Hivi umeshawahi kujiuliza au kuona baadhi ya watu, wakiwa na fedha nyingi sana na wakiendelea kupata nyingine zaidi, na huku wengine wakiishia kupata riziki ya jioni tu na huku wakijitahidi sana kutafuta bila ya mafanikio?
 

Na vilevile bila shaka umeshawahi kuwaona baadhi ya watu, wakimudu kununua kila wakitakacho, wakati wengine wakiwa wanajaza  madeni kila mahali pamoja na kwamba, wana ajira au shughuli zenye kuwaletea kipato kila siku katika maisha yao.
Umeshawahi tena kujiuliza nini hasa kinacho sababisha hali hii ya maisha iwe tofauti sana katika maisha yetu wakati ukweli ni kwamba kila mtu anaweza kufanikiwa. Kumbuka kwamba, kwa sehemu kubwa watu hao, kila mmoja amechagua njia ya maisha anayoitaka na ndiyo iliyomfikisha hapo alipo mpaka sasa.  
Nakumbuka kuna wakati nilitaka kupigwa mgahawani baada ya kusema kwamba mtu kushindwa kupata pesa ni uchaguzi wake mwenyewe. Wale watu waliokuwepo siku ile walinipinga sana “aaah kwa sababu wewe unazo bwana”. Lakini bado naamini mpaka leo nilichokisema kipo sahihi ingawa waliotaka kunipiga hawakujua nilichokuwa nikimaanisha na kauli ile.
Kwa kusoma sana, kupitia tafiti mbalimbali za mafanikio na kuzungumza na wale waliofanikiwa zaidi yangu kifedha nimejifunza kitu kimoja muhimu sana katika maisha yangu ambacho na wewe ni muhimu kukijua ili ufanikiwe na uvuke pale ulipo. Kitu hiki ndicho kimewafanya watu hawa wawe juu na kujikuta kuwa ni watu wa mafanikio huku wengine wakilia shida tu kila siku.
Kitu pekee na cha muhimu nilichojifunza ni kwamba, watu hawa wana sifa ya kuwa na mitizamo chanya kuhusiana na pesa. Ni watu wanaopata fedha kwa sababu, siku zote wanaamini kwamba watapata fedha. Huu ndio mtazamo sahihi ambao tunatakiwa kuwa nao ili kusonga mbele zaidi ya pale tulipo na kama una mtazamo huu  kuhusu pesa, tayari wewe ni tajiri. 
Kwa sababu ya kuamini kwao hivyo, na kuwa na mtazamo chanya kuhusu pesa mara zote matokeo yake yamekuwa ni kuvuta fedha kuja upande wao. Wamekuwa wakivuta nafasi au uwezekano wa kutengeneza fedha kwenda upande wao na kuweza kuweka akiba fedha hizo na hatimaye fedha hizo zimeweza kuwasaidia na kuwafikisha pale walipo leo. 
Lakini watu hawa hawakuanza wakiwa na fedha nyingi kama unavyofikiri, ila wengi wao walianza polepole kwa kuzalisha na kuingiza fedha hizo, kitu pekee walichokuwa nacho na ambacho kimewasaidia sana kuwasogeza mbele ni kuwa na mtazamo chanya kuhusu pesa na kufatilia malengo na mipango yao waliyojiwekea kila siku.
Ukiamini kwamba, unaweza na utamudu kutengeneza pesa na hatimaye kuwa tajiri, ni kitu ambacho kinawezekana na utamudu kuwa tajiri kweli. Kuamini huku ni lazima kuambatane na kujua kwamba , wewe kama binadamu unayo haki ya kupata fedha na kutengeneza utajiri wa kutosha katika maisha yako kama utaamua.
Kumbuka kwa kuweka mawazo yetu upande wa kushinda, tutatengeneza mazingira ya kushinda pia. Naomba nikwambie ukweli huu kama ukiamini moyoni kwamba, kuwa na fedha na kutengeneza fedha ni haki yako ambayo unastahili na siyo suala geni au la ajabu, ni lazima utapata fedha na kuwa tajiri, kitu cha msingi kabisa jifunze kuchukua hatua zaidi kwa vitendo na sio kukaa tu hutafika mbali sana utaishia kupiga kelele na kulaumu.
Kufanikisha safari hii ya kuelekea kwenye utajiri ni lazima kwanza utazame sana mahali ulipo hivi sasa. Baada ya kufanya hivyo unatakiwa kubuni mpango halisi wa miezi mitatu, sita, mwaka au hata miaka mitano ijayo. Ni hatari sana kwa mtu ambaye, hana shughuli maalum kutarajia kupata mamilioni ya fedha kwa kipindi kisichozidi miezi sita au mwaka. Hiyo itakuwa ni sawa na ndoto ya mchana. 
Watu wengi huwa wanajiambia hivi, ‘sijui nitapata vipi fedha’, au ‘Ni vigumu sana kupata fedha’ ama ‘niko kwenye madeni, sijui nitatoka vipi.’Kitu ambacho wengi hawakijui kila penye tatizo pana suluhu, vinginevyo kusingekuwa na matatizo. Lakini, wengi kutokana na mitizamo hasi tuliyonayo hatutaki suluhu tunang’ang’ania tatizo.
Pale ambapo tuna shida ya fedha, tunahitaji kupata fedha, ni lazima tuyaambie mawazo yetu ya kina kwamba, tunataka fedha. Tusipeleke nguvu yetu ya kufikiri kwenye kukosa fedha, bali kwenye namna ya kupata pesa zaidi. Mara nyingi wengi huwa tunakaa kutwa nzima tukiwaza na kuumizwa na kukosa fedha, siyo kupata fedha.
Jifunze zaidi kuipanga mipango yako vizuri, ifatilie na kisha jenga mtazamo chanya juu ya fedha utaipata kweli na kuwa tajiri, acha kulalamika na kuwa na tabia za ajabu za kutaka uanze biashara leo na utajirike leo, hautafika mbali. Huwa nashangaa sana unapomwambia mtu aanzishe mradi leo ili aje afaidi baada ya miaka 20 kutoka sasa, atacheka hadi mbavu zitamuuma. Anataka leo leo hata kama ni kwa muujiza.
Kwenye kutafuta mafanikio tunatakiwa tuwe na subira kuvuna mavuno sahihi na tuachane na haraka zisizo na maana, maisha yako hayaendeshwi kwa muujiza au bahati ni mipango na malengo sahihi. Kikubwa zingatia unachokitafuta na ng’ang’ania mpaka malengo yako yatimie.
Napenda kukumbusha tena unastahili kuwa tajiri, kila kitu unacho cha kukufanikisha, jenga tu mtazamo sahihi kuhusu fedha utafanikiwa na acha kulalamikia mtaji wala nini, una utajiri mkubwa unaomiliki kupitia wewe bila kujijua, chukua hatua muhimu juu ya maisha yako.
Nakutakia ushindi katika safari yako ya mafanikio, chukua hatua, wajibika na endelea kutembelea mtandao huu wa AMKA MTANZANIA kwa kujifunza zaidi na zaidi.
DAIMA TUKO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE.
IMANI NGWANGWALU – 0767048035/ingwangwalu@gmail.com