Karibu tena msomaji wa KISIMA CHA MAARIFA, tunaendelea na uchambuzi wa kitabu THE RICHEST MAN BABYLON.

Kwenye makala iliyopita tuliona jinsi Bansir na Kobbi walivyoyatafakari maisha yao na kuona kuna tatizo kubwa. Na hivyo waliamua kumtafuta mtu tajiri na kujifunza kwa sababu waliamini matajiri wana siri inayowafanya waendelee kuwa matajiri.

Mtu tajiri kuliko wote babeli.

Katika zama za babeli aliishi mtu mmoja tajiri sana aliyejulikana kwa jina la Arkad. Alijulikana kila kona ya babeli kwa utajiri wake uliotukuka.

Alinunua na kumiliki vitu vya thamani, alitoa msaada kwa wasiojiweza na pia alitoa sadaka na aliijali familia yake sana. Pamoja na yote hayo utajiri wake uliendelea kukua kila mwaka.

Siku moja rafiki wake wa utotoni alimfuata akamwambia wewe Arkad umebahatika kuwa mtu tajiri sana. Umekuwa mtu tajiri kuliko wote babeli wakati sisi wenzako tunateseka na maisha. Tulicheza wote pamoja na hukuwa na tofauti sana. Tulifundishwa na mwalimu mmoja na hukuonesha uwezo mkubwa kuliko sisi. Hata tulipoanza kufanya kazi hukufanya kazi kwa nguvu zaidi kuliko sisi. Sasa ni kitu gani kimekufanya wewe uwe tajiri sana wakati sisi wenzako tunateseka na maisha?

Arkad alimjibu kwa kusema, kama kuanzia ujana wako mpaka sasa hujaweza kutengeneza fedha zaidi ya fedha ya kula basi unaweka kuwa na matatizo haya mawili. Labda umeshindwa kujifunza sheria za fedha na utajiri au huzifuati sheria hizo. Alimwambia kufikiria bahati ndio inaleta utajiri ndio kitu ambacho kinawakwamisha watu wengi sana kufikia utajiri. Alimwambia pia watu ambao wanapata fedha ambazo hawajazitarajia huishia kuzitumia hovyo na kurudi kwenye hali yao ya umasikini. Alitoa mfano wa watu wanaopata urithi mkubwa ila baada ya muda mfupi wanajikuta wamerudi kwenye umasikini wao. Alisema yote hayo ni kutokana na kutokuzijua sheria za fedha.

Arkad aliendelea kusema kwamba katika ujana wake alijiangalia na kuona anao uwezo wa kutengeneza utajiri. Alitambua kwamba utajiri ni nguvu, na kwa kuwa na utajiri mambo mengi yanawezekana. Kwa kuwa na utajiri unaweza kuwa na nyumba nzuri, kununua vitu vya thamani, kusaidia wengine na hata kutoa sadaka. Anasema baada ya kugundua hayo aliamua kwamba lazima na yeye awe tajiri na hataishia kuwa mtazamaji tu wa watu wengine ambao ni matajiri. Aliamua kutoridhika na maisha ya umasikini na hivyo kuchukua hatua ya kuelekea kwenye utajiri.

Arkad anasema kwa kuwa alitokea familia ya kimasikini, hakuona uwezekano wowote wa kurithi mali na hivyo alitambua kwamba ili kufikia lengo lake alihitaji vitu viwili muhimu; muda na kujifunza. Alisema muda kila mtu anao wa kutosha kwa sababu wote tumepewa muda sawa, ila bado wengi hawawezi kuutumia vizuri. Na kujifunza alisema mwalimu wao aliwafundisha kujifunza kwa aina mbili; kujifunza vitu unavyovijua na kuelewa na kupata mafunzo ya kujua vitu ambavyo huvijui.

Hivyo Arkad aliamua kujifunza ni jinsi gani watu wanaweza kutengeneza utajiri na kufanya hilo kuwa jukumu lake na hivyo kulifanya vizuri. Arkad alipata kazi kama mwandishi kwenye nyumba ya kumbukumbu, na kila siku kwa masaa mengi alikuwa anawaandikia watu kumbukumbu zao. Alifanya kazi kwa juhidi sana na miezi kwa miezi hakuona mabadiliko makubwa kwenye maisha yake zaidi ya kupata hela ya kula na matumizi tu. Pamoja na hayo lengo lake la kuwa tajiri halikumtoka.

Siku moja Algamish, mkopeshaji wa fedha alikuja kwa Arkad na alitaka kuandikiwa sheria ya tisa. Alimwambia Arkad nataka sheria hii ndani ya siku mbili na nitakulipa shaba mbili. (Thamani ya pesa kipindi cha babeli ilipimwa kwa madini, shekeli ndio ilikuwa ndogo, ikifuatiwa na kopa(copper), fedha(silver) na dhahabu(gold)). Arkad alifanya kazi kwa nguvu sana lakini sheria ile ilikuwa ndefu. Algamish alirudi siku ya pili na kukuta bado Arkad hajamaliza huandika sheria ile. Alikasirishwa sana, lakini Arkad hakuogopa na alimwambia “Algamish wewe ni mtu tajiri, niambie na mimi nawezaje kuwa tajiri na nitakesha usiku mzima kukamilisha sheria hii”. Algamish alikubaliana nae na akamwambia akamilishe sheria hiyo na kesho yake angemweleza siri ya utajiri.

Arkad alifanya kazi usiku kucha kuandika sheria ile, mgongo ulimuuma na mpaka alishindwa kuona vizuri. Mpaka kufika asubuhi alikuwa amekamilisha sheria ile na Algamish alipofika alimwambia nimeshakamilisha sasa tekeleza ahadi yako. Algamish alimwambia umekamilisha wajibu wako na nitakuambia vyote unavyotaka kujua kwa sababu nimeshakuwa mzee sasa, na wazee wanapenda kutoa ushauri. Alimwambia wazee wana ushauri mzuri sana ila vijana huamini kwamba ushauri wa wazee ni wa zamani na hauendani na wakati wa sasa. Alimwambia jua linachomoza mashariki na kutua magharibi kuanzia enzi za mababu na litaendelea hivyo mpaka vitukuu vyako watakapokuwa wazee. Hivyo mambo hayabadiliki sana na wazee wameona mengi.

Algamish aliendelea kusema mawazo ya ujana ni sawa na mwanga wa kimondo ambao unapita mara moja ila buasara za wazee ni sawa na nyota inayoonekana kila siku na wasafiri wanaitegemea. Aliendelea kumuambia yashike maneno yangu vizuri sana la sivyo kazi yote yako ya usiku itakuwa bure na umepoteza muda wako.

Tutajifunza kile Arkad alichoambiwa kwenye makala ijayo.

Tunajifunza nini hapa?

1. Watu matajiri sio kwamba wana bahati kuliko watu wengine na sio kwamba wana akili sana au wanafanya kazi sana bali wanajua sheria ya fedha ambayo imewafanya kuwa matajiri.

2. Watu wanaotegemea bahati kuwa matajiri huishia kufa masikini, pia watu wanaopata fedha ambazo hawajazifanyia kazi huishia kuzitumia hovyo.

3. Unaweza kuwa unafanya kazi kwa juhudi sana ila kama huna maarifa na elimu ya sheria za fedha utaendelea kuwa masikini.

4. Wazee wana hazina kubwa ya kujifunza, wamepitia mengi ambayo unaweza kujifunza ili kuyafanya au kutorudia makosa.

Nakutakia kila la kheri katika safari yako ya kufikia mafanikio makubwa.

TUKO PAMOJA, TUTAKUTANA KILELENI.