Kuna hadithi ambayo huwa naipenda sana. Nilisimuliwa na mwalimu wangu mmoja hivi wakati nipo sekondari. Mwalimu wangu alinisimulia kwamba hapo zamani kulikuwa na mtoto ambaye alipenda sana kufuga kuku na ndege pia. Siku moja, mototo huyu aliokota yai kwenye kiota cha ndege tai. Alilichukua yai lile hadi nyumbani ambapo aliyachanganya na mayai ya kuku aliyekuwa akilalia mayai.

Kuku Yule kwa bahati nzuri, alifanikiwa kuangua kifaranga cha tai. Kwa hiyo, kifaranga cha tai nacho kikawa sehemu ya vifaranga wa kuku Yule. Kwa kadiri walivyokuwa wanakua, Yule kifaranga wa tai alihisi kama kuna tofauti. Alihisi kuwa ana uwezo zaidi, pengine ya wale kuku aliokuwa nao kila siku na katika mazingira yale yale.

Tunaambiwa kwamba, nguvu kubwa kabisa katika vitu ni ile ya vitu visivyoonekana kwa macho. Hebu angalia kama joto, sauti, upepo, umeme na vingine. Hizi ni nguvu ambazo hazionekani, lakini ndizo zinazohesabika kuwa kubwa zaidi ya nyingi kuliko zinazoonekana.

Kwa binadamu, nguvu zisizoonekana ni pamoja na upendo, mawazo, matamanio, imani na vingine. Kwa hiyo, tai Yule mtoto alianza kuhisi tofauti kwamba, ana nguvu zaidi. Alianza kuamini kwamba, anaweza kufanya mambo makubwa zaidi. Alianza kuamini kwamba, hakuwa kuku, bali alikuwa tai mwenye uwezo mkubwa wa kupaa juu.
Hatimaye kwa kuamini kwamba angeweza kupaa, alianza polepole kujifunza kupaa na hatimaye kupaa kabisa. Kumbuka alipokuwa bado akiamini kwamba, yeye ni kuku na hivyo asingeweza kupaa kwa sababu ya maumbile, alishindwa kupaa na wala hakuwa na sababu ya kupoteza muda kujaribu kufanya hivyo.

Lakini alipohisi kuwa yeye ni tofauti na kuamini kwamba, angeweza kupaa, alianza kuelekea kwenye kile alichokiamini. Ni kweli, aliweza hatimaye kupaa kama tai wengine. Mazingira yalimfanya kuwa na imani ya aina Fulani. Lakini polepole alijitahidi kubadilisha imani hiyo. Alibadili imani ya kwamba yeye ni kuku na ameumbwa kutembea ardhini na siyo kupaa na kuwa na imani mpya, anaweza kupaa.

Kile ambacho mawazo yanakiamini, binadamu anaweza kukifanikisha. Kitu chochote kile unachokifiria sana katika mawazo yako uwe na uhakika utakipata. Hii ikiwa na maana kuwa, kile ambacho unakiamini ndani kabisa, hutokea na kuwa kama tunavyoamini katika maisha yetu ya kila siku.( Soma pia Hii Ndiyo Imani Unayotakiwa Kuwa Nayo Ili Kufanikiwa )

Hivyo basi jinsi tulivyo sisi, ni matokeo ya kile tunachokifikiria. Tunapofikiria kuwa sisi ni watu wa kabila Fulani, wa rangi Fulani na wa dini Fulani ama wa familia na ukoo Fulani duni, kwa hiyo hatuwezi, hivyo ndivyo itakavyokuwa. Utabaki hapo hapo na utaendelea kutokuweza mpaka ubadilishe mawazo yako uliyonayo.

Kama tukifikiri kwamba, sisi kwa sababu hatukusoma, kwa sababu hatuna ‘marefa’, kwa sababu hatufahamiki, tunapaswa kuishi maisha ya huku huku chini, ni lazima tutabaki huko chini, tutakuwa tuna kosea sana. Hata kama ikitokea tumesoma vipi, tuna ‘marefa’ na tunapata misaada kila kona, kama hatuamini katika kuweza, hiyo ni kazi bure.

Refa wa kwanza wa mtu, msaada wa kwanza wa mtu, usomi wa kwanza wa mtu, ni kuamini katika yeye kwanza. Mtu ambaye haamini katika yeye, hana anachoweza kukikamilisha maishani mwake. Ili uweze kufanikiwa zaidi, ni lazima uamini kuwa unaweza. Kama unafikiri na unaamini hivi katika maisha yako kuwa una uwezo wa kufanikiwa, tayari wewe ni tajiri.

Tukiamini sisi ni tai katika maisha yetu, ni ukweli usiopingika tutaruka na kufika kule tunakotaka. Tukiamini ni kuku hakuna tunachoweza, basi tutakuwa tumekwama. Tulio wengi ni tai na wala siyo kuku sema hatujijui, ingawa tunalelewa pamoja  na vifaranga wa kuku.

Wengi wetu tuna haja ya kuanza kujiuliza na kuuona uwezo wetu ndani ya kundi la wengi ambao wanaamini kwamba wao ni kuku na hawawezi kuruka. Kama tukianza kushtuka na kuona tofauti, kuona kwamba, tunajua kidogo na hivyo tunaweza kuruka, tutaweza tu nakufikia mafanikio makubwa tunayoyataka.
Nakutakia Ushindi Katika safari yako ya mafanikio, endelea kuembelea mtandao huu wa AMKA MTANZANIA kwa kuhamasika na kujifunza.

TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE.

IMANI NGWANGWALU – 0713 048 035/ingwangwalu@gmail.com