Hivi Ndivyo Unavyoweza Kuzuia Watu Wanaokwamisha Na Kuingilia Maisha Yako Kila Mara.

Kila mmoja wetu anakutana na watu wakorofi katika maisha yake, ambapo watu hawa huwa wakiingilia maisha yetu kwa namna moja au nyingine. Hivyo, karibu kila mmoja anajua jinsi inavyokuwa vigumu kushughulika na watu wa aina hii katika maisha.Watu wakorofi tunawafahamu vizuri, kiasi kwamba hatuhitaji fasili yake sana ili kuwatambua na kuwajua zaidi.

Watu hawa wakorofi mara nyingi wanaweza kuwa ndugu, jamaa, jirani au rafiki zetu. Wanaweza kuwa wenzetu kwenye shughuli zetu au hata wageni tunaokutana nao kwa muda mfupi tu. Watu hawa mara wanapoingilia maisha yetu kuna wakati huweza kutuvuruga au kutunyima amani kabisa, na pengine kutufanya tushindwe kufanikiwa kwenye malengo na mipango yetu tuliyojiwekea.
Kila mmoja wetu anatamani sana kujua namna ambavyo anaweza kukabiliana au kuishi na watu wanaoingilia maisha ya watu wengine. Kwa hali hiyo, nimeona nikusaidie katika hilo. Ningependa kwa muhtasari tu, ujue namna ya kukabiliana au kuishi na watu hawa wakorofi. Njia pekee unayoweza kuitumia kukabiliana na watu wakorofi ni mipaka.( Soma pia Wajue watu hawa na waepuke kwenye maisha yako
Ni lazima kama binadamu uwe na mipaka yako. Jiwekee mipaka kwenye mambo yako, ambapo mtu anapoivuka na kuonyesha kutojali, utapaswa kusema au kumwambia ili aelewe vizuri. Kuna wakati tunaweza kuwa na ndugu au jamaa ambao wanaingilia sana mipaka yetu kimaisha, kama kwamba, sisi hatutakiwi kukamilika. Kwa sababu ni ndugu zetu au wazazi wetu, wanashindwa kujua kuwa kuna mipaka katika uhusiano wetu. Hili hutuumiza wengi.

Mipaka yako unaipanga au kuiweka mwenyewe na kama ni lazima, inabidi ndugu, jamaa au wazazi au marafiki waijue. Hata usipowaambia, wataijua kwa sababu, ikivukwa itabidi uwaambie. Mipaka ni yale maeneo ambayo unajiambia kwamba , hutaki yaguswe na mtu mwingine katika maisha yako.
Kuna haja ya kujua kwamba, uhusiano wowote ambao unakutesa au unakuletea matatizo ya aina yoyote, hauna maana sana kwako. Kama ni mtu au ni watu unaohusiana nao ndiyo chanzo cha matatizo, huna haja ya kuwavumilia, kwa sababu tu ni ndugu, wazazi au jamaa. Wanapaswa kujua kile ambacho hukipendelei, ambayo ndiyo mipaka yako.
Kuna wakati,  unaweza ukajikuta hata baada ya kuonesha na kusema kuhusu mipaka yako, bado utakuta kuna mtu au watu wengine wataendelea kukuingilia na kukusumbua katika maisha yako. Kama hali hii ikiendelea kwa muda mrefu una haja ya kuwaepuka watu hawa au kuvunja uhusiano kabisa kama itawezekana. Tambua ukweli huu,  Wanaokuzunguka wanamchango mkubwa kwenye maisha yako pia, usipokuwa makini watakukwamisha.
Kumbuka usalama wako na amani yako, ni muhimu sana katika safari ya mafanikio uliyonayo.  Unaposhindwa kuweka mipaka, watu wanaweza kukuchukulia kama mtu ambaye ni rahisi, asiye na lake jambo, anayeweza kuchezewa na kukubali. Kwa hiyo, unapobadilika ghafla na kuanza kuweka mipaka, ni lazima watashangaa na kushtuka. Hivyo, usishangazwe na kushangaa kwao.
Usijali wanasema nini kuhusu kubadilika kwako. Wanaweza kusema, umeshikwa na mke au mumeo, wanaweza kusema unaringia pesa ulizonazo  au kingine chochote wanachoweza kusema. Hilo lisikutishe wala usijali sana, kwani hawajawahi kukuona ukiwa na mipaka, hivyo wamepatwa na mshtuko.
Imarisha mipaka hiyo bila kujali. Kuna njia nyingi za kuimarisha mipaka, lakini mojawapo muhimu ni kumwambia mtu kwamba, hungependa hiki na kile kifanywe , kwa sababu unadhani ni kuingilia mambo yako. Ukiweza kufanya hivyo utaweza kuishi maisha safi na yenye amani. Hivyo ndivyo unavyoweza kuzuia watu wanaokwamisha na kuingilia maisha yako kila mara.
Nakutakia mafanikio mema na endelea kutembelea AMKA MTANZANIA, kwa kujifunza zaidi na kuhamasika, karibu sana. 
DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE.
IMANI NGWANGWALU – 0767048035/ingwangwalu@gmail.com

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

Create a website or blog at WordPress.com

Up ↑

%d bloggers like this: