Wengi wetu tumekuwa ni watu wa kutafuta pesa usiku na mchana ili ziweze kutusaidia kutimiza malengo na mipango yetu tuliyojiwekea. Kutokana na umuhimu wa pesa, kila mmoja wetu kwa sehemu yake amekuwa akijitahidi kufanya chochote kile, ikiwa ni pamoja na kuwekeza ili kuongeza kipato ambacho kitamtoa pale alipo na kumfikisha sehemu nyingine hata kuwa tajiri. 
 

Pamoja na wengi wetu kufanya harakati hizo zakutafuta pesa ili tuweze kuwa matajiri, lakini wengi tumekuwa tukijikuta ni watu wa kutofikia malengo hasa yale tunayoyataka yawe katika maisha yetu. Pesa tunayoipata wakati mwingine, inakuwa kama haikai mikononi mwetu au haitusaidii kufikia malengo yetu.(Soma Pia Hiki Ndicho Kitu Kinachosababisha Pesa Unayotafuta Isikae Mkononi Mwako)
Kitu pekee ambacho wengi hawakijui kinachosababisha malengo yako yasitimie, ni makosa ambayo umekuwa ukiyafanya mara kwa mara wakati unapokuwa na pesa. Wengi wengi tumekuwa tukijikuta ni watu wa kufanya makosa haya sana wakati tuna pesa, ambayo yamekuwa yakituzuia kufikia malengo yetu na kuturudisha nyuma siku hadi siku.
Ili uweze kuwa huru kifedha na hatimaye kuwa tajiri, ni muhimu kwako kuyajua makosa haya ambayo hutakiwi tena kuyafanya katika maisha yako ili uweze kufanikiwa zaidi. Kwa kadiri utakavyoweza kuepuka makosa haya, ndivyo utajikuta ambavyo ndoto zako zinazidi kutumia na kuwa za kweli. Unataka kuwa tajiri kweli katika maisha yako, acha kufanya makosa haya.
Haya ndiyo makosa ambayo hutakiwi kufanya unapokuwa na pesa:-
1. Acha kutumia kiasi kikubwa cha pesa kuliko ya kile unachokipata.
Watu wengi wanapata shida katika maisha yao kwa sababu ya kufanya kosa hili la kutumia kiasi kikubwa cha pesa kuliko ya kile wanachokipata. Unapotumia pesa nyingi kuliko ya zile unazozipata, mwisho utajikuta wewe ni mtu wa madeni na unakuwa unashindwa hata kuweka akiba ambayo inaweza kukusaidia kuwekeza katika miradi yako hapo baadae. 
Kama una malengo na mipango imara ya kuwa tajiri katika maisha yako, hakikisha kuanzia sasa, unaepuka kuishi juu ya kipato chako na mafanikio utayaona. Utaweza kufanikisha hili kama utajiwekea bajeti yako vizuri na kuisimamia. Acha maisha ya tamaa ambayo yatakuingiza kwenye matumizi yasiyo lazima, na mwisho utajikuta unatumia pesa hovyo kuzidi kipato chako.
 

2. Acha kufanya kosa la kutojilipa wewe mwenyewe kwanza.
Mara nyingi tumekuwa tukilisema hili mara kwa mara katika mtandao huu wa AMKA MTANZANIA, ili uweze kufanikiwa na kuona ndoto zako zinatimia, unalazimika kujilipa wewe kwanza kwa kile unachokipata. Ni muhimu kujilipa, kwa sababu wewe ndiye mtu wa kwanza ambaye umekuwa ukiifanyia kazi hiyo pesa uliyoipata.
Wengi wetu tumekuwa tukifanya kosa hili mara kwa mara kwa kutumia kiasi chote cha pesa tunachopata na kusahau kujilipa. Kama unaishi maisha haya ya kutojilipa, sahau kuwa tajiri katika maisha yako. Hivyo, unapopata pesa hakikisha unatenga asilimia kumi ambayo ni malipo yako kwanza. Kumbuka unawalipa watu wote kasoro huyu mmoja wamuhimu ambaye ni wewe.
