa na kwenda haraka kwenye neno lingine au maneno mengine.

2. Soma sentesi nzima na sio neno kwa neno.

Wakati mwingi huwa tunasoma neno moja halafu unaenda neno jingine hivyo hivyo. Kama unataka kuongeza kasi yako ya kusoma acha mfumo huu wa kusoma neno moja moja, bali soma sentensi nzima au soma kikundi cha maneno kwa mara moja. Hii itakusaidia kwenda haraka unaposoma.

3. Chukua muhtasari au weka alama.

Kama unasoma kitabu kilichochapwa unaweza kuwa unatumia rangi kuweka alama kwenye sehemu ambazo ni muhimu sana kwa kile unachosoma. Pia unaweza kuwa unachukua muhtasari wa baadhi ya vitu muhimu ulivyoelewa kadiri unavyosoma.

4. Tumia kifaa chochote kufuata mstari au sntesi unayosoma.

Kama unasoma vitabu vilviyochapwa unaweza kutumia kidole au hata kalamu kufuata sentensi unayosoma. Hii itakusaidia kuweka msisitizo wako pale unaposoma na kuacha kuangalia maneno mengine ya mbele zaidi auyaliyopita nyuma. Hata kama unasoma kwenye kompyuta au simu fuata na kidole na utaona kasi yako yakusoma inaongezeka.

5. Tafakari kila unapomaliza kusoma.

Usichukulie muda uliojiwekea kusoma kama kifungo kwamba unapoisha unakimbia haraka na kuanza kufanya mambo mengine uliyoacha kusoma. Jipe dakika chache za kutafaari yale uliyoyasoma na kufikiri kidogo zaidi. Hii itakusaidia kuelewa zaidi na pia kukumbuka zaidi. Wengi wetu ukishamaliza kusoma unakimbilia simu au tv au kupiga hadithi, hii inakufanya usahau haraka sana yale uliyojifunza. Hii inaumika pia hata kama unasoma na umetoka kufundishwa, au unafanya kazi na umetoka kwenye mkutano muhimu, tumia dakika chache kutafakari yale uliyofundishwa au uliyosikia.

Zipo njia nyingi sana za wewe kuweza kujifunza kuongeza kasi yako ya kujisomea. Ukianza na hizo chache utajikuta unaongeza kasi yako ya kusoma mara mbili ya unavyosoma sasa hivi. Utaweza kusoma vitabu vingi sana na utapata faida kubwa.

Kitu kimoja cha ziada nachoweza kukusisitiza ni KUWA NA KITABU POPOTE UENDAPO. Usidhubutu kabisa kwenda popote kama huna kitabu ambacho unaweza kujisomea wakati ambao utakuwa unapoteza muda.

ZOEZI LA WIKI.

Wiki hii tutafanya zoezi la kujifunza kuongeza kasi ya kusoma. Ili kupata mwanga zaidi nakupa kitabu kinachoitwa The Speed Reading Course, kitabu hiki kimeelezea mbinu za kuweza kuongeza kasi yako ya kusoma. Kukipata bonyeza maandishi hayo ya kitabu.

Kitabu hiki kina kurasa 40 tu hivyo kama ukiweza kusoma kwa kurasa moja kwa dakika moja itakuchukua dakika 40 tu. Nakushauri ukisome na kukirudia kama mara tatu ili uweze kuelewa kila kilichoandikwa.

Baada ya kusoma na kuelewa kitabu hiki, rudia mbinu ulizojifunza kusoma baadhi ya vitabu ambavyo nilishakutumia lakini bado hujaweza kuvisoma. Nina uhakika kuna vitabu vingi nimekutumia ila bado hujavigusa, huu ndio wakati muafaka wa kuvisoma.

Baada ya kusoma kitabu hiko tunaweza kushirikishana yale tuliyoelewa kwenye FORUM-MAJADILIANO ili tuweze kujadiliana zaidi.

Nakutakia kila la kheri katika yote unayofanya ili kuboresha maisha yako,

TUKO PAMOJA,