Tafiti nyingi zinaonesha kwamba kujiamini ni kiungo muhimu sana cha mtu kuweza kufikia mafanikio makubwa. Ukiangalia, watu wengi waliofanikiwa wanajiamini kwa kiasi kikubwa. Japokuwa kuna watu ambao wanajiamini ila hawana mafanikio na pia kuna watu ambao wana mafanikio makubwa ila hawajiamini kabisa. Pamoja na hayo, kujiamini kunakuongezea nafasi ya kufikia mafanikio mara kumi zaidi kuliko ambavyo ingekuwa kama ungekuwa hujiamini.

Ni kipi kinaanza, mafanikio au kujiamini? Mafanikio na kujiamini ni vitu ambavyo vinategemeana sana. Ukujiamini utaweza kufikia mafanikio makubwa na ukiwa na mafanikio unajiamini zaidi. Mwanzoni unahitaji kujiamini ili uanze kufikia mafanikio. Baada ya hapo mafanikio na kujiamini kunakwenda sambamba.

Mchango wa kujiamini kwenye mafanikio.

Hivi ndivyo kujiamini kunavyoweza kukusaidia kufikia mafanikio makubwa.

1. Unapata kile unachowekea mkazo. 

Kama mtu ataamini kwamba hawezi kufikia mafanikio, hatofikia mafanikio. Ataishi maisha yake kutimiza utabiri wake huo wa uongo na hivyo kushindwa kabisa kufikia mafanikio. Kujiamini kunamfanya mtu kuondokana na mawazo ya kutokujiamini hivyo kuwa na nafasi nzuri ya kufikia mafanikio makubwa.

2. Mafanikio yanatokana na kujaribu mara nyingi.

Mpaka uje kufikia mafanikio makubwa unahitaji kujaribu mara nyingi sana. Utaanzisha kitu kitashindwa, utaanzisha tena na kitashindwa na utaendelea kufanya marekebisho huku ukiendelea kushindwa. Kama hujiamini itakuwa rahisi sana kwako kukata tamaa na kuachakile unachofanya. Hiki ndio kinafanya watu wengi washindwe kufikia mafanikio makubwa. Kama unajiamini utaendelea kufanya kile ulichopanga kufanya hata kama unakutana na wakati mgumu. Kwa sababu unapojiamini unajua ya kwamba kinashosababisha ushindwe sio kwa sababu unauwezo mdogo ila kwa kuwa mwanzo wowote huwa mgumu.

3. Kujiamini na mafanikio.

Ili uweze kufikia mafanikio makubwa unatakiwa kuamini kwamba unaweza kufikia mafanikio makubwa. Na pia unahitaji kuaminika na watu ambao wanakuzunguka ili waweze kukupa ushirikiano unaohitaji ili kuweza kufikia mafanikio makubwa. Ili uweze kuamini kwamba unaweza kufikia mafanikio makubwa unahitaji kujiamini wewe mwenyewe binafsi. Na pale unapojiamini wewe mwenyewe hata watu wanaokuzunguka nao wanakuamini.

4. Kujiamini, sononeko na mafanikio.

Watu wanaojiamini nao hupata sononeko(depression) lakini haliwaathiri sana na huisha haraka. Kukosa kujiamini ndio chanzo kikubwa cha sononeko na huwasababishia watu kushundwa kabisa kuendelea na malengo na mipango yao. Sononeko hutokea pale mtu anapopoteza matumaini ya kufikia malengo yake. Ila kama unajiamini utakuwa na uhakika kwamba unaweza kufikia malengo yako na hivyo kuweza kuondokana na sononeko.

5. Kujiamini na kukataliwa.

Moja ya kikwazo kikubwa cha watu kufikia mafanikio ni hofu ya kukataliwa. Na sababu namba moja ya watu wengi kukata tamaa ni kukataliwa. Ukiangalia utaona watu wote ambao wamefikia mafanikio makubwa waliwahi kukataliwa mwanzoni. Pamoja na kukataliwa hawakukata tamaa kwa sababu walijiamini kwamba wanaweza na hakuna anayeweza kuwazuia. Unahitaji kujiamini ili uweze kuondokana na hofu ya kukataliwa na uweze kuendelea na mipango yako hata baada ya kukataliwa.

Kujiamini ni kiungo muhimu sana cha kufikia mafanikio makubwa. Kama kweli unahitaji kufikia mafanikio makubwa kwenye maisha yako ni muhimu sana kujijengea tabia ya kujiamini. Kujua jinsi ya kujijengea kujiamini soma makala hii iliyopita. Na pia soma makala hii kujua mazoezi ya kujijengea kujiamini.

Nakutakia kila la kheri katika kufikia mafanikio makubwa.

TUPO PAMOJA, TUTAKUTANA KILELENI.