3. Acha kuishi maisha ya kutegemea chanzo kimoja cha kipato.
Wengi tunaishi maisha ya kutegemea chanzo kimoja tu cha kipato na wakati mwingine huwa ni watu wa furaha hiyo yote kuonyesha tunakubaliana na kile tunachokipata. Kama kweli unataka kuwa tajiri katika maisha yako, unalazimika kutengeneza vyanzo vingi vya fedha ambavyo vitakusaidia hata pale mambo yako yanapokwenda vibaya.
Unapokuwa na pesa acha kufanya kosa la kutokuwekeza. Jifunze, kuwekeza zaidi na zaidi kwani utakuwa unapanda mbegu ambayo utakuja kuivuna katika maisha yako baadae na hatimaye utajenga nguvu ya kukufanya kuwa tajiri kutokana na miradi ambayo umejiwekea.(Soma pia Hivi Ndivyo Unavyoweza Kutengeneza Pesa Zako Na Kuwa Tajiri)
4. Acha kununua vitu visivyo vya lazima kwako.
Ili tuweze kufanikiwa na kusonga mbele katika maisha yetu, ni muhimu kujenga tabia ya kununua vitu vile tunavyovihitaji ambavyo ni lazima kwa matumizi na si vinginevyo. Acha kununua vitu kwa sababu ya tamaa ya macho au kwa sababu umeona jirani yako amenunua kitu Fulani nawe unataka kununua. 
Kama unaishi maisha haya ya kuangalia Fulani kafanya nini, utashindwa kusonga mbele. Ishi maisha yako wewe kama wewe, tengeneza bajeti yako itakayokuongoza kwa siku, wiki au hata mwezi kisha uifate. Acha kufata mkumbo kimbia mbio zako mwenyewe hiyo itakusaidia hautaweza kupoteza pesa nyingi.
5. Acha kuishi maisha ya kutokuwa na mipango endelevu.
Hakikisha una mipango imara ambayo ipo mikononi mwako na itakufikisha kwenye uhuru wa kifedha unaoutaka. Pesa hizo ulizonazo hata kama unaona ni kidogo zipangilie vizuri, zitakusogeza hapo ulipo na kukupeleka sehemu nyingine ambayo hukutarajia hapo mwanzoni. Kama unaona pesa zako hazitoshi, jifunze kutunza pesa zako kidogo kidogo mpaka ziwe nyingi.
Acha kuzitumia pesa zako hovyo kwa kuzidharau eti ni kidogo, hapo utakuwa unakosea. Kumbuka kila pesa yoyote ile iliyopo mikononi mwako, ina thamani kubwa sana kuliko unavyofikiri. Unaweza ukaanza kuishi maisha yako ya kuwa na mipango endelevu leo na sio kesho kama ambavyo umekuwa ukiahirisha mara kwa mara.(Soma Hivi Ndivyo Unavyoweza Kutajirika Kwa Kuanza Na Shilingi Elfu Moja )
Kama unataka kuwa tajiri katika maisha yako, naomba nikwambie ukweli huu tena, acha kufanya makosa haya unapokuwa na pesa. Katika maisha hakuna njia rahisi, hakuna njia ya mkato zaidi ya kupambana na kujitoa mhanga kwa kila hali na kukubali kukabiliana na changamoto unazokutana nazo na kuzishinda. Kwa kila nafasi unayopata unapokuwa na pesa itumie vizuri utajiri utakuwa ni wako.
Nakutakia mafanikio mema katika safari yako ya uhuru wa kifedha, endelea kutembelea mtandao huu wa AMKAMTANZANIA na KISIMA CHA MAARIFAkwa kujifunza na kuhamasika.
TUKO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE.
IMANI NGWANGWALU – 0713048035/ingwangwalu@gmail.com