Habari za leo mpenzi msomaji wa AMKA MTANZANIA, karibu tena kwenye kipengele hiki cha ushauri wa changamoto mbalimbali zinazotuzuia kufikia mafanikio. Kwa wiki chache zilizopita kulikuwa na makala ya ushauri kwa wanafunzi wanaoanza chuo kikuu pia tumewahi kuweka makala za ushauri kwa wahitimu wa vyuo vikuu. Leo tutatoa ushauri mwingine kwa wanafunzi wanaoendelea na masomo yao ya vyuo vikuu na vyuo vingine vya elimu ya juu.

Kabla ya kuingia kwenye ushauri huo kwanza tupate maoni ya msomaji mwenzetu;

Habari za kazi , nina kupongeza kwa makala nzuri na za kuelemisha , nina ombi moja kwako utoe makala ya biashara gani au ujasiriamali gani mwanafunzi wa chuo Kikuu anaweza kufanya huku anaendelea kusoma ?

Hayo ndio yalikuwa maoni ya msomaji mwenzetu aliyetaka kujua ni biashara gani au ujasiriamali gani mwanafunzi wa chuo anaweza kufanya.

Kuna maswali matatu muhimu ya kujiuliza katika swala hili;

Swali la kwanza, je inawezekana kufanya biashara au ujasiriamali ukiwa mwanafunzi wa chuo?

Kwa kuwa mimi ni mmoja wa watu ambao naamini hakuna kinachoshindikana ikiwa mtu atakuwa na nia ya dhati, jibu ni ndio, inawezekana. Japokuwa inawezekana sio rahisi, inahitaji kujitoa kweli na kujituma katika sehemu zote mbili, masomo na biashara.

Swali la pili, je mwanafunzi wa chuo kikuu ana muda wa kutosha kufanya masomo na biashara pia?

Kabla ya kusema ndio au hapana tuangalie kwanza muda uliopo. Kwa Tanzania vyuo vina mihula miwili na kila mhula una siku 120 au 140 kwa wenye mihula mirefu. Hivyo kwa mihula miwili ni siku karibu 300 na hivyo mwanafunzi anabaki na miezi miwili kwa mwaka ambayo hana masomo kabisa. Tukija kwenye muda wa siku, katika masaa 24, darasani anatumia masaa yasiyozidi 8, kulala yasiyozidi 8, kujisomea mwenyewe hayazidi 4 na kupumzika masaa 2. Jumla hapo ni masaa 22 na hivyo kubaki na masaa 2 kwa siku. Hapo bado hatujahesabu siku za mwisho wa wiki ambapo mwananfunzi anaweza kupata masaa zaidi ya 5.

Hivyo basi muda upo na mwanafunzi anaweza kupata masaa yasiyopungua mawili kila siku ya wiki na yasiyopungua matano kila siku ya mwisho wa wiki. Masaa haya yasiyopungua 20 kwa wiki yanamtosha kuwekeza kwenye biashara bila ya kuathiri masomo yake.

Swali la tatu; ni biashara gani anazoweza kufanya mwanafunzi wa chuo kikuu?

Baada ya kuona kwamba inawezekana kufanya biashara huku unasoma na baada ya kuona unaweza kupata muda wa kutosha kufanya biashara na kusoma pia swali la msingi ni je ufanye biashara gani?

Kuna biashara nyingi sana unazoweza kufanya kulingana na kile unachopenda wewe na hata vipaji vyako. Kwa kifupi nikushirikishe baadhi ya biashara ambazo mwanafunzi wa chuo kikuu anaweza kufanya kwa muda huo alionao.

1. Biashara ya mtandao(network marketing).

Hii ni biashara ambayo mwanafunzi anaweza kuifanya kwa muda mchache kila siku au kila wiki na baada ya mwaka au miaka miwili akawa ametengeneza mafanikio makubwa. Hii ni biashara ambayo unatengeneza mtandao wa watumiaji wa bidhaa au huduma na hivyo wanaponunua biashaa au huduma hiyo wewe unalipwa kamisheni. Kuna makampuni mengi yanafanya biashara hii kwa hapa kwetu Tanzania, zifuatilie vizuri kampuni hizi na chagua ni ipi unayoweza kuingia na kufanya biashara. Mbali tu na kufanya biashara pia utajifunza biashara katika ulimwengu halisi.

ANGALIZO; Ukiwauliza watu kuhusu biashara hii watakukatisha tamaa sana kwa sababu wengi wa waliofanya biashara hizi wameshindwa kwa sababu mbalimbali, wewe unaweza kama ukiamua.

2. Ujasiriamali wa taarifa(information entrepreneur).

Hii ni biashara ambayo unatoa taarifa mbalimbali ambazo zinaweza kuwasaidia watu na hatimaye wakawa tayari kukulipa au ukafaidika kwa njia nyingine. Kuanza biashara hii unachagua ni aina gani ya taarifa ambazo unapenda kufuatilia au kutoa kisha unaanzisha blog ambayo utakuwa unatoa taarifa hizo. Ukitoa taarifa nzuri utapata watembeleaji wengi na hatimaye unaweza kuwauzia bidhaa au huduma nyingine au kuuza nafasi za matangazo kwenye blog yako hiyo na ukapata kipato kizuri.

Kujifunza jinsi ya kuanzisha blog na kufanya biashara hii pata kitabu; Jinsi ya kutengeneza fedha kwenye mtandao kwa kutumia blog.

3. Endeleza vipaji vyako.

Kila mmoja wetu ana vipaji au vitu fulani anavyopendelea kufanya. Unaweza kutumia muda huu wa chuo kuendeleza vipaji vyako na kuangalia ni jinsi gani unaweza kuwafanya watu wakulipe kupitia kipaji chako, Unaweza kuwa na kipaji cha kuimba, kuigiza, mitindo, kuandika na kadhalika. Weka muda maalumu wa kuendeleza kipaji chako kila siku. Kwa mfano kwa wanaopenda kuandika nashauri utenge saa moja kila siku kwa ajili ya kuandika tu, kwa njia hii utaboresha uandishi wako.

4. Fanya biashara inayohusiana na TEHAMA

Teknolojia ya habari na mawasiliano(IT & ICT) bado inakua kwa kasi sana. Kama unapenda kutumia kompyuta au mtandao unaweza kufanya biashara nzuri sana inayohusisha IT. Unaweza kujifunza vitu kama kutengeneza picha(graphic design), kutengeneza website, kutengeneza program za kompyuta na hata za simu(mobile app). Ukishajua kutengeneza vitu hivi na ukawa mbunifu unaweza kutengeneza biashara nzuri na kubwa sana.

5. Uchuuzi wa kawaida.

Unaweza pia kufanya biashara nyingine ndogo ndogo kwa maeneo ya chuoni au unakoishi. Angalia ni bishaa au huduma gani wanafunzi wanazihitaji ila wanazikosa au hawazipati kwa kiwango kizuri kisha ingia kwenye biashara hiyo na toa huduma nzuri sana. Utatengeneza biashara nzuri na yenye faida.

Mtaji wa kuanzia unatoa wapi?

Hili ni swali ambalo baadhi wameshajiona kwamba hawawezi kufanya biashara hizo kwa sababu hawana mtaji. Biashara zote nilizozungumzia hapo zinaanza na mtaji kidogo sana na nyingine kama ujasiriamali wa taarifa unaweza kuanza bila hata ya mtaji ni wewe na kopmyuta yako tu. Lakini zile zinazohusisha mtaji kidogo unaweza kuupata kama ukifuata ushauri niliotoa kwa wanafunzi wanaoanza chuo kikuu.

Hizo ndizo baadhi ya biashara ambazo mwanafunzi wa chuo kikuu anaweza kufanya. Kumbuka sio biashara hizo tu ndio zinawezekana, bali hizo ni chache ambazo nina uhakika zinawezekana. Hivyo kama una wazo lako jingine la biashara bado unaweza kulifanyia kazi.

Pia biashara hizo sio rahisi, ila kama umedhamiria kweli na ukajituma kweli inawezekana.

Na utakapoanza maisha hayo ya kusoma na kufanya biashara kuna vitu unatakiwa uache, baadhi ni, kuangalia tv, movie, mipira, kuperuzi mitandao muda wote  n.k

ZIADA; Ushauri niliotoa hapa hauwezi kuwa sawa kwa kila mtu na wewe kama mwanafunzi wa chuo kikuu unaweza kuangalia ni kipi kinaweza kufanya kazi kwako na kisha kukibopresha zaisi kulingana na mazingira uliyopo. Kama unaendelea kupata shida kujua ni biashara gani unaweza kufanya katika mazingira uliyopo tafadhali wasiliana nami kwa email amakirita@gmail.co au 0717396253.

Nakutakia kila la kheri katika mafanikio ya masomo yako na biashara yako.

TUPO PAMOJA.

Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja makala zijazo kila siku ya jumatatu. Kama unahitaji ushauri wa haraka wasiliana na mimi kwa kwa email amakirita@gmail.com au simu 0717396253/0755953887.

kitabu-kava-tangazo